BAADHI ya wakazi wa jiji la Mwanza, akiwamo Hakimu mmoja wa Mahakama ya Mwanzo wamelalamikia maamuzi ya Halmashauri ya Jiji la Mwanza kwa kuwekewa alama za ‘X’ katika nyumba zao bila kushirikishwa, wakielekeza malalamiko hayo kwa Meya Josephat Manyerere (Chadema) wakidai kwamba anatumia vibaya madaraka yake kwa kukiuka taratibu sheria za ardhi.
Hii ni mara ya pili baada ya wakazi wa jiji hilo kumtuhumi Meya Manyerere kwamba alishirikiana na waumini wenzake wa kanisa la Waadventista Wasabato (SDA) Majengo katika mtaa wa Mabatini Jijini hapa kujenga jengo la gorofa la Kanisa hilo bila vibali.
- Meya wa Jiji la Mwanza, Josephat Manyerere
Habari zilizoifikia FikraPevu zinadai kwamba safari hii, uongozi wa jiji chini ya Meya huyo umetoa maamuzi ambayo pamoja na mambo mengine, yameibua manung’uniko pamoja na hofu kuhusiana na ardhi miongoni mwa wakazi wa mtaa wa Bwiru-Mnarani, wilaya ya Ilemela Jijini hapa.
“ Sisi ni watu wa kuagizwa tu; sasa wewe ungelifanyaje iwapo Meya anakupigia simu na kukuagiza “ alidai mmoja wa wafanyakazi wa idara ya ardhi, kwa sharti la kuotajwa jina.
Alidai mara kadhaa, Meya alikuwa akiwapigia simu ili wakaweke alama ya X katika baadhi ya nyumba zilizoko katika mtaa wa Bwiru-Mnarani.
Baadhi ya wakazi wanadai kwamba kuna harufu ya ukabila na udini hatua ambayo inadaiwa kuongeza idadi ya malalamiko, migogoro pamoja na kesi zinasababishwa na tabia ya ukiukwaji wa taratibu na sheria ya ardhi jijini.
“ Kwa mfano, wiki iliyopita Meya alishinikiza watumishi wa halmashauri ambao walifika katika mtaa wa Bwiru-Mnarani na kuweka alama ya X katika baadhi ya nyumba, ikiwemo nyumba za Mheshimiwa Hakimu, Isaack Mbolile,” kilidai chanzo chetu cha habari kwa sharti la kutotajwa jina.
Habari zinasema wamiliki wa nyumba hizo bado hawajaelezwa sababu za kuweka alama za X Katika nyumba zao.
Inadaiwa kuwa nyumba zilizowekwa alama ya X ziko nje ya eneo la barabara kuu, kwa mujibu wa maelezo pamoja na ramani iliyooneshwa kwa wananchi hao, zaidi ya mwaka mmoja uliopita.
Habari zinadai kwamba kila mwaka wamiliki wa nyumba zilizowekwa alama ya X wanalipa kodi ya majengo kama kawaida.
“Sasa inakuwaje jiji wapokee kodi ya nyumba ambazo ziko ndani ya hifadhi ya barabara; tena kwa zaidi ya miaka mitano sasa” kilidai chanzo cha habari.
Alipoulizwa, Manyerere alikiri kupokea malalamiko kutoka kwa baadhi ya wakazi wa Mtaa wa Bwiru-Mnarani .
Hata hivyo, Meya huyo hakuwa tayari kutoa ufafanuzi juu ya malalamiko hayo huku akisisitiza kwamba yeye hafanyi kazi kwa itikadi za dini na ukabila.
Alikiri pia kwamba jiji limeagiza nyumba hizo ziwekewe alama ya X, wakati ofisi yake ikiendelea kufanya madai yaliyofikishwa ofisini kwake.
“Ni kwamba mimi nimeletewa malalamiko ofisini kwangu ; na siyo lazima niwasiliane na wenye nyumba kabla ya kuweka alama ya X katika nyumba zao,” alisema Manyerere.
Alidai yeye ana uwezo wa kufanya maamuzi yoyote juu ya malalamiko yanayofikishwa ofisini kwake.
“Unajua, mabaraza ya ardhi yana kazi zake; na pia mimi ninaweza kuchukua uamzi wowote ninaoona inafaa dhidi ya malalamiko yanayonifikia ofisini yangu “ alisema
Kaimu Mhandisi wa Halmashauri ya Jiji, Victre Mashamba alikataa kuzungumzia suala hilo kwa madai kuwa yeye siyo msemaji.
Suala hilo ninalifahamu; lakini mimi siwezi kulizungumzia kwa vile siyo msemaji wa Halmashauri. Kamuulize Meya ama Mkurugenzi Mtendaji,” alisema Mashamba.
Alipoulizwa, Makamu mwenyekiti wa mtaa huo, Misana Mwanga, alikiri juu ya kuwepo kwa suala hilo .
Alikiri pia kwamba yeye alikuwa amefuatana na watumishi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, wakati zoezi hilo likitekelezwa.
“Ni kweli ninafahamu kwamba nyumba hizo ziko nje ya eneo la barabara na kwamba mimi nilikuwepo wakati jiji wanaziorodhesha nyumba ambazo zimepitiwa na barabara ya mtaa,” alikiri makamu mwenyekiti huyo.
Alidai kuwa hawezi kuzungumzia suala hilo kwa sababu aliombwa na wafanyakazi wa Jiji ili awaoneshe ziliko nyumba walizokuwa wameagizwa kuziwekea alama ya X.
Alikiri pia kwamba nyumba karibu zote katika mtaa huo zimejengwa bila vibali, isipokuwa nyumba za biashara.
“Mimi ninajipanga kwenda mahakamani;… kwamba kitendo cha kuweka alama za X katika nyumba zangu ni cha kunidharirisha mbele ya jamii. Sijashirikishwa kabla ya hatua hiyo; na pia wakati wote nimelipa kodi za majengo kama kawaida” alisema mmojawapo ya watu ambao nyumba zao zimewekwa alama ya X,” alisema Issack Mbolile, ambaye ni hakimu Mahakama ya Mwanzo Usagara, Msungwi mkoani hapa akisisitiza kuchukua hatua dhidi ya walioweka alama za X katika nyumba zake.
Alidai ramani aliyonayo inaonesha kuwa viwanja vyake viko nje ya eneo la baarabara na kwamba njama hizo zimefanywa na watu wachache ambao wanalenga kumchafua .
Habari hii imeandikwa na Juma Ng’oko, Mwanza
Mimi ni mkazi wa mwanza, mzee wangu ana kesi na mpangaji wake kwa muda wa miaka mitano sasa ankaa kwenye nyumba bila kulipa kodi na kesi iko mahakama ya ardhi na inaukumiwa visivyo kulingana na hakimu na mshitakiwa wanavyopanga. je mtanisaidia vipi kujua mwenendo wa sheria za haki za kitanzania katika kumiliki haki za binaadam bila kukiuka haki za kibinadam.