IKIWA imebaki takribani miezi minne mwaka wa fedha wa 2012/2013 umalizike, Ofisi ya Mratibu wa UKIMWI wa Halmahsuari ya wilaya ya Iringa haijapata fedha yoyote kutoka katika bajeti yake na hivyo kuathiri utekelezaji wa mipango yake.
Mratibu wa Ukimwi wa halmashauri hiyo, Odia Hezron alisema jumla ya Sh Milioni 138 ziliidhinishwa kwa ajili ya kazi za ofisi yake katika kipindi cha mwaka huo wa fedha.
“Hii ni changamoto kubwa kwasababu mipango mbalimbali inayohitaji fedha utekelezaji wake unakwama japokuwa nina imani fedha hizo zitakuja hata kama ni kwa kuchelewa,” alisema.
Alisema bajeti hiyo ni kwa ajili ya kukabiliana na matokeo ya UKIMWI, kutoa elimu, na uratibu wa shughuli mbalimbali za Ukimwi katika halmashauri hiyo.
Katika kukabiliana na matokeo ya Ukimwi, Hezron alisema wajawazito, watoto yatima na wanaoishi na Virusi Vya Ukimwi (VVU) wakiwemo watumishi wa halmshauri hiyo wamekuwa wakipata misaada mbalimbali.
“Kwa upande wa wajawazito na watumishi upo utaratibu wa kutoa fedha kwa ajili ya lishe ili ziwasaidie kuboresha afya zao na kwa upande wa watoto yatima tunao utaratibu wa kugharamia ada za shule huku wananchi wengine wakihamasishwa kuanzisha vikundi vya ujasiriamali na kupewa msaada,” alisema.
Alisema kwa njia ya elimu, halmashauri hiyo imekuwa ikiendesha kampeni za kukabiliana na janga hilo kupitia sinema, makongamano na mikutano kwa makundi mbalimbali ya kijamii.
Akizungumzia maambukizi ya virusi vya UKIMWI, Hezron alisema takwimu zinazotokana na upimaji wa hiari katika halmashauri hiyo zinaonesha kuwepo kwa asilimia 9 ya maambukizi.
Katika kipindi cha Januari na Desemba mwaka jana, jumla ya watu 10,414 walipima kwa hiari na kwa kupitia kampeni maalumu katika maeneo yenye mikusanyiko mikubwa ya watu na kati yao 943 waligunulika kuwa na maambukizi ya VVU.
Hata hivyo alisema utafiti wa kitaifa unaonesha wilaya hiyo ina asilimia 15.7 ya maambukizi ya VVU kama ilivyo kwa wilaya nyingine za mkoa wa Iringa na Njombe.