Hati mpya za kusafiria kupatikana kwa 150,000, wananchi walalamikia kupanda kwa gharama za usajili

Jamii Africa

Rais John Magufuli amezindua rasmi utolewaji wa hati ya kusafiria ya kielektroniki ambayo itakuwa inapatikana kwa sh. 150,000 na itadumu kwa miaka kumi.

Uzinduzi huo umefanyika leo jijini Dar es Salaam katika makao makuu ya Idara ya Uhamiaji ambapo Rais  Magufuli amesema kila mtanzania ana haki ya kupata hati ya kusafiria na ameitaka idara hiyo kutekeleza jukumu hilo kwa uadilifu.

“Passport (hati ya kusafiria) ni haki ya kila mtanzania. Wakati wa kupata passport umefika kwa wale walio na haki ya kupata mna wajibu wa kupata passport. Na ndio maana nimetaja na bei yake kwamba ni 150,000 tu si zaidi ya hapo, na passport hii ni ya kisasa”, amesema Rais Magufuli.

Mfumo huo mpya wa kielektroniki wa utoaji hati ya kusafiria  ni maboresho yanayofanywa na serikali ili kurahisisha upatikanaji wa huduma hiyo na kuimarisha usalama wa wananchi wanaoingia na kutoka nchini.

“Kama mnavyofahamu nchi yetu ina passport yake, mfumo ulioitengeneza ni wa zamani hivyo kuruhusu wahalifu kuforge (kughushi). Passport tunayozindua leo ni ya kielektroniki na itakuwa ngumu kugushi, itasaidia kupeleka taarifa bila passport yenyewe”, amesema Rais.

Awali gharama za upatikanaji wa hati hiyo zilikuwa sh. 50,000 lakini mfumo mpya umepandisha mara tatu zaidi na kuzua maswali kutoka kwa wananchi wakihoji ongezeko hilo la bei ambalo linaweza kuwa kikwazo kwa baadhi ya wananchi kupata hati kwa wakati.

Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba akizungumza kabla ya uzinduzi wa hati hiyo amesema  jambo hilo limekuja kwa wakati na hati hiyo itadumu kwa miaka kumi ili kutoa urahisi kwa wananchi kuitumia katika maeneo mbalimbali ya usafiri.

“Uzinduzi huu ni hatua muhimu sana katika mapambano dhidi ya uhalifu wa kimataifa unaowezeshwa na mfumo dhaifu wa mifumo isiyosomana hasa katika karne hii ya ukuaji wa teknolojia”, amesema waziri Nchemba na kuongeza kuwa,

“Gharama za Passport hii tumeweka kuwa ni Tsh. 150,000 ambayo ni sawa na Tsh. 15,000 kwa mwaka kwasababu tunakadiria passport hii itatumika kwa miaka kumi na tumeongezea kurasa nyingi kuliko zile zilizokuwepo na ni ya kisasa kuliko nchi nyingine”.

Akizungumza katika hafla hiyo, Kamishna Jenerali wa Uhamiaji , Dkt. Anna Makakala amesema sifa ya kupata hati hiyo ni kuwa na kitambulisho cha Taifa pekee kwasababu kina taarifa zote za muombaji.

Amesema mfumo huo utaunganisha mifumo yote ya utoaji huduma na kuwezesha mawasiliano yote ya kielektroniki katika idara za uhamiaji. Pia itaunganisha mifumo ya idara ya Uhamiaji na mifumo mingine ikiwemo  Vitambulisho vya Taifa, RITA, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Wakala wa Usajili wa Kampuni (BRELA) na mfumo wa kielektroiniki wa malipo ya serikali.

Ameongeza kuwa utasaidia kuhifadhi na kutunza kumbukumbu za raia wanaoingia na kutoka nchini na kurahisisha utoaji wa viza kwa wageni wanaoingia nchini. Pia kudhibiti maduhuli ya serikali.

Dkt. Makakala amebainisha kuwa mradi huo  wa kutoa hati utagharimu bilioni 127.2  na dhabuni imetolewa kwa kampuni ya IHD Global ya nchini Marekani kutoa huduma hiyo kwa kushirikiana na Idara ya uhamiaji.

Hata hivyo, Amesema hati za zamani zitaendelea kutumika hadi 2020 ambapo hazitaumika tena.

 

Maoni ya wananchi

Baada ya serikali kuzindua utolewaji wa hati mpya ya kusafiria ya kielektroniki, wananchi wametoa maoni yao juu ya mfumo huo.

Mchangiaji wa mtandao wa JamiiForums, Goodluck5  amesema “Tunawaomba uhamiaji wawe fair, kwa waombaji passport kubwa ambao wameshalipia Tsh 50,000/- lakini bado hawajapewa hati zao. Ni kwanini msiandae utaratibu mwingine kwamba hawa walipe tena Tsh 100,000/- ili jumla iwe Tsh 150,000/- inayohitajika kupata hati mpya za digital. Ikumbukwe malipo ya Tsh 50,000/- yamekwishafanyika na hati hizo bado uhamiaji kuzitoa”.

Mwandishi wa Vitabu, Yericko Nyerere ameandika kwenye ukurasa wake wa Twitter, “Paspoti ya kusafiria ni haki ya kila raia wa Tanzania, kwenye katiba pakiandikwa "haki", basi hiyo ni lazima. Serikali tumeipa dhamana ya kutuongoza na kusimamia haki hizo kikatiba sio kufanya biashara, Leo paspoti mpya itauzwa 150,000/=, badala ya zamani kuchangia 50,000/= tu”.

Mchangiaji mwingine JamiiForums aitwae Dublin ameandika “Dah! afadhali maana hizi za zamani zilikuwa zinafana na za nigeria sasa ndio uwe kwenye migration office au airport za huko ughaibuni wakikuona tu umeshika kajikitabu cha kijani wanakuita na swali la kwanza ni how is lagos! mpaka wachungulie weeee ndio utasikia you from Tanzania!!? Great work, Great visions (kazi nzuri, maono makubwa)”.

“Ni jambo jema kwa uhamiaji na nchi kwa ujumla lakini je katika system (mfumo) zao za digital (digitali) wana usalama wa kutosha kutunza hizo data maana kwenye huu mfumo kama hawako makini ndiyo itakuwa shida zaidi maana wajanja wa kudukua wapo wengi sana kwenye hilo eneo na watatumia kama njia mbadala wa kipato. Hongera Rais lakini wawezeshe kuboresha kitengo kizima cha ICT ili waweze kupamabana na wezi wa kwenye mitandao”, ameandika Kishalu kwenye mtandao wa JamiiForums.

1 Comment
  • Migration hongereni kwa kutuwezesha kupata passport za kidigital ili kuzuia wainaingia Nchini mwetu kiholela.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *