Idara ya misitu Mpwapwa yalia na uharibifu wa misitu

Kulwa Magwa

IDARA ya misitu katika wilaya ya Mpwapwa, imepaza sauti kulilia uharibifu wa misitu unaofanywa kwenye mapori ya akiba na misitu ya serikali.

Hata hivyo, imewataka watu waoendesha shughuli mbalimbali ndani ya misitu ikiwemo kukata miti, kufuata utaratibu kuacha kufanya hivyo, vinginevyo itawakamata na kuwachukulia hatua.

Ofisa Misitu wa wilaya hiyo, Devis Mlowe, anasema kuna mazowea yamejengeka miongoni mwa watu kufanya shughuli zinazoathiri ustawi wa misitu, suala ambalo limekuwa likichangia kupungua kwa mvua na kuzorotesha uoto wa asili nchini.

Devis Mlowe

Ofisa Misitu wa wilaya ya Mpwapwa, Devis Mlowe

Anasema wamegundua katika baadhi ya maeneo kuwepo kwa watu wanaoingia kwa wingi misituni ambako hukata miti, kuchoma misitu na kuharibu vyanzo vya maji vinavyoanzia sehemu hizo, wengi wao wakiwa watafiti wa madini.

“Mambo hayo yanapofanyika bila kufuata taratibu, yanaharibu misitu na sisi kama idara iliyopewa mamlaka ya kisheria na serikali, hatutakubali kuharibiwa kazi yetu, “anasema Mlowe.

Mkuu huyo wa idara anasema wameweka utaratibu wa kukabiliana na watu hao kwa kushirikiana na wadau wengine serikalini na mashirika yasiyokuwa ya kiserikali.

Anasema, uharibifu wa mazingira katika maeneo ya misitu unaweza kutishia upatikanaji wa mvua, iwapo utaachwa uendelee.

Kitaugimbi

Mandhari ya misitu inayozunguka mliima Kitaugimbi, uliopo Mpwapwa

“Tutaendelea kufuatilia kwa karibu uharibifu unaofanyika na kuwabana wanaofanya hivyo ili mwisho wa siku wilaya iwe na misitu mizuri, licha ya kwamba tunaujua ugumu wa tutakaokutana nao, lakini kwa ushirikiano na ofisi ya mkuu wa wilaya mambo yatakwenda vizuri, “ anasema Mlowe.

Kwa upande wake, Ofisa-Mratibu wa Tanzania Forestry Conservation Group (TFCG), ambalo ni shirika lisilo la kiserikali, Mopilio Mwachali, anasema watashirikiana na serikali kuhakikisha kuwa miti haikatwi hovyo kwenye maeneo wanayoyasimamia yaliyoko katika Kata ya Lumuma.

Mopilio Mwachali

Ofisa Mratibu wa TFCG, Mopilio Mwachali

Anasema shirika hilo lipo tayari kusaidia kushughulikia mambo ya kisheria, ikiwa ni pamoja na kuweka mawakili watakaohakikisha haki inatendeka dhidi ya waharibifu wa misitu.

Kwa mujibu wa sheria ya misitu ya mwaka 2002, inatoa adhabu kali kwa mtu au taasisi inayothibitika kuharibu misitu ikiwemo kifungo na faini na kwamba, iwapo wakati wa hukumu inasomwa na ile ya mazingira ya mwaka 2004, kiwango cha juu cha faini hakipungui au kuzidi sh. milioni 50 au kifungo kisichozidi miaka saba; ama vyote viwili kwa pamoja.

Pia kifungu cha 160 (1) na (2) cha sheria hiyo kinasisitiza mtu, kijiji au taasisi yenye maslahi ya kisheria ya ardhi inawajibika kulipwa fidia, ambapo haki hiyo inapaswa ilingane na thamani ya ardhi au miti iliyopotea au kuharibiwa na kuwa, thamani halisi ya ardhi huzingatiwa chini ya kifungu kidogo cha (1) cha sheria ya ardhi ya mwaka 1967 na sheria ya ardhi ya 1999.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *