Je, Talaka ni Suluhisho la matatizo ya Ndoa? – Sehemu ya Pili

Jamii Africa
Na Lady ViVa

Katika sehemu ya kwanza, nilikuacha msomaji na maswali kadhaa kuhusu nini kinaweza kufanyika pale mwenza wa ndoa anapofungwa. Sheria ya Ndoa ya 1971 inatamka wazi katika kifungu cha 67 kwamba wanandoa wataweza kukubaliana kuishi mbalimbali. Katika makubaliano hayo wanandoa wataweka bayana makubaliano yao na jinsi gani wamekubaliana kuishi mbalimbali na majukumu yao ya kutunza familia yatakuwa vipi. Endapo mahakama itaona kwamba kuishi mbalimbali siyo kwa manufaa hasa ya watoto basi makubaliano hayo yanaweza kutenguliwa.

(Kama hukusoma sehemu ya kwanza, inapatikana hapa )

Msisitizo uko kwenye “kukubaliana kuishi mbalimbali”. Katika kifungu cha 107 (2) (g) cha sheria ya ndoa,kinasema kwamba mwanandoa anaweza kudai kuwa ndoa imevunjika pasina shaka pale ambapo mwenza wake atakuwa amefungwa maisha au kwa kipindi kisichopungua miaka mitano  kwa kuzingatia urefu wa muda wa kifungo na pia aina ya kosa lililotendwa na mwenza huyo hadi kupelekea kufungwa. Bahati mbaya sana sheria imeiachia mahakama kuamua hayo mambo mawili – muda na aina ya kosa. Yatosha hata hivyo kusema kwamba ndoa inahitaji wawili hao waishi pamoja na siyo kuishi kila mmoja kivyake pasipo makubaliano.

Tukiangalia aina ya maisha watu wanayoishi siku hizi, ambapo wanandoa wanatafuta  fursa mbalimbali za biashara na kazi popote ili kuweza kujikimu kimaisha, tutaona kuwa wanandoa wanajikuta wakiishi mbalimbali.Cha kujiuliza ni kama wanakuwa wamekubaliana kuishi hivyo au la. Miaka ya nyuma mara nyingi waajiri walikuwa wakimpangia mwanamke kazi sehemu aliko mume, au mwanamke aliweza kuomba uhamisho au kukataa uhamisho ili awe pale alipo mume. Siku hizi tunaona waajiri wakipanga kazi kufuatana na mahitaji yao na siyo mahitaji ya wanandoa. Je, waajiri wanajua takwa  hili la kisheria? Na je, wakilijua na kulitekeleza ni nani atapata faida au hasara? Mwajiri anachoangalia ni mahitaji yake na siyo mahitaji ya wanandoa na kwa msingi huo, mke au mume hawezi kutoa masharti kwa mwajiri. Itabidi achague kufanya kazi pale mwajiri anapotaka au kupisha wengine wachukue nafasi hiyo.

Maisha ya ndoa yana changamoto nyingi ambazo zinaletwa na mahitaji  mbalimbali. Kuishi mbalimbali kwa wanandoa wakati mwingine siyo kwa kupenda bali ni kutokana na uwepo wa ulazima kufanya hivyo. Wanandoa wanatakiwa kuhangaika ili waweze kuzitegemeza familia zao. Miaka ya nyuma ilikuwa rahisi mwanaume kufanya kazi na mwanamke kukaa nyumbani kutunza familia. Siku hizi kipato cha mmoja tu hakitoshi, na hata pale wote wana vipato, bado inalazimika wakati mwingine wanandoa kusafiri vipindi virefu kikazi au hata kwenda  masomoni na kuziweka ndoa zao mashakani.

Ndoa nyingi zimeingia misukosuko hasa ya kusaliti pale wanandoa walipoishi mbalimbali. Ni sahihi kusema kwamba kuishi mbalimbali kwa wanandoa ni kihatarishi kimojawapo kinachoweza kupelekea ndoa kuvunjika. Kuishi mbalimbali huweza kutoa fursa kuanzisha mahusiano ya muda na hatimaye kuharibu uhusiano baina ya wanandoa na kusababisha ndoa kuvunjika. Mfano ni  Bwana H. ambae alikiri kwamba wakati mkewe alipoenda kusoma shahada ya pili, upweke ulimfanya aanzishe  mahusiano na msichana  wa kazi aliyebaki hapo nyumbani kulea watoto. Alifanya hivyo kwa vile alishindwa kubaki peke yake bila mkewe. Mkewe aliporudi, huyu bwana alisitisha yale mahusiano lakini yule msichana akawa na kiburi kisicho na kipimo. Ilipelekea kumwachisha kazi maana angeendelea kukaa nao huenda siri ingefichuka na yeye hakuwa tayari kwa hilo.

Nini kifanyike kunusuru ndoa zisivunjike na hatimaye kuishia kwenye talaka?

1.   Kuwa tayari kukabili changamoto

Inatia moyo kujua kuwa hakuna ndoa isiyo na matatizo au changamoto za namna moja au nyingine  kwa sababu maisha  ya ndoa yanahusisha watu wawili ( au zaidi kwa zile ndoa za mitala) ambao wamekutana ukubwani kila mtu akitokea kwenye malezi tofauti.Hilo peke yake latosha kuonyesha kwamba migogoro na tofauti lazima ziwepo.Ni vizuri mtu anapoingia kwenye ndoa aingie akijua kuwa ameingia kwenye changamoto na siyo paradiso.Utambuzi huu  utamfanya mwanandoa awe makini katika  kila anachokifanya akijua kuwa yuko na mwenzake anayeweza kuwa na mtizamo tofauti.Kipimo mara zote kiwe sitamtendea mwenzangu kile ambacho sitapenda yeye anitendee”.

2.   Uvumilivu na subira

Maisha ya ndoa yanahitaji subira ya hali ya juu na kujitoa au kujitolea kwa namna ya kipekee. Ubinafsi na umimi ndio chanzo kikubwa sana cha kusambaratisha ndoa. Ndoa inaweza kufanya maisha yakawa mepesi au magumu kutegemeana na wahusika wenyewe. Wepesi huja pale kila mmoja anapojitahidi kutekeleza wajibu wake ipasavyo. Hata hivyo wanandoa hawapaswi kuingia kwenye ndoa na mategemeo makubwa sana kiasi ambacho yasipofikiwa inakuwa ndio chanzo cha migogoro. Mwanamke anayeingia kwenye ndoa akitegemea kulelewa kama mtoto na kufanyiwa kila kitu na mumewe au mwanaume anayetegemea kumfanya mkewe kama mtumwa kwenye ndoa – ampikie, amfulie, amstareheshe nakadhalika atakuwa ameanza safari yake vibaya mno. Inabidi wahusika wajifunze kuishi na wenzao na kuwasaidia wasijisikie wanaelemewa na mzigo wa ndoa.Unapomfanya mwenzio aanze kutathmini ni kwanini akakuchagua wewe uwe mwenza wake wakati  wewe hujamfanya ajisikie unamuongezea thamani kwenye maisha yake ujue huo ni mwanzo wa matatizo.

Mara zote jitahidi kuwa “msaada” na siyo “mzigo” kwa mwenzio.Nimekumbuka kisa cha  Bi Siwezi (siyo jina lake) ambaye aliolewa na Bwana Jaribu akitegemea mume kumpa matumizi yake yote kwa vile hakuona ulazima wa kujibidisha kwa chochote ilhali mumewe ana uwezo kipesa. Mwanzoni aliyafurahia sana maisha kwa vile mume alimpa kila kitu alichotaka. Kadiri siku zilivyosonga mbele, pesa ikaanza kupungua na kuleta ugomvi wa mara kwa mara na hatimaye  ndoa ikavunjika. Kadhalika wako wanaume ambao hutarajia makubwa kama siyo maajabu kwa wake zao. Baba Samuel alijikuta kila mara akigombana na mkewe kisa hakutaka kula chakula alichopika msaidizi wa nyumbani.Mwanzoni mkewe alijitahidi kumtimizia alivyotaka lakini ikafika mahali mke akazidiwa na majukumu ya kikazi na watoto. Migogoro haikuisha.

3.    Kuwasiliana

Ni vizuri kila mara kuzungumza na kuwasiliana, kuambizana na kusahihishana kwa upole pale jambo linapokuwa haliendi sawa. Hata hivyo siyo kila jambo unatakiwa kulilalamikia. Wanandoa wapeane nafasi ya “kuwa wao” bila kuhofia kukosolewa. Hakuna kitu kibaya kama kuishi kwenye hofu ya kukabiliwa na kukosolewa, lawama au shutuma kila wakati. Tukumbuke kuwa wanandoa wametoka katika mazingira na malezi tofauti na hata wakati wanachumbiana huenda kuna vitabia ambavyo vilijitokeza lakini wakadhani watasahihishana mbele ya safari. Tukumbuke kuwa wakati mwingine tabia haina dawa.Inaweza kubadilika au isibadilike. Rejea kipengere 2 hapo juu. Uvumilivu unahitajika.

4.    Kuwa mwepesi kusamehe  

Tukumbuke kwamba maisha ya ndoa yana changamoto kama ilivyo maisha mengine yawe ya kazini, shuleni na kadhalika. Walipo binadamu na makosa yanakuwepo. Hakuna mtu asiye na makosa au asiyejikuta akimuudhi mwingine. Hata kwa wazazi ilikuwa ni kawaida kukosa, kukanywa, wakati mwingine kuadhibiwa lakini mwisho wa siku msamaha ulitolewa.

Ndoa nyingi zimevunjika shauri ya ukosefu wa msamaha. Mtu anapokosea, ustaarabu unasema kuwa kubali kosa, kiri na uombe msamaha. Wanandoa wengi hawako tayari kuupitia huo mchakato. Huwa na kiburi sana kusema “SAMAHANI” mwenzangu nimekukosea. Kitendo cha kuomba samahani huwa ni kigumu sana kwa wanandoa. Katika maandishi au hata simulizi na mazungumzo, watu wanasema kwamba  wanaume wengi huona ugumu sana kuwaambia wake zao samahani kwani inatafsiriwa kama udhaifu! Kuna ukweli kwamba kusema samahani ni kujishusha, lakini kitendo hicho cha kujishusha ndicho kinachopelekea kujenga imani na upendo kwa yule aliyekosewa. Pia huwa kama kinga dhidi ya kurudia tena kosa kwa sababu mtu akifikiria kujishusha tena mara nyingine, atajitahidi sana isitokee hasa kwa makosa yale makubwa. Usipoweza kusema samahani hasa kwa makosa yale makubwa, ujue nawe utaweza kuja kutendwa kwa kiwango kilekile na kufanya ndoa yenu iingie mgogoro mkubwa zaidi na hatimaye kusambaratika.

Wapo wanawake ambao nao hawasemi samahani kwa waume zao kwa sababu ya kiburi tu. Hujishauri sana kabla hawajasema samahani.Hii ni tabia mbaya isiyofaa katika ndoa. Kwa yule anayeombwa msamaha, naye ajifunze kuwa mwepesi kurudisha moyo na kumsamehe mwenzake tena bila masharti. Kuna wanandoa ambao japo wanaombwa msamaha, huwa wagumu kama jiwe kusamehe. Watajivuta kwa miezi ati wamechukia sana na wanatafakari wasamahe au hapana. Tabia hii haileti suluhu bali hukaribisha mengine mabaya. Kumbuka unapomfanya mwenzio ajisikie mkosaji muda mrefu bila kupata msamaha, ubinadamu utamfanya atafute amani mahali pengine. Amani hiyo inaweza kupatikana sehemu ambayo ni hatari kwa ndoa.Wiliam ( siyo jina lake)  alijikuta anashinda nyumba ndogo hadi akazaa nje kwa vile hakutaka kutumia muda  mwingi na mkewe aliyekuwa kakasirika kwa miezi kadhaa kisa mume alimpiga na hakuwa tayari kumsamehe.Hapa tunaona kosa moja likizaa lingine kwa vile tu msamaha ulikosekana.

5.   Jifunze kusahau

Tujiulize kwanini Mungu ameweka “kusahau” katika maisha ya mwanadamu.Hebu fikiria ni mambo mangapi machungu tunapitia katika maisha. Tunafiwa na ndugu na wapendwa wetu. Tunaugua na kupata maumivu makali.Akina mama wanazaa kwa uchungu usio kifani. Tunapitia vipindi vigumu vingi katika maisha. Ingekuwa hatupati kusahau, ingekuwaje? Nadhani tungeishi maisha mafupi mno maana hakuna mtu angetamani kuendelea kuishi tena maana hayo machungu yasingevumilika. Mwanandoa unayeng’ang’ana kumhesabia mwenzio makosa na kumkumbushia kila mara makosa aliyoyafanya huko nyuma hata pale alipokuomba msamaha unafikiri unajenga au unabomoa? Kukubali kuachia mambo mengine yapite inakupa wewe nguvu ya kuendelea kuishi maisha ya amani. Wanandoa wanapaswa kujizoeza kusahau. Kusahau kutakuongezea siku za kuishi pia.

6.   Usirudie kosa

Wahenga walisema “ kukosa siyo kosa, kosa ni kurudia kosa”. Mwanandoa unapokuwa unarudia kosa lile lile kila mara unatarajia mwenzio ana moyo wa jiwe? Umemsaliti kakusamehe, bado unaendelea tena na tena. Leo kakufuma na Mary, kesho na Fatuma, unadhani namba 4 na 5 hapo juu itafanya kazi? Mwanamke unazurura hukai nyumbani unakesha na mashosti kwenye viwanja vya starehe kama  vile hujaolewa na unatarajia mumeo asikasirike? Ukionywa hujirekebishi. Ndoa itaacha kuvunjika?

 

Hitimisho

Tunaona kabisa kwamba visababishi vingi vya ndoa kuvunjika vinaweza kuepukika kama wanandoa wataweza kujitambua na kujua kuwa ndoa inahitaji kazi ya ziada ili isimame. Wanandoa wakiweza kujifunza kuwa wavumilivu na kujishusha badala ya kujikweza basi ni dhahiri kuwa ndoa itaweza kudumu. Kutambua hilo kutawafanya wajitahidi kuvumiliana na kuchukuliana kwa upole na kupunguza ule msukumo wa kutafuta talaka.

Cha msingiIshi maisha yako ya ndoa kwa akili!

5 Comments
  • Lady Viva, hakuna maisha mazuri kama ya ndoa imara.Tatizo kubwa la ndoa za siku hizi,zimekuwa zikiiga sana maisha ya Egoli,lakini tu mimi nikate story kwa kusema siraha kubwa ya doa ni kuishi kwa kumtumainia MUNGU,kama wana ndoa watakuwa hai kiroho basi ndoa nyingi sana zitapona sababu hakuna kwazo lilo jipya kwenye viatabu vya MUNGU,kila tatizo lina majibu ndani yake.Niwaase tu wana ndoa wajitahidi kuishi maisha ympendezayo MUNGU.

  • mabadiliko muhimu, ndo sio lazima na ndoa si upendo, ndoa zilianzishwa na taasisi za kidini, kuna watu zaidi ya billioni tano duniani… kwa nini uishi maisha yakona mtu mmoja tu, siku hazigandi na maishani mara moja na sio mbili, Binafsi siamini kama mungu yupo ila inasaidia kwa baadhi ya watu kuogopa kutotenda mabaya, be happy with or without marriage

    • Brother, life is the way u choose it, and you are the one to choose the colour of your life. Vyovyote vile ulivoaminishwa lakini Mimi nakuhakikishia kua MUNGU YUPO. Naomba ujitahidi sana uamini hili. Usiwe mbishi sana.
      Ebu fikiria swali hili, Hivi unajua EXACTLY DAKIKA sekunde gani unahama from being conscious into deep sleep and back to activeness after some hours?
      If you can have the answer, basi unaweza kujua mda utakapoacha uhai na kuwa mfu.
      But if U have no answer, basi amini kuna nguvu KUU ambayo ipo some where and believe GOD IS THERE

  • duuuuu!mshkaji kweli umepinda hata miungu ya kienyeji111NDOA LAZIMA IWE NA UPENDO TUUU!hakuna cha uvumilivu wala nini!kama hakuna upendo ni kuivunjilia mbali kwani inaleta maumivu na baadaye yanaweza kutokea ya KANUMBA
    Ushauri wa bure hata kama unampenda mtu vipi lakini yeye haonyeshi mapenzi achana naye kwa gharama yeyote ile

    • Ila kumbuka unaposema UPENDO huwezi kuutenganisha na neno UVUMILIVU. Tatizo ni tafsiri wanayoichukulia wengi haswa unapoongea neno UPENDO ukaweka sura ya kike na kiume pamoja. Maana unayoipata utaambiwa upendo ni Mapenzi…”

      UPENDO ni NINI HASWA? ni wigo mpana sana unaojumuisha UVUMILIVU, MATUMAINI, KUSTAHIMILI.
      Mtu mwenye upendo HAJIVUNI, HANA UBINAFSI, ANAWAJALI WENZAKE, NI MKARIMU, ANAWAJIBIKA, HANA KIBURI.
      Kwa ujumla wake yeye ni MTU WA WATU, ni mcha Mungu

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *