Kagera: Mtaalam aonya athari za kisaikolojia baada ya tetemeko

Jamii Africa

Matukio yanayohusishwa na athari za kisaikolojia baada ya tetemeko la ardhi la Septemba 2016 yanaendelea kuibuka katika maeneo tofauti mkoani Kagera huku waathirika wengi wakiwa ni wananchi wenye kipato cha chini, FikraPevu inaripoti.

Mtaalam wa Saikolojia Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Ignatia Mbatta, ameonya uwezekano wa ongezeko la matukio hayo na kutaka wananchi wapewe  msaada wa kisaikolojia baada ya kushuhudia pigo hilo.

Baadhi ya matukio ya hivi karibuni ambayo hayakuzoeleka kabla ya tetemeko la ardhi ni mwanamke aliyetupa mtoto kando ya barabara wilayani Misenyi, na mwanafunzi wa shule moja  ya msingi katika Kijiji cha Burifani  amejeruhiwa vibaya kwa moto mikononi ikiwa ni adhabu aliyopewa  na mama yake kwa tuhuma za kuiba shilingi 700.

Daktari muuguzi wa Kituo cha Afya Bunazi, Benjamin Eyakuze, amekiri kumpokea mtoto huyo akiwa na maejeraha makubwa baada ya kuunguzwa kwa moto na kuwa hatua ya kwanza walimfanyia usafi.

Mmoja wa ndugu wa mwanamke anayetuhumiwa aitwaye Silvia Mugarula alisema kuwa mwanamke huyo anaishi na watoto watano na nyumba yao ilikuwa haijafanyiwa ukarabati baada ya kuathiriwa na tetemeko la ardhi. 

Tukio jingine ni la mjamzito Atumaini Elias aliyejifungulia uwanjani baada ya kukataliwa kupokelewa na wauguzi katika Zahanati ya Nshambya mjini Bukoba kwa madai kuwa hawakuwa na uwezo wa kumhudumia.

Kwa mujibu wa Elias Rwiza ambayer ni mume wake, baada ya kufika katika zahanati hiyo waliwakuta wauguzi wawili ambao walishauri mjamzito huyo apelekwe Hospitaii ya Mkoa kwa kuwa hawakuwa na vifaa vya kumhudumia.

FikraPevu imeelezwa kwamba, tukio jingine ni kufariki dunia kwa Kudra Wincheslaus akiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Bukoba wakati akisubiri kutajwa kwa kesi yake ya kukutwa na dawa za kulevya aina ya bangi.

Taarifa iliyothibitishwa na Polisi mkoani Kagera inasema Kudra alifariki dunia baada ya mshtuko na moyo kushindwa kufanya kazi.

Akihojiwa na FikraPevu kuhusu tukio la mwanamke aliyetupa mtoto wake kando ya barabara wilayani Misenyi, Mbatta alisema siyo sahihi kutanguliza lawama bila kuangalia pigo la tetemeko la ardhi ambalo linaweza kuwa limeleta madhara kisaikolojia.

“Mapigo makubwa kama tetemeko la ardhi yanaweza kuleta mshtuko mkubwa na madhara kisaikolojia, wengine wanakuwa na msongo wa mawazo, unaweza kuona matukio yenye sura tofauti ambayo hayakuwepo kabla,” alisema Mbatta.

Alisema eneo lililopata mapigo kwa nyakati tofauti kama Mkoa wa Kagera ni muhimu wananchi wakapata tiba ya kisaikolojia huku akibainisha hata watoto wadogo waliosikia kishindo cha tetemeko wanaweza kuathirika hata kuwa na tabia zisizo za kawaida nyumbani na shuleni.

Pia alisema mwanamke huyo aliyemuacha mtoto wake kando ya barabara na siyo kichakani asiukumiwe na jamii kuwa inawezekana alikuwa na aina fulani ya pigo lililomgusa na kuwa juhudi zielekezwe kuwapatia wananchi huduma ya kisaikolojia.

“Hakuna mwanamke anayependa kutupa mtoto, mbona hakumuua? Jamii isihamaki, tuangalie mtu na mazingira yanayomzunguka kwani wapo vijana wenye msongo wa mawazo na yanaweza kuendelea kuwepo matukio kwa sura tofauti,” alifafanua Mbatta.

Vilevile alisema baadhi ya watoto waliokuwa wanafanya vizuri darasani tabia zao zinaweza kubadilika ghafla na wengine kuanza kugombana mara kwa mara jambo linaloweza kuchangiwa na mshtuko waliopata.

Mtaalam huyo anabainisha kuwa madhara ya kisaikolojia kwenye eneo lililopata pigo mara nyingi hutokea kipindi cha kuanzia miezi sita na kuwa athari zinaweza kuwa kubwa zaidi hasa kwa Mkoa kama Kagera ambao wananchi wameshuhudia majanga kwa nyakati tofauti.

 

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *