Uvuvi katika Ziwa Victoria, umekuwa ukihusisha kambi nyingi za wavuvi zilizosheheni idadi kubwa ya wavuvi wenye umri mkubwa na mdogo wanaokadiriwa kufikia 182,741 huku kukiwa na vyombo vya uvuvi vinavyokadiriwa kufikia 28,470 (hii ni kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi ya 2012/2013).
Pamoja na ukweli kuwa zao la samaki na sekta ya uvuvi kwa ujumla, huchangia katika upatikanaji wa lishe bora, ajira, kipato kwa wananchi na kwa taifa, hivyo kuchangia sana katika kuondoa umasikini kwa umma; lakini licha ya faida yote hiyo kazi hii kwa huku imegeuka janga.
Janga hili linatokana na wanafunzi wa kike na kiume kukacha na wakati mwingine kuacha shule kabisa na kujitumbukiza kwenye kambi hizo za wavuvi, kutokana na sababu mbalimbali; kubwa ikitajwa kuwa ni umasikini.
Kufuatia hali hiyo, mwandishi wa makala hii amepata nafasi ya kufanya uchunguzi kwenye baadhi ya kambi zinazotajwa kuathiriwa zaidi na hali hiyo, ambapo ametembelea kambi mbalimbali zilizoko katika fukwe za visiwa vya Rukuba, Mroba na Masakala.
Ziara hiyo ya uchunguzi pia ilimchukua hadi visiwa vya Ryamgasile, Iriga, pamoja na fukwe maarufu za Bukima na Burungu, maeneo yote hayo yakiwa katika wilaya za Musoma vijijini na Butiama mkoani Mara, ambako alipata nafasi ya kuhojiana na wavuvi wenyewe, wanafunzi, viongozi wa serikali, maofisa wa elimu, walimu na wazazi.
Katika uchunguzi huo, pamoja na mambo mengine amebaini kuwepo kwa tatizo la utumikishwaji na ajira haramu za watoto kwenye baadhi ya kambi za wavuvi, sambamba na ngono zisizo salama, mikesha ya madisco na miziki ya kienyeji maarufu kama ‘Mazinduke’ bila kusahau mikesha ya picha za ngono.
Uchunguzi huo pia umewashuhudia baadhi ya wavulana wakiwasaidia wavuvi kuwaondoa samaki kwenye nyavu, kushona na kurekebisha nyavu; huku wenzao wa kike wakijishughulisha na kuwapikia wavuvi, kusaga unga na kwenda kuchanja kuni kwa ajili ya matumizi ya kila siku kwenye kambi hizo za wavuvi.
Nyamweko Mjinja (13) na Nyakaji Robert (15) ni wanafuzi wa Shule ya Msingi Burungu, ambao niliwashuhudia wakifanya maandalizi ya chakula kwa ajili kambi moja ndogo ya wavuvi iliyoko Burungu, ambapo walidai kuwa hawafanyi uchuuzi wa chakula bali wanafanya kazi ya kupika katika kambi hiyo kwa ujira.
“Huwa tunawapikia wavuvi chakula na kusenya (kuchanja) kuni…,wakitupatia pesa tunatumia kununua nguo na mahitaji mengine;..tunalazimika kufanya hivyo kwa sababu wazazi hawana pesa ndiyo maana hatuendi hata shuleni.” anasema Nyakaji huku akiungwa mkono na mwenzake.
Kwa mujibu wa wanafunzi hao; wanadai wamekuwa wakilipwa ujira wa kati ya shilingi elfu mbili na elfu tatu kwa siku kwa ajili ya kazi hizo, huku pia wakiambulia samaki kidogo kwa ajili ya matumizi ya nyumbani, hali inayowashawishi baadhi ya wazazi wasio na uwezo, kufumbia macho utoro wa watoto wao shuleni.
Shughuli zote hizo ni kwa malipo kiduchu ya kati ya sh. 1500/= hadi 2000/= kwa siku na samaki kidogo kwa ajili ya matumizi nyumbani, huku wenzao wa kiume wakidaiwa kujipatia ujira wa kati ya shilingi 4,000 na 5,000 kwa siku kwa kusaidia uvuvi, kufua nyavu na kuzikarabati.
Kwakuwa wakazi wengi wa maeneo yanayopakana na kambi za uvuvi, huendesha maisha yao kwa kutegemea shughuli za uvuvi, hali hiyo imeonekana kuwavutia siyo tu wanafunzi, bali hata walimu wao ambao baadhi wanamiliki zana za uvuvi ikiwa ni pamoja na kumiliki baadhi ya kambi za kuvulia samaki, hivyo kwa kiasi fulani kuathiri ratiba za masomo.
“Hata walimu tuna zana zetu za uvuvi kama sehemu ya kujiingizia kipato cha ziada ingawa haihusiani na ratiba yangu shuleni…, bahati mbaya hapa kwetu wanafunzi wengi wamekuwa watoro na wengine hata kuacha shule kwa sababu ya kushamiri kwa shughuli za uvuvi na tatizo la umasikini.” Anasema mwalimu Malima Ng’aranga wa Shule ya Msingi Burungu.
Hali kama hiyo pia iko katika kisiwa cha Rukuba hasa Shule ya Msingi Rukuba yenye wanafunzi 800, ambapo inadaiwa karibu asilimia 20% ya wanafunzi ama ni watoro wa kudumu ama wameacha shule kabisa kwa sababu ya kukimbilia kwenye kambi za wavuvi.
“Unajua kambi hizi za wavuvi ni hatari sana kuwa jirani na shule, wanafunzi wanapewa mimba, wanakesha kwenye miziki na picha za ngono…, hapa shuleni tuna wanafunzi takribani mia nane lakini zaidi ya 160 hawaonekani shuleni kwa sababu kama hizo.” Anasema mwalimu Hamisi Maiga.
Aidha kumeripotiwa pia kuwepo kwa vitendo vya ngono, mimba zisizotarajiwa na maambukizi ya magonjwa ya zinaa miongoni mwa wanafunzi, ambapo takwimu zinaonesha katika shule mbili za msingi za Majita na Irugwa pekee, zaidi ya wanafunzi 15 walishindwa kumaliza shule kwa sababu za ujauzito katika kipindi cha kati ya mwaka 2011 na 2013. Hii ni kwa mujibu wa walimu wakuu wa shule hizo; Mwalimu Raymond kimaro (Majita) na Victor Luginya (Irugwa).
Kulingana na hali aliyoishuhudia mwandishi huyu ni kwamba, mikesha kwenye madisco na picha za video za ngono, hutawaliwa kwa kiasi kikubwa na baadhi ya wanafunzi wa kike na kiume, sanjari na wavuvi wanaotumia kila aina ya kilevi kutokana na vipato vikubwa vya pesa zinazotokana na shughuli za uvuvi.
John Mwanjara ni mmiliki wa Duka la Dawa Muhimu katika kisiwa kikubwa cha Irugwa; yeye anasema kuwa wateja wake wakubwa huja kununua dawa zinazohusiana na magonjwa ya zinaa, huku akitanabaisha kwamba matumizi ya mipira ya kuzuia uzazi (condom), ya kiume na kike ni madogo sana.
“Nimekuwa naifanya biashara hii ya kuuza madawa ya binadamu kwa muda mrefu sana hapa kisiwani, lakini licha ya kushamiri kwa vitendo vya ngono na ulevi bado matumizi ya kinga ya ngono ni madogo sana…, hapa siyo salama …huwenda hata maambukizi ya ukimwi yakawa ni makubwa.” Anasema Mwanjara.
Nilitinga ofisini kwa Afisa Mtendaji wa Kata ya Bukima, kutaka kujua serikali kwa upande wake inalizungumziaje tatizo hilo; ambapo pamoja na majibu mengine, afisa huyo alikiri kuwepo kwa changamoto hiyo kwa wanafunzi na walimu wanaopakana na kambi za wavuvi.
Aidha alilalamikia pia kutokuwepo kwa Vituo vya Polisi karibu na maeneo hayo ya kambi za wavuvi, jambo linalopelekea baadhi ya watu kutokujali sheria na amri za serikali, licha ya kuwa wapo baadhi ya watendaji wadogo wadogo wa serikali ambao hujinufaisha kutokana na kambi hizo, hivyo kujikuta wakishindwa kuchukua hatua yoyote dhidi ya wavuvi wanaokiuka sheria za nchi.
“Ni kweli tunazo taarifa za matukio kama hayo huko kwenye kambi za wavuvi, lakini sasa baadhi ya wazazi na watendaji wadogo wadogo wa serikali, wamekuwa wakishindwa kuwachukulia hatua watu kama hao, kutokana na ama kutokuwepo vituo vya polisi ama rushwa ya pesa na kitoweo kutoka kwa wavuvi” anasema Mtendaji Kata huyo, Tumaini Mugeta.
Kwa kuhitimisha uchunguzi wake, mwandishi wa makala hii alifika pia ofisini kwa Afisa Elimu Shule za Msingi, Musoma Vijijini, Boniphace Magesa ambaye hakukiri moja kwa moja wala kukanusha kuwepo kwa tatizo hilo, ingawa alikiri kuwepo kwa utoro, ufahuru duni na kudorora kwa kiwango cha elimu katika maeneo hayo.
Magesa anadai kuwa hilo tatizo lilikuwepo kwa kiasi kikubwa hapo siku za nyuma, lakini baada ya kufuatilia na kuhimiza uwajibikaji kwa walimu wanaofundisha kwenye maeneo hayo, ikiwa ni pamoja na kutishia kuwachukulia hatua wazazi wa wanafunzi wanaotorokea kwenye kambi za wavuvi, walau tatizo hilo lina unafuu kidogo.
“Nipe nafasi nikutafutie data kamili kuhusiana na changamoto hiyo, kwa sasa sina taarifa sahihi kuhusiana na swali lako, lakini hayo uliyoyasema yanaweza kuwa na ukweli…, siku za nyuma hali ilikuwa mbaya lakini tumekemea kemea kufuatia kukithiri kwa utoro na kushuka kwa kiwango cha ufahuru,…, walau sasa hali siyo mbaya sana,… anyway nipe nafasi nitakutafutia data kamili…” anasema Magesa.
Pamoja na Sera ya Elimu ya Mwaka 1995 sambamba na sheria ndogo ndogo (by- lows) kuwabana wazazi dhidi ya kutowapeleka watoto shule na kufuatilia maendeleo yao kielimu, bado sheria hizo zimekuwa zikipuuzwa na baadhi ya watendaji wa Serikali na wazazi, licha ya kusimamiwa kwa karibu na Kamati za Shule zinazowajumuisha pia wazazi hao hao!.