YANGA imetwaa ubingwa wa soka wa Tanzania Bara kwa mara ya tatu mfululizo na kuibeba ‘ndoo’ moja kwa moja katika msimu ambao umekuwa na changamoto nyingi zaidi.
Mabingwa hao wa kihistoria, ambao wamewanyima watani wao wa jadi, Simba, fursa ya ubingwa walioukosa kwa misimu mitano sasa, wameweza kuwa timu pekee yenye safu kali zaidi pamoja na ngome imara kuliko timu zote zilizoshiriki ligi hiyo msimu wa 2016/2017.
Licha ya sherehe zao za ubingwa kuingia mkosi baada ya kufungwa bao 1-0 na Mbao FC jijini Mwanza Jumamosi, Mei 20, 2017, lakini Yanga imeunyakua ubingwa huo kwa tofauti ya idadi ya mabao ya kufunga na kufungwa dhidi ya mahasimu wao, Simba, ambao katika mechi yao ya mwisho walishinda 2-1dhidi ya Mwadui kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.
Simba na Yang azote zimefikisha pointi 68, lakini uwiano wa mabao ndio uliowanyima ubingwa vijana hao wa Msimbazi ambao waliongoza ligi kwa muda mrefu hasa duru la pili na kulikuwa na matumaini makubwa ya kunyakua ubingwa.
FikraPevu inatambua kwamba, Yanga ilikuwa katika kipindi kigumu kwa muda mrefu tangu kuanza kwa msimu, hasa baada ya kumwondoa kocha Mholanzi Hans van Pluijim na kumleta Mzambia George Lwandamina, lakini mambo yaliyumba zaidi baada ya mdhamini wa timu hiyo aliyepewa mkataba wa miaka 10, Yussuf Manji, kukumbwa na matatizo yaliyosababisha hata akaunti zake kufungwa na serikali.
Ubingwa wa mabao
Yanga imepata ubingwa kwa uwiano wa mabao baada ya kufunga mabao 57 na kufungwa 14, wakati Simba imefunga mabao 50 na kufungwa 17.
Hii siyo mara ya kwanza kwa Yanga kunyakua ubingwa kwa staili hiyo, kwani kumbukumbu ambazo FikraPevu inazo zinaonyesha kwamba, katika kipindi cha miaka 52 ya uhai wa kusaka ubingwa wa soka Tanzania, vijana hao wa Jangwani wamewahi kutwaa ubingwa mara nne huko nyuma kwa staili hiyo hiyo.
Wachezaji wa Simba wakishangilia moja ya mabao yao katika ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Maji Maji msimu wa 2016/2017.
Katika Ligi Kuu ya Muungano mwaka 1983 iliyozishirikisha timu nne – mbili kutoka Tanzania Bara na mbili Zanzibar – ubingwa ulionekana kuwa ama wa Simba au KMKM wakati timu zote zimebakiza mechi moja moja.
Kumbukumbu za FikraPevu zinaonyesha kwamba, kabla ya Oktoba Mosi, 1983 ambayo ilikuwa siku ya mwisho ya kukunja jamvi la ligi hiyo, Simba ilikuwa inashika nafasi ya pili nyuma ya KMKM, lakini zote zikiwa na pointi 6, ingawa KMKM walikuwa na mabao sita ya kufunga na kufungwa matatu, huku Simba ikiwa na mabao matano ya kufunga na matano ya kufungwa.
Yanga wenyewe walishika nafasi ya tatu wakiwa na pointi tano, wakiwa wamefunga mabao manne na kufungwa matatu.
Kwahiyo KMKM na Simba kila moja ilihitaji ushindi na wakati huo huo kuiombea Yanga ifungwe na Small Simba ili kuunyakua ubingwa.
Lakini ushindi wa Yanga wa mabao 4-1 dhidi ya Small Simba ya Zanzibar na kutoka suluhu kwa Simba na KMKM ndio ulioipa Yanga ubingwa wa Muungano mwaka huo kwa tofauti ya uwiano wa mabao.
Yanga ilifikisha pointi 7 sawa na KMKM na Simba, lakini ilikuwa na mabao 8 ya kufunga na manne ya kufungwa, hivyo kuwapiku ‘Wanamaji’ KMKM ambao walikuwa na nafasi kubwa zaidi ya ubingwa.
Kumbukumbu za FikraPevu zinaonyesha kwamba, mabao ya Yanga katika mechi hiyo ya mwisho yalifungwa na Charles Boniface Mkwasa katika dakika za 9, 41 na 76 na Abeid Mziba akafunga dakika ya 37, wakati lile la Small Simba lilifungwa na Suleiman Omari dakika ya 25.
Yanga siku hiyo iliwachezesha Joseph Fungo, Isihaka Hassan 'Chukwu', Ahmad Amasha, Athumani Juma 'Chama', Allan Shomari, Juma Mkambi, Fred Felix Minziro, Charles Boniface, Makumbi Juma/Moshi Majungu, Abeid Mziba, na Juma Kampala/Hussein Idd.
Small Simba yenyewe ilikuwa na Ali Muhsini, Leonard William, Salum Suleiman, Mohammed Khalfani, Yussuf Mussa, Fadhil Ramadhan, Abdulwakati Juma, Rashid Khamis, Suleiman Omari na Seif Bakari/Hussein Ally.
Kwa mujibuwa kumbukumbu za FikraPevu, mwaka 1987 Yanga pia ilitwaa ubingwa kwa tofauti ya mabao dhidi ya Pamba FC ya Mwanza Katika Ligi ya Tanzania Bara baada ya timu hizo kufikisha pointi 23.
Hata hivyo, Yanga ilikuwa na mabao 20 ya kufunga na 10 ya kufungwa, wakati Pamba ilikuwa imefunga mabao 18 na kufungwa 9.
Mechi ya mwisho Septemba 1, 1987 ilishuhudia Yanga ikiifunga Maji Maji bao 1-0 Songea kupitia kwa Mziba. Siku hiyo Yanga iliwachezesha Fungo, Yussuf Ismail Bana, Minziro, Allan Shomari, Lawrence Mwalusako, Issa Athumani, Abubakar Salum, Athumani China, Mziba, Edgar Fongo/Moshi Majungu na Lucius Mwanga/Said Mrisho ‘Zicco wa Kilosa’.
Kikosi cha Yanga cha mwaka 1987.
Maji Maji, ambayo ilishika nafasi ya tatu msimu huo kwa kufikisha pointi 20, iliwachezesha Steven Nemes, Hussein Kaitaba, Samli Ayoub, Peter Mhina, Mhando Mdeve, Abdallah Chuma, Ahmed Abbas, Kevin Haule, Peter Tino, Madaraka Selemani na Venance ‘Motto’ Mwamoto/Rajab Mhoza. Mechi hiyo ilichezeshwa na Kassim Chona wa Mwanza aliyesaidiwa na Shaaban Nyamwera wa Morogoro na Twaha Kaujanja kutoka Mbeya.
Siku hiyo Pamba nayo ilichapa Nyota Nyekundu bao 1-0 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, bao ambalo lilifungwa na Hamza Mponda katika dakika ya 81.
FikraPevu inakumbuka kwamba, mwaka huo Simba ilinusurika kushuka daraja, na ishukuru ‘sare ya ajabu’ ya mabao 5-5 dhidi ya Tukuyu Stars kwenye Uwanja wa Taifa ambayo iliifanya ichupe hadi nafasi ya tatu kutoka mkiani na kuzipisha Reli ya Morogoro na Nyota Nyekundu ambazo ziliteremka.
Kabla ya mechi hiyo ya mwisho, Simba ilikuwa na pointi 16 na mabao 14 ya kufunga huku ikiwa imefungwa mabao 15, lakini sare ikaifanya ichupe juu ikilingana pointi na Biashara (RTC) Mwanza, Coastal Union na Nyota Nyekundu ambayo hata hivyo ilikuwa na mabao 15 ya kufunga na 16 ya kufungwa.
Karibu mechi tatu za mwisho msimu huo zilikuwa na walakini, au kwa lugha nzuri, ‘zilipangwa’ matokeo yake.
Simba ilitoka sare 5-5 na Tukuyu Stars ambayo haikuwa katika hatari ya kushuka daraja huku mabao ya Wana Msimbazi yakifungwa na Edward Chumila (mawili), Francis Mwikalo, Daniel Menembe na Malota Soma ‘Ball Jugler’, wakati ya Tukuyu yalifungwa na Michael Kidilu na Lumumba Richard ‘Burruchaga’ aliyefunga manne.
RTC Kigoma ambayo haikuathirika na matokeo, ilifungwa mabao 5-1 na ‘ndugu zao’ Biashara Mwanza ili kuwaepusha wasishuke daraja. Bao la RTC Kigoma lilifungwa na Wastara Baribari dakika ya 35 wakati yale ya Biashara Mwanza yalifungwa na Philemon ‘Fumo’ Felician aliyefunga manne dakika za 9, 10, 64, na 73, na Dioniz John dakika ya 48.
Reli ndio waliochezea kibano hasa kutoka kwa Coastal Union baada ya kufungwa mabao 5-2, lakini nao hata kama wangeshinda mechi hiyo isingewasaidia kwani tayari walikuwa wameshuka daraja, hali ambayo inadhihirisha wazi kwamba mechi ‘ilipangwa’ kuinusuru Coastal Union isiteremke.
Kumbukumbu za FikraPevu zinaonyesha kwamba, hata bao la kujifunga la beki Salum Pembe katika dakika ya 18 lilikuwa la kizembe kwa sababu alifumua shuti la nguvu wakati akiuridisha mpira huo kwa kipa wake.
Mabao ya Reli siku hiyo yalifungwa naLivingstone Sanke dakika ya 23 na Madundo Mtambo dakika ya 62 (sasa ni Profesa na Mkurugenzi Mkuu wa
Tanzania Industrial Research Developments Organization (TIRDO), wakati yale ya Coastal yalifungwa na Idrissa Ngulungu dakika ya 5, Yassin Abuu Napili dakika ya 14, Salum Pembe (alijifunga dakika ya 18), na Hussein Mwakuruzo akafunga mawili dakika za 35 na 82.
Katika mwaka 1993, Yanga iliinyima Simba ubingwa wa Tanzania Bara kwa uwiano wa mabao pia, ambapo licha ya timu zote kufikisha pointi 43, lakini Yanga ilikuwa na mabao 46 ya kufunga na 15 ya kufungwa, wakati Simba ilifunga mabao 40 na kufungwa 13.
Kikosi cha Yanga cha mwaka 1993.
Hata hivyo, Yanga iliupata ubingwa huo kwa mbinde baada ya kuifunga Milambo mjini Tabora mabao 3-2 katika mechi ya mwisho, wakati Simba wenyewe waliichapa Pan African 2-0 jijini Dar es Salaam kupitia kwa Dua Said na Abdul Mashine.
Vile vile, katika msimu wa 2010/2011, Yanga ilitwaa ubingwa kwa uwiano wa mabao dhidi ya Simba japokuwa zote zilifikisha pointi 49.
Yanga ilifunga mabao 32 na kufungwa 7, wakati Simba ilifunga mabao 40 na kufungwa 17, hivyo ikaukosa ubingwa licha ya kushinda mechi yake ya mwisho dhidi ya Maji Maji kwa mabao 4-1. Yanga yenyewe iliifunga Toto African 3-0.
Timu nyingine pia
FikraPevu inafahamu kwamba, Yanga siyo timu pekee kutwaa ubingwa kwa uwiano wa mabao nchini Tanzania.
Kumbukumbu zinaonyesha kwamba, Coastal Union iliunyakua ubingwa wa Tanzania Bara mwaka 1988 kwa tofauti ya mabao ingawa ilifungana pointi na Yanga na African Sports. Zote zilikuwa na pointi 26.
Licha ya Abdallah Burhani na Kenneth Mkapa kuifungia Yanga mabao mawili katika dakika ya 3 na 74 na kuipa ushindi wa 2-0 dhidi ya Nyota Nyekundu Julai 16, 1988 bado ‘Wagosi wa Kaya’ waliweza kutwaa ubingwa.
Coastal ilifunga jumla ya mabao 27 na kufungwa 17 wakati Yanga ilifunga 24 na kufungwa 16 huku African Sports ikifunga 23 na kufungwa 13.
FikraPevu inakumbuka kwamba, msimu huo pia Simba ilinusurika kushuka daraja kwa mara ya pili mfululizo na katika mechi yake ya mwisho ilichapwa bao 1-0 na Pamba kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.