Serikali yawasilisha rasimu ya kanuni kusimamia mitandao ya kijamii na utangazaji

Jamii Africa

Katika kile kinachotajwa kubana uhuru wa kujieleza na haki ya kupata habari, serikali imeendelea na mchakato wa kuandaa kanuni zitakazosimamia maudhui ya mitandao ya kijamii na utangazaji ili kulinda maslai ya taifa.

Hatua hiyo ya serikali inakuja mwezi mmoja tangu Kamati ya Maudhui ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kukutana na wadau wa habari nchini ili kujadili utaratibu mzuri wa kusimamia  maudhui ya mitandao ya kijamii (online Content) ili kuepuka kuwalinda watumiaji wa mtandao dhidi ya habari zisizofaa.

Akizungumza leo jijini Dar es salaam, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Prof. Elisante Ole Gabriel amesema serikali inakuja na kanuni mpya kwasababu mitandao ya kijamii inatoa habari zisizo na uhakika ambazo hulenga kuishambulia serikali na watendaji wake.

“ Mitandao imekuwa ikitoa habari kwa harakati lakini inatumiwa vibaya  kuanika siri za watu na kushambulia serikali. Tunaweka kanuni hizi ili mtumie mitandao hiyo kwa mujibu wa maslahi ya kuhabarisha huku mkiwa salama”, amesema.

Amesema kuwa kanuni hizo zitasimamia kwa karibu habari za mitandaoni ili kuhakikisha wananchi wanapata habari za uhakika na kuwaepusha na mambo ya nje ya nchi yanayopingana na maadili ya Taifa.

"Ni lazima tuwe na kanuni ambazo zitaangalia maudhui ya ndani na kuepuka mambo ya kigeni.  Habari ina nguvu, pasipokuwa na kanuni nzuri, mifumo na msingi madhubuti inaweza kuwa hatari ", anaeleza na kuongeza kuwa,

“Nataka kanuni hizi zihakikishe vyombo vya habari vinawapa haki ya kupata habari wenye mahitaji maalumu. Uhuru wa mitandao lazima uwe na mipaka yake ili usibugudhi au kuwadhuru watu wengine”.

Rasimu ya kanuni za Maudhui Mtandaoni zitawahusu wamiliki wa Blogs, Majukwaa (Forums), waendeshaji wa mitandao ya kijamii kama Facebook, Instagram, Twitter na WhatsApp, runinga za mtandaoni (Online TV) na vibanda vinavyotoa huduma ya internet na watumiaji wa mtandao. Lakini pia zitagusa wamiliki wa radio na runinga (television).

Kwa muktadha huo, wamiliki wa Blogs itawalazimu wasajiliwe na kuchuja baadhi ya taarifa, pia wawe tayari kuwataja wanaowapa taarifa wakati wowote atakapotakiwa na mamlaka husika.

Kwa wamiliki wa internet cafe watatakiwa kuweka tangazo linalokataza kuangalia picha na video za ngono na kuweka kamera maalumu (CCTV) kwenye cafe zao.  Kwa watumiaji watatakiwa kuhakiki taarifa wanazoweka mtandaoni .

TCRA wamepewa nguvu ya kisheria kusimamia kanuni hizo kwa kuhakikisha maudhui kwenye vyombo vya habari yanapita katika mchakato unaotakiwa kabla ya kumfikia mwananchi wa kawaida.

Rasimu ya pili ya kanuni za utangazaji inasema kwamba kuanzia saa 11:00 asubuhi mpaka 03:00 usiku muziki wa ndani ndio unaotakiwa kupigwa kwa aslimia 80% ama zaidi ila kuhusu habari na mengineyo zitarushwa kadiri ya vipindi vyao ambavyo wamejipangia wao.

Kanuni hizi siyo kanuni za sheria ya Makosa ya Mtandao. Ni kanuni mpya ambazo serikali imeziandaa kwa lengo la kusimamia maudhui ya mitandao ya kijamii na matangazo ya radio na TV, huku ikisema kanunu hizo zinalenga kulinda maslai ya taifa na kuhakikisha wananchi wanakuwa salama na kupata taarifa sahihi kutoka vyanzo sahihi.

 

Maoni ya Wadau

Wadau wa habari nchini wanasema kanuni hizo ni muendelezo wa serikali kuminya uhuru wa  kujieleza na haki ya kupata habari kwa wananchi. Ni vigumu kuwazuia wananchi wasipate taarifa kutoka maeneo mbalimbali duniani kwa kuanzisha sheria ambazo  zina lengo la kuwalinda baadhi ya watu walio katika madaraka.

Hivi karibuni akitoa maoni yake katika Kamati ya Maudhui ya TCRA, Mkurugenzi wa Jamii Forums, Maxence Melo aliitaka serikali kushirikiana kwa karibu na watumiaji wa mitandao ili kujua mahitaji yao kabla ya kutunga sheria na miongozo ambayo inawanyima wananchi uhuru wa kujieleza.

“TCRA ishirikiane na watumiaji wa Mitandao ya Kijamii; iende jamii ilipo ili kuelewa mahitaji ya jamii. Si jambo la busara kwa mamlaka kuanza kutunga sheria na kuzitumia kwa watu wasioelewa hata nini maana ya kosa”. Amesema Melo.

 Akifafanua suala la maadili ameiomba serikali kuweka bayana tafsiri sahihi ya ‘Maadili ya Mtanzania’ili kuondoa mkanganyiko uliopo katika jamii, ambapo watumiaji wa mitandao ya kijamii wamekuwa wakilalamikiwa kuharibu maadili ya taifa.

“Mnapoongelea "Maadili ya Mtanzania" ni yapi na nani aliyaweka? Nadhani ni wakati muafaka sasa wa kuwa na hicho kinachoitwa "Maadili ya Mtanzania" ili kieleweke. Watumiaji wa mtandao wa Tanzania hawawezi kuutumia mtandao sawa na mataifa mengine hivyo mnapotunga sheria basi muwe sehemu ya jamii mnayoitungia sheria”. Amesema Melo.


 
 

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *