Katavi: Madawati bado yatesa wanafunzi, wanakaa sakafuni

Jamii Africa

MIONGONI mwa mafanikio ya harakaharaka ya uongozi wa Rais John Magufuli tangu aingie madarakani, Novemba 5, mwaka jana, ni wingi wa madawati katika shule nchini.

Idadi kubwa ya shule, hasa za msingi, zimekuwa na “mafuriko” ya madawati, kiasi cha kukosekana mahali pa kuyahifadhi, kwani yanazidi mahitaji ya shule.  Mwongozo wa Wizara ya Elimu unahimiza dawati moja kukaliwa na wanafunzi watatu hadi wanne.

Pamoja na mafanikio hayo, bado upo “ukame” wa madawati katika Shule ya    Msingi Mkuyumani, Kata ya Majimoto, Wilaya  ya  Mlele,  Mkoa  wa  Katavi.

Shule hiyo yenye wanafunzi 2500, ni wanafunzi wanaozidi kidogo, 1750, ndiyo wanaokalia madawati wakiwa darasani, huku wengine wakikaa juu ya sakafu au kukalia ‘madumu.’

Idadi hiyo ni sawa na asilimia 70 ya wanafunzi wanaosoma vyema, huku wenzao, asilimia 30 “wakiteseka” kuipata elimu. Pamoja na kuwepo changamoto huyo ya madawati, shule hiyo pia ina upungufu wa walimu; kwani ina walimu watatu tu kwa shule nzima.

Mwalimu  Mkuu  wa  shule  hiyo,  Mbamba Makoye ameieleza FikraPevu kuwa shule yake iliyoko  katika Halmashauri ya Mpimbwe  ina walimu watatu wa  kuajiliwa.

“Tunashukuru pia kwamba pamoja na kuwa na idadi ndogo ya walimu wanaofundisha masomo yote na madarasa yote, pia tunao vijana wanne wa kujitolea, hawa wanatusadia sana,” anaeleza.

Mwalimu huyo anasema ongezeko la wanafunzi walioandikishwa darasa la kwana mwaka huu, linesababisha kukosekana kwa madawati ya kutosha.

Serikali ya awamu ya tano, chini ya Rais John Magufuli ilitangaza kuwepo kwa elimu bure kuanzia darasa la awamu hadi elimu ya sekondari, uamuzi ambao umeongeza wanafunzi katika shule za msingi na sekondari.

Pamoja na mwalimu Makoye kueleza hali hiyo kuwa ameizoea, walimu watatu anaowaongoza wameilalamikia, huku wakisisitiza kuwepo kwa mazingira bora ili wapate mwanya wa kufundisha vyema.

Mwalimu wa   taaluma  wa   shule  hiyo,   Dickson  Fabiani  ameiambia FikraPevu kwamba mazingira yao ya kufundisha ni magumu na kamwe hayawezi kuwapa wanafunzi elimu bora. “Ninalazimika kufundisha madarasa  matano na masomo yote, wakati sio  utaratibu wa taaluma yetu katika kuwapa wanafunzi elimu nzuri,” anaongeza mwalimu huyo.

FikraPevu imebaini kuwepo kwa wanafunzi wanaofikia 250 kwa darasa moja na ambao hufundishwa kwa wakati mmoja, wengine wakiwa wamekaa chini.

Pia imebainika, mbali na uhaba wa madawati na walimu, shule hiyo inakabiliwa na upungufu wa matundu ya vyoo, hivyo kufanya mazingira ya kusoma na kusomesha kuwa magumu.

“Inasikitisha kuwa walimu wa shule hii wanatumia vyoo kwa pamoja, walimu hawana choo, hii siyo nzuri kwa utoaji wa elimu bora,” analalamika mwalimu Fabiani.

Mwenyekiti  wa halmashauri  hiyo,   Nyasongwa    Serengeti    ameiambia FikraPevu kuwa   Halmashauri  ya   Mpimbwe  imeanza  kufanya   jitihada za  kuondoa   tatizo la  wanafunzi  kukaa  chini  kwani  wameanza    kutengeneza  madawati  200   .

Mwandishi wa   habari    hizi  aliyetembelea  shule  hiyo ya amebaini  kuwa hata kama Halmashauri  hiyo  itatengeneza  madawati  hayo, bado  hayatatosha.

Mmoja  wa  wazazi wa  wanafunzi, Michael  Kalubwa  alisema kuwa  ni  jambo la  kushangaza kwamba shule hiyo na nyingine za mkoa wake, bado zinakabiliwa na ukosefu wa madawati wakatizipo shule zilizozidisha madawati wakati wa zoezi la kuyatengeneza.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *