Kemikali za  sumu bado tishio kwa uhai wa binadamu

Jamii Africa

Imeelezwa kuwa matukio ya watu kunywa sumu yameongezeka nchini na kuchangia vifo vya watu wanaokufa muda mfupi kabla ya kupatiwa huduma ya kwanza.

Sumu ni kitu chochote kinachoweza kuua au kudhuru kupitia  kemikali zinazoingia mwilini. Neno ‘Sumu’ limetokana na neno la Kilatini potare ambalo lina maana ya kunywa. Lakini sumu inaweza kuingia mwilini kwa njia mbalimbali ikiwemo: hewa, ngozi, kuchomwa sindano, mionzi, kung’atwa na nyoka au wadudu.

Kwa maana nyingine sumu ni  kemikali za hatari ambazo binadamu hatakiwi kunywa au kugusa, lakini zipo baadhi ya kemikali ambazo zinapatikana kwenye chakula na dawa ambapo zinaweza kuleta madhara.

Kulingana na takwimu za Kituo huru cha takwimu za serikali (2017) zinaeleza  kuwa sumu imekuwa miongoni mwa visababishi vya vifo kwa wagonjwa wanaolazwa katika hospitali mbalimbali nchini ambapo unywaji au kumeza sumu ndio njia inayotumiwa sana na watu wanaotekeleza vitendo hivyo vya kujidhuru. 

Kwa mujibu wa takwimu hizo zinaonyesha unywaji wa sumu ulisababisha vifo vya watu 207 kwa mwaka 2013 pekee. Sababu kubwa ya vifo hivyo ni kwamba kemikali zinazopatikana kwenye sumu huathiri seli za mwili ndani ya muda mfupi baada ya sumu hiyo kuingia mwilini na kama msaada wa haraka haujatolewa uwezekano wa mtu kufa ni mkubwa.

Vifo vinavyosababishwa na sumu hutofautiana kutoka mkoa mmoja hadi mwingine. Mwaka 2013, Mikoa ya Mbeya, Arusha, Mara, Tabora, Kigoma, Kagera, Simiyu ndio ilikuwa na vifo vingi vya watu kunywa sumu. Katika mwaka huo Arusha na Mbeya zilishika nafasi ya juu ya kuwa na watu wengi ambao walifariki kwa matukio ya kunywa sumu.

 

MIKOA YENYE VIFO VINGI VYA WATU WALIOKUNYWA SUMU (2013) Chanzo: OpenData Tanzania

Lakini mikoa ya Tanga, Pwani, Dar es Salaam haikuripotiwa kuwa na watu waliofariki kwa kunywa sumu ambapo inaweza kutafsiriwa kuwa mikoa hiyo  imeboresha huduma za dharura kwa watu wanaopatikana na kesi za kunywa sumu.

Vifo vichache vimeshuhudiwa kwenye mikoa ya Manyara kifo (1), Rukwa (3), Katavi (3) , Iringa (3) na Shinyanga (3). Idadi ya vifo 207 iliyotajwa inaweza ikawa ni ndogo ikilinganishwa na matukio yanayotokea kila siku ya watu kunywa sumu na kufariki.

 

Dalili za mtu aliyedhurika na sumu

Baadhi ya dalili hizo ni kuungua au mdomo kuwa mwekundu, kupumua kwa taabu, kuchoka na kulegea, kutapika, kuchanganyikiwa na kupoteza fahamu. Endapo itatokea mtu amekunywa sumu au amekula chakula chenye sumu apelekwe kwenye kituo cha  afya  ili kupata matibabu ya haraka.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *