Wakili wa upande wa utetezi avutana na Wakili wa Jamhuri ambayealiiomba mahakama ipokee kielelezo cha taarifa iliyowekwa kwenye mtandao wa JamiiForums ikisadikiwa kuichafua kampuni ya mafuta ya Oilcom.
Kesi 456 ni ile inayoikabili JamiiForums na kampuni ya Oilcom inadaiwa kukwepa kodi na uchakachuaji wa mafuta katika bandari ya Dar es Saalam imeendelea tena leo kwa kusikilizwa kwa mashahidi wawili wa upande wa Jamhuri.
Kesi hiyo ilibadilishiwa hati ya mashtaka (ingawa shahidi wa kwanza alishasikilizwa na ushahidi kuletwa mbele za mahakama). Kilichobadilika katika hati hiyo ni kifungu cha sheria (Kifungu cha 22(1) badala ya 22(2) cha Sheria ya Makosa ya Mtandao), ilianza leo kwa shahidi wa kwanza kutoa ushahidi wake kabla shahidi wa pili Usama Mohammed kujieleza mbele ya mahakama na kuibua mvutano wa mawakili.
Mvutano huo wa maneno ulijitokeza baada ya Wakili wa Jamhuri Kisheji kuomba Mahakama ipokee kielelezo cha maudhui ya taarifa iliyowekwa kwenye mtandao wa JamiiForums mnamo 13 Februari 2016 ambazo zililenga kuichafua kampuni ya Oilcom. Kielelezo hicho kilitolewa na shahidi wa pili wa kesi hiyo aliyejitambulisha kwa jina Usama Mohammed, Meneja Forodha wa kampuni ya Oilcom.
Usama amesema baada ya kuthibitisha kuwa taarifa hiyo iko kwenye mtandao alichapisha kwenye karatasi na kuwasilisha kielelezo hicho Polisi kwa ajili ya uchunguzi dhidi ya madai yaliyotolewa na mtumiaji wa mtandao huo aliyejulikana kwa jina la Furheer kuandika ujumbe wenye kichwa, “USHUHUDA: Hivi ndivyo mafuta yanavyoibiwa Bandarini Dar…”.
Licha ya Wakili Kisheji kutaka ombi lake likubaliwe, Wakili wa upande wa utetezi Peter Kibatala alipinga maombi hayo kwa madai kuwa hayakidhi matakwa ya Sheria ya Kielekroniki ambayo imefafanua hatua za kufuata ili kutoa ushahidi kama huo.
Wakili Kibatala amesema kulingana na uamuzi wa Jaji Mwakilamba juu ya mchakato wa kielekrotoniki wa kuwasilisha ushahidi kama huo, umemuomba Hakimu Simba asipokee kielelezo hicho ambacho maudhui yake yamewekwa kwenye karatasi ambapo taarifa hiyo ilikuwa ya mtandaoni.
Wakili Kibatala amesema ushahidi wanaotaka kuutoa unaangukia katika ‘electronic evidence’ na kuna masharti ya kisheria mahakama kupokea electronic evidence. Vigezo hivyo vitano ambavyo vyote lazima viendane kwa pamoja viliwekwa na shauri la Kesi ya Biashara (Commercial case) namba 10 ya mwaka 2008 kati ya Lazurius Mirisho Mafie dhidi ya Gasper Kilenga Alias na Moiso Gasper uamuzi wa Jaji Makaramba.
Anaongeza kusema kuwa vigezo hivyo ni mfanano (Upande unaoleta ushahidi lazima ulete misingi ili uonekane wa kweli) na sheria ambayo inataka maandishi kama yalivyo kwenye kifaa husika.
Anabainisha kuwa “ Shahidi hajajengewa misingi ya kukidhi hivyo vigezo na vinatakiwa kuzibwa na Shahidi. Pia haipo katika uhalisia (original form), hiyo ni kopi na kwa misingi hiyo miwili tunapinga ushahidi kupokelewa”.
Kauli hiyo ya Kibatala iliibua mabishano baina ya mawakili hao wawili ambapo Wakili Kishenyi alimwambia Hakimu kuwa mapingamizi yaliyotolewa na Kibatala hayana uzito kisheria huku akifungua vifungo vya sheria kujibu hoja za wakili wa utetezi.
Wakili Kishenyi anasema “mapingamizi ya wakili msomi Kibatala hayana uzito kwenye ombi la kupokea kielelezo. Upokeaji wa electronic printout inaongozwa na Sheria namba 18 ya Electronic Act” (Anavitaja vifungu na kujibu mapingamizi yaliyotolewa na wakili Kibatala).
Kwa mara nyinge, Wakili Kibatala anasema vifungu vya Sheria ya Kielekroniki viko sawa utofauti unaojitokeza ni lugha iliyotumika kwani kifungu cha 18 kimefanana na hukumu ya Jaji Makaramba na ufafanuzi umetolewa kwenye kifungu cha 19 cha sheria hiyo.
Baada ya mfutano huo wa mawakili wa pande mbili, Hakimu hajatoa uamuzi wa kupokea kielelezo hicho na amesema atatoa uamuzi huo Desemba 20 mwaka huu.
Shahidi wa kwanza azungumza
Hata hivyo, kesi hiyo ilianza kwa shahidi wa kwanza, ASP Fatuma Kigondo, Afisa Kikosi cha Reli (RCO) kuapa na Hakimu kumruhusu Wakili wa Jamhuri kumuuliza maswali.
Shahidi huyo amesema mnamo 23 Februari, 2016 alikuwa anafuatilia kesi ambayo jalada la uchunguzi lilikuwa linahusu taarifa za mtandao za kuchafuliwa kwa kampuni ya Oilcom baada ya mtumiaji wa JamiiForums aliyejulikana kwa jina la Furheer kuandika ujumbe wenye kichwa, “USHUHUDA: Hivi ndivyo mafuta yanavyoibiwa Bandarini Dar…”.
Anasema aliandika barua kwa Wakurugenzi wa JamiiForums ili apatiwe taarifa muhimu za mtumiaji huyo ili zitumike kwenye uchunguzi wa tuhuma lakini hakujibiwa barua hiyo. Shahidi anaisoma barua hiyo mbele ya Hakimu Simba na Wakili wa Jamhuri anaomba Barua ipokelewe Kama kielelezo baada ya upande wa mashtaka kutokuwa na pingamizi.
Kwa upande wake, wakili wa Utetezi Peter Kibatala alimtaka shahidi aimbie mahakama kama barua hiyo iliyoandikwa kwenda JamiiForums ilikuwa ni ombia au amri? Shahidi amesema barua hiyo ilikuwa amri. Lakini Kibatala alipomuhoji kwa kiasi gani barua hiyo ilikidhi matakwa ya kisheria, shahidia alibadilisha kauli yake na kusema barua hiyo ilikuwa ni ombi. Haya yalikuwa sehemu ya mahojiano yake na wakili Kibatala:
Kibatala: Kosa mnalotaka kuchunguza, Ni kosa lipi?
ASP Fatuma: Kosa linabainishwa baada ya kufungua jalada la uchunguzi.
Kibatala: Kosa Ni nini?- Kwa hio mpaka mnafungua jalada mlikuwa hamjuhi kosa?
ASP Fatuma: Tulikuwa tunachunguza Preliminary investigation.
Kibatala: Kosa gani?
ASP Fatuma: Kosa ndio Hilo jalada la uchunguzi. Kosa linakuja baada ya kuchunguza.
Kibatala: Taarifa zilizoandikwa na JF expert member Ni za kweli au sio kweli?
ASP Fatuma: Mimi nilifungua jalada la hii Kesi na Wala sio mpelelezi.
Kibatala: Bado mpaka leo taarifa zinachunguzwa?
ASP Fatuma: Nilihama May mwaka jana.
Kibatala: Mpaka unahama?
ASP Fatuma: Niliacha under investigation
Kibatala: Unaifahamu nchi inaitwa Brunei mji wake mkuu ni Dar es Salaam.
ASP Fatuma: Sifahamu
Kibatala: Barua yako imesema Dar es Salaam iko nchi gani?
ASP Fatuma: Jeshi la Polisi la Tanzania
Kibatala: Sio kwenye barua, Kwenye post aliandika Dar es Salaam inayoibiwa mafuta Ni ya nchi gani?
ASP Fatuma: Alisema Tanzania.
Kibatala: Wapi? Msomee hakimu hiyo Dar es Salaam ni ya nchi gani.
ASP Fatuma: Oilcom iko Tanzania
Kibatala: Ni wapi kwenye post wameandika Ni Dar es Salaam ya Tanzania?
ASP Fatuma: Haipo.
Kibatala: Hii kampuni ya Oilicom unafahamu imesajiliwaje?
ASP Fatuma: Sifahamu
Kibatala: Ulifatilia bandarini ukweli wa tuhuma?
ASP Fatuma: Sikwenda(kwa sababu Mimi sio mpelelezi)
Kibatala: Content zake za hio post unazifahamu?
ASP Fatuma: Kwa wakati huo niliziona, Sifahamu.
Kibatala: Leo huwezi kuzitolea ushahidi mahakamani?
Kibatala: Mlipopeleka hio barua mliprint content?
ASP Fatuma: Sikumbuki, hatukuweka
Kibatala: Mpaka unaondoka, ulikuwa unajua JamiiForums wana taarifa ulizoomba?
ASP Fatuma: Ndio
Kibatala: Nini kilikufahamisha?
ASP Fatuma: Kwa uelewa wangu Mdogo, nilijua wanafahamu, mtu anaweza kuacha namba za simu.
Kibatala: Unafahamu steps mpaka mtu anajisajili JamiiForums?
ASP Fatuma: Sifahamu.
Kibatala: Mlichukua Hatua gani nyingine kumfikia Furheer
ASP Fatuma: Mimi nilihama na sikuwa mpelelezi?
Kibatala: Mpaka unahama ulichukua Hatua yoyote kumfahamu Furheer JF
ASP Fatuma: Mimi sikuchukua Hatua yoyote(kwa sababu sikuwa mpelelezi)
Kibatala: Hii barua ilielekezwa kwa nani?
ASP Fatuma: Mkurugenzi mkuu.
Kibatala: Nani?(Maana naona washtakiwa wawili)
ASP Fatuma: Sifahamu
Kibatala: Mpaka unatoa ushahidi, ulifanya chochote kujua Max Melo na mwenzake wana uhusiano gani na hicho cheo.
ASP Fatuma: Sikufanya
Kibatala: Kwa ufahamu wako, Je Kuna Kesi yoyote iliyowahi kufunguliwa na Oilcom dhidi ya JamiiForums?(Defamation)
ASP Fatuma: Sijui
Kiabatala: Hapa mahakamani umetoa kithibitisho chochote kwamba haya yaliandikwa JamiiForums?
ASP Fatuma: Binafsi sijatoa
Mwenendo wa kesi
Kesi hiyo ambayo ilianza kusikilizwa Disemba 13, 2016 inawahusu Wakurugenzi wa JamiiForums, Maxence Melo na Micke Williams kukataa kutoa ushirikiano kwa Polisi ili wasaidie kupatikana kwa taaarifa za mtumiaji wa mtandao wa JamiiForums, Furheer katika upepelezi wa jalada la uchunguzi lililofunguliwa na kampuni ya Oilcom ikidai kuchafuliwa kwa kukwepa kodi na kuchakachua mafuta bandari ya Dar es Salaam.
Kwa kutambua uhuru wa kujielezwa JamiiForums hawakutoa taarifa hizo na waliitaka polisi kufuata taratibu za kimahakama. Desemba, 2016 Maxence Melo alikamatwa na kufunguliwa mashataka akiwa kama Mkurugenzi wa Kampuni ya Jamii media inayoendesha mtandao wa JamiiForums alishindwa kutoa taarifa za kiuchunguzi zilizochapishwa kwenye mtandao huo kwa Jeshi la polisi.
Kesi hiyo inaendelea kusikilizwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na hukumu ya mwisho inatarajiwa kutolewa kabla ya mwaka huu kuisha. Kesi hiyo itaendelea tena Desemba 20, mwaka huu.