Kikwete aanza ziara mpya kwa Wizara mbalimbali

Jamii Africa

Rais Kikwete leo ameanza mlolongo mpya wa ziara za kutembelea wizara mbalimbali ili kujionea utendaji wa wizara hizo na kutoa maelekezo mbalimbali. Ziara hizi zinafanana kwa maudhui ziara alizozifanya mwezi mmoja baada ya kuingia madarakani mwaka 2006. Kwa kuanzia ziara hizo Bw. Kikwete ametembelea wizara ya Fedha (Hazina) ambako licha ya kujionea shughuli mbalimbali alizungumza na watendaji na wafanyakazi wa wizara na kutoa maelekezo mbalimbali.

Hata hivyo, ziara hizo inaonekana zimeanza kufanywa kwa kificho huku Idara ya Mawasiliano ya Ikulu ndio ikiwa mtoaji  habari wa matukio yanayoendelea kwenye ziara hizo. Vyombo huru vya habari havijapewa uhuru mkubwa wa kuhudhuria, kuuliza maswali ili kuweza kupata taarifa zaidi na kuweza kuwataarifu Watanzania kuhusu  undani wa ziara hizo za mkuu huyo wa nchi.

Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu iliyotolewa leo Rais Kikwete katika ziara yake huko hiyo Rais alipata nafasi pia ya kutembelea Long Room kitengo cha Mamlaka ya Mapato Tanzania ambapo mapema mwaka huu vyombo mbalimbali vya habari viliripoti juu ya matatizo ya kukatika kwa umeme yalivyosababisha usumbufu mkubwa katika shughuli mbalimbali zinazohusiana na kitengo hicho ambacho kinahusika kwa kiasi kikubwa katika kusimamia uingizaji na usafirishaji mizigo nchini.

Kwa mujibu wa Afisa mmoja wa kitengo hicho Bw. Walid Juma aliyenukuliwa na gazeti moja la Kiingereza nchini mapema Januari mwaka huu TRA inakusanya kiasi cha shilingi bilioni 5 kila siku kupitia kodi na ushuru mbalimbali wa forodha. Hivyo kukatika umeme kunasababisha usumbufu na msongamano mkubwa bandarini na katika vituo vingine vya kuinzia na kuondolea mizigo nchini.

Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu Rais Kikwete aliambiwa kuwa “mapato ya Serikali yameongezeka kutoka makusanyo ya kiasi cha shilingi bilioni 215 kwa mwezi mwaka 2005 wakati Rais kikwete anaingia maradakani hadi kufikia wastani wa shilingi bilioni 420 kwa mwezi kwa sasa.”

Hata hivyo, Rais Kikwete ameendelea kuonesha kuwa serikali yake inapata kazi kubwa ya kusimamia matumizi ya serikali na yeye akiwa ni msimamizi mkuu wa serikali hiyo inaonekana imekuwa vigumu kwake kuwashughulia na kuleta nidhamu katika matumizi ya fedha za umma. Hivyo Rais Kikwete aliitaka Wizara hiyo “kusimamia matumizi ya fedha zinazokusanywa akiwakumbusha viongozi hao kuwa fedha za Serikali siyo shamba la bibi na wala makusanyo hayo ya kodi siyo sawa na ubani wa kilioni.”

Rais Kikwete akionesha kuchoshwa na suala la malalamiko ya wazee wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki kabla ya kuvunjika ameagiza wazee wanaolalamika walipwe “hata kama ni kweli kuwa wengi wa watumishi hao tayari wamelipwa.” Agizo hilo hata hivyo haieleweki lina maana gani katika suala la kufuata utawala wa sheria, kanuni za ajira na maadili ya utendaji kwani linaonekana kubariki malipo ya bila kujali madai halisi.

Wakati huo huo Rais Kikwete alionekana kudokeza kuwa Serikali ya Tanzania imewahi kuwa na hali mbaya sana ya kifedha kiasi cha kushindwa kukopesheka. Kwa mujibu wa taarifa hiyo “Rais Kikwete amesema kuwa ni jambo la heri sana kuwa Tanzania sasa inakopesheka tena, lakini lazima Wizara ya Fedha itumie uangalifu mkubwa katika kukopa ili Tanzania ijikute inarudi tena katika mazingira yaliyopelekea kuachwa kukopeshwa huko nyuma.”

Hata hivyo taarifa ya Ikulu kuhusiana na ziara za Rais imeshindwa kutoa ratiba inayoeleweka ya ziara hizo ili vyombo huru vya habari viweze kufuatilia na kuweza kuwataarifu wananchi badala ya kutegemea taarifa ambazo zimeandikwa kisiasa na kuficha kwa makusudi maswala mengine ambayo yanajadiliwa au kuulizwa katika mikutano hiyo.

Kikwete atembelea Hazina, TRA (Video)

2 Comments
  • wenye kupiga magoti wapige, wanaoinama wainame na wanaoenda chini ya miti wasichelewe yasitukute ya misri, tunisia, libya na bahrein; japo mapolisi walishaanza arusha sijui wanaendelea bado ama ss wametambua na bongo demokrasia imeanza kuota ndevu? tuwaachie jibu wanalo…. watahesabia…. maana kama kule libwa ndege, mabomu.. na maguvu ya kila aina ya kuua watu yametumika bado demokrasia iliendelea kuwika japo hapa bongo wanaita ni fujo… wakati huo itajulikana wenye fujo ni wakijani na doli ama apana….

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *