Kilaini: Andikeni habari za ufisadi na si majigambo ya wanasiasa tu!

Jamii Africa

ASKOFU Msaidizi wa Jimbo Katholiki la Bukoba Methodius Kilaini amevitaka vyombo vya habari kuripoti habari za ufisadi na uzembe ili kuleta unafuu wa maisha kwa wananchi maskini badala ya kuandika majigambo ya viongozi.

Kiongozi huyo wa kiroho ameyasema hayo juzi mjini Bukoba katika ukumbi wa Mtakatifu Francis alipokuwa akifungua mkutano wa mwaka wa Chama Cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Kagera (KPC) uliofanyika sambamba na uchaguzi wa viongozi wapya wa chama hicho.

Katika ufunguzi wa mkutano huo Askofu Kilaini aliwaasa wanahabari wasiogope kutafiti na kufichua mambo ya ufisadi na kuwa vyombo hivyo ni sauti ya wanyonge inayoweza kuifanya Serikali kuwajibika.

“Msiogope kufichua habari za ufisadi na uzembe kama vipo, sio kuandika habari za majigambo ya viongozi badala ya kuandika uozo uliopo. Tangazeni mambo mazuri pia na habari za maeneo ya vijijini” alisema Kilaini.

Pia alisifu kazi nzuri inayoendela kufanywa na vyombo vya habari huku akiwapongeza waaandishi walioonyesha ujasili wa kufuatilia na kuandika habari za utoroshaji wa rasilimali za taifa ukiwemo usafirishaji haramu wa magogo kwenda nje ya nchi.

Aidha Askofu Kilaini alionya kuwa vyombo vya habari vikitumika vibaya vinaweza kuleta maafa makubwa kwa taifa huku akionyesha kukerwa na baadhi ya wanahabari ambao huisaliti fani yao na kupindisha ukweli.

“Mwanahabari mwenye njaa husaliti fani yake na kupindisha ukweli inabidi usome magazeti matatu ili kupata picha kamili ni lazima muandike ukweli na kuanzisha shughuli za kujikimu kwani mafanikio yanatokana na juhudi ya jasho” alisema Kilaini.

Katika ufunguzi wa mkutano huo pia Kilaini aliwaasa waandishi wa mkoa wa Kagera kuandika habari za kuutangaza mkoa na kuvutia shughuli mbalimbali ukiwemo utalii na habari zinazowahusu wananchi wa vijijini badala ya kuandika habari za mjini tu.

Katika uchaguzi wa viongozi wanachama walimchagua John Lwekanika kuwa mwenyekiti wa chama hicho huku Phinias Bashaya akichaguliwa kuwa Katibu na Lilian Lugakingira nafasi ya Mweka Hazina.

Wengine waliochaguliwa ni Gilbert Makwabe mwenyekiti msaidizi huku Mbeki Mbeki akichaguliwa kuwa Katibu Msaidizi na Winfrida Saimon Mweka Hazina Msaidizi ambapo wajumbe wa Kamati ya utendaji ni Mathias Byabato, Perajia Katunzi, Clement Nshelenguzi na Ayuob Mpanja.

3 Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *