Kilimanjaro: Wazazi wagoma kuchangia fedha za chakula kwa ajili ya wanafunzi

Jamii Africa

MPANGO  wa utoaji wa elimu ya msingi bure unaotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Tano umeingia dosari baada ya wazazi kugoma kutoa michango ya fedha kwa ajili ya chakula cha mchana kwa wanafunzi katika shule za msingi zilizopo ndani ya Manispaa ya Moshi.

Hatua hiyo imekuja siku chache baada ya serikali kutoa waraka unaotoa mamlaka kwa wakuu wa mikoa kutoa vibali kwa ajili ya kuziwezesha shule za msingi kuwa na nguvu ya kuchangia fedha kutoka kwa wazazi. 

Waraka huo wa Elimu Namba 3 wa mwaka 2016 umefuta nyaraka zote kuhusu malipo yaliyokuwa yakitozwa katika uendeshaji wa elimu msingi kutoka kwa wazazi na walezi kwenye shule za serikali.

Wanafunzi wa Shule za Msingi za Azimio na Mandela za mjijni Moshi wakitoa burudani za nyimbo na ngoma wakati wa uzinduzi rasmi wa vyoo vya kisasa katika shule hizo vilivyojengwa kwa ufadhili wa Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) hivi karibuni.

Hata hivyo, waraka huo umetoa maagizo na miongozo kwa mamlaka za serikali ikiwamo wakuu wa mikoa kupokea maombi na kutoa vibali kwa wazazi na walezi kuchangia huduma ya chakula cha mchana kwa wanafunzi.

Waraka huo uliosainiwa na Kamishna wa Elimu, Profesa Eustella Balalusesa, pia umewapa nguvu wakuu wa mikoa kuwachukulia hatua za kinidhamu na kisheria wale wote watakaobainika kukiuka taratibu za utoaji wa elimu bure bila malipo.

Kwa upande wao, wakuu wa wilaya nao wamepewa rungu la kuwawajibisha wazazi na walezi ambao watashindwa kuwaandikisha watoto wao shule na kusimamia mahudhurio na maendeleo ya taaluma yao.

HALI YA CHAKULA SHULENI

Ukosefu wa chakula cha mchana kwa baadhi ya shule za msingi katika Manispaa ya Moshi umekuwa ukiwaathiri baadhi ya wanafunzi ambao huishiwa nguvu na kushindwa kuzingatia masomo darasani kwa sababu ya njaa.

Abdulrazuli Kibwiti ni Mwenyekiti wa Kamati ya Shule ya Msingi Azimio iliyopo Kata ya Bomambuzi katika Manispaa ya Moshi, ambaye anasema baadhi ya wanafunzi ambao wazazi wao wameshindwa kulipia fedha kwa ajili ya chakula wamekuwa wakitengwa wakati wa chakula.

Anasema kutengwa kwa watoto hao ni kutokana na mifumo ya utoaji wa chakula shuleni hapo kwa kutumia kadi maalum zinazotolewa kwa watoto ambao wazazi wao wamechangia fedha ya chakula hicho.

Anasema, kamati ya shule ilikaa na wazazi wenye watoto wanaosoma katika shule hiyo na kutoka na maazimio ya kila mzazi kuchangia Shs. 400 ambazo zingesaidia huduma za ulinzi pamoja na chakula cha mchana kwa watoto wao.

Mwenyekiti huyo anasema ni wazazi wachache walioitikia maazimio ya kikao hicho huku wengi wao wakishindwa kuchangia gharama za chakula hali ambayo imesababisha baadhi ya wanafunzi ambao wazazi wao hawajachangia kunyimwa chakula.

Mwalimu Mkuu wa shule hiyo ya Azimio, Doroth Mbuya, anasema kwa sasa mwitikio wa wazazi kuchangia chakula cha mchana kwa watoto wao ni mkubwa na kwamba kati ya wanafunzi 1,101 wa shule hiyo ni wanafunzi  251 tu mpaka sasa ndio hawajalipiwa na wazazi wao.

“Tutatengeneza sheria ndogo za kuwabana baadhi ya wazazi na walezi  watakaoshindwa kulipia huduma za chakula shuleni na huduma nyingine kama za ulinzi, maji na umeme maana haya ni majukumu yao,” alisema.

MADIWANI WANASEMAJE

Diwani wa Kata ya Karanga, Jonathan Makupa, anasema, uongozi wa Kata hiyo yenye Shule ya Msingi ya Magereza umeweka kanuni kwa kila mzazi na mlezi kuchangia Shs. 250 kwa kila mmoja kwa siku sawa na Shs. 45,000 kwa mwaka.

Anasema fedha hizo ni kwa ajili ya chakula cha mchana kwa wanafunzi, gharama kwa ajili ya nishati ya kuni na fedha kwa ajili ya malipo ya wapishi na kuongeza kuwa baadhi ya wazazi wameanza kuwa na mwitikio katika kuchangia.

Hata hivyo, diwani huyo anasema uongozi wa kata kwa kushirikiana na uongozi wa Shule ya Msingi Magereza umeweka kanuni za kuwabana wazazi na walezi ambao watashindwa kuchangia fedha za chakula baada ya mwezi huu kwisha.

Moja ya kanuni hizo ni kuwatoza faini kulingana na thamani ya fedha wanazodaiwa na watakaogoma mali zao zitakamatwa na kuuzwa ili kulipia gharama za chakula kwa mujibu wa maazimio ya vikao vya wazazi. 

MSIMAMO WA SERIKALI NI UPI

Ofisa Elimu wa Manispaa ya Moshi, Patrick Leyana, anasema wajibu wa chakula shuleni ni jukumu la wazazi na kukiri kuwa mwitikio wa wazazi kuchangia chakula cha mchana na maendeleo ya shule haujafikia asilimia 100.

Anasema pamoja na Manispaa ya Moshi kutoa elimu kwa jamii juu ya umhimu wa kuchangia chakula cha mchana shuleni, bado mwitikio ulikuwa si wa kuridhisha na kuongeza kuwa wanakusudia kutumia sheria ya mtoto katika kuwabana wazazi watakaoshindwa kutimiza wajibu wao.

NI YAPI MAJUKUMU YA WAZAZI KATIKA KUCHANGIA CHAKULA SHULENI

Kwa mujibu wa Waraka wa Elimu Namba 3 wa mwaka 2016, moja ya majukumu ya wazazi na walezi ni kushirikiana na uongozi wa shule kuweka utaratibu wa kutoa chakula cha mchana.

Majukumu mengine ni kukemea na kutoa taarifa kwa ngazi husika kuhusu mienendo inayokwenda kinyume na elimu bure bila malipo na kufuatilia mahudhurio na maendeleo ya taaluma ya watoto wao.

WAZAZI WANASEMAJE

Salum Kemanae ni mmoja wa wazazi na mkazi wa Kata ya Njoro Manispaa ya Moshi, ambaye anasema wazazi wasiowalipia watoto wao fedha kwa ajli ya chakula cha mchana shuleni wanarudisha nyuma maendeleo ya watoto wao.

Pia anasema watoto wanaokula chakula shuleni ambacho wazazi wao hawakuchangia fedha nao wanakula jasho la wenzao na kutoa wito kwa wazazi kuchangia.

“Pengine wazazi hawajaelewa dhana ya elimu bure na hii ni muhimu wakaeleweshwa maana si kila kitu ni bure, hata sisi wazazi tunao wajibu wa kuchangia baadhi ya mahitaji ya watoto wetu,” anasema.

NINI KIFANYIKE?

Wazazi na walezi hawana budi kujenga mahusiano na ushirikiano wa karibu na walimu ikiwamo kuitikia wito wa kuchangia fedha za chakula kwa lengo la kuwezesha wanafunzi kuwa na maendeleo mazuri darasani.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *