Kilimo cha muhogo chawanufaisha akinamama Kisarawe

Jamii Africa

TAKRIBAN kilometa 35 kutoka Ikulu ya Tanzania jijini Dares Salaam, kusini magharibi, kuna Kijiji cha Kisanga ambacho kipo Kata ya Msimbu.

Ni miongoni mwa vijiji vingi vya Wilaya ya Kisarawe katika Mkoa wa Pwani, ambacho wenyeji wake wengi ni Wazaramo, japokuwa yapo makabila mengine kwa sasa.

Kama vilivyo vijiji vingi vya wilaya hiyo, shughuli za uchumi za Kijiji cha Kisanga ni kilimo, ambacho hata hivyo kinaathiriwa na ukame ambao umeikumba Tanzania na dunia kwa ujumla kutokana na mabadiliko ya tabianchi.

Katika Kijiji cha Kisanga huwezi kupanda mahindi yakastawi na ukavuna. Kwa kifupi, huwezi kupanda mazao yanayohitaji mvua nyingi kwani zama hizo zilikwishapita kitambo na kwa sasa hakuna mvua za kutosha – si za vuli ambazo zilikuwa zikiwakomboa, bali hata za masika.

Mazao pekee ambayo wakazi wa Kisanga na vijijini vingine wilayani humo wamekuwa wakilima ni mihogo, viazi na mbaazi, kilimo ambacho hata hivyo kimekuwa cha mazowea na siyo chenye kuleta tija.

Lakini Kisanga ya sasa siyo ile ya miezi tisa iliyopita ambayo ungewakuta wakazi wake wakilima vishamba vidogo tu visivyozidi ekari moja wakichanganya mihogo, mbaazi, viazi na mahindi ambayo hata hivyo, hushindwa kumea na kunyauka kabla ya kuzaa kutokana na kukosekana kwa mvua.

Licha ya kwamba mvua zimeshindwa kunyesha, lakini hivi sasa wananchi wa Kisanga wameandaa maeneo makubwa zaidi kwa lengo la kilimo cha mihogo, ambayo wanasema imebadilisha maisha yao kwa kiasi kikubwa.

Na sasa wananchi hao wanasema hawalimi mihogo kwa mazowea ama kwa kufuata msimu wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan ambapo huuza mihogo yao mibichi kwa ajili ya matumizi ya futari.

“Hatuna haja ya kusafirisha mihogo mibichi, wanatupunja, sasa tunaicharanga wenyewe kwenye mashine kutengeneza bidhaa mbalimbali ambazo zinatupatia faida kubwa,” anasema Mwanaisha Pazi (41), mama wa watoto watano.

Mwanaisha anasema kwamba, akinamama wengi wa kijiji hicho tayari wamekwishajifunza kusindika muhogo kwa teknolojia bora ambapo stadi walizozipata zimewahakikishia kwamba wanaweza kuutumia muhogo kujiletea manufaa pamoja na kuwa na uhakika wa chakula na hivyo kukabiliana na baa la njaa ikiwa ni njia mojawapo ya kutekeleza Malengo Endelevu ya Dunia hasa ya kutokomeza njaa na umaskini pamoja na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

“Tumeanzisha kikundi cha akinamama, tumefundishwa na tumepata mashine ambazo zimetufanya tuwe na kiwanda kidogo hapa hapa kijijini, tunatengeneza unga safi na kupitia unga huo tunaongeza thamani kwa kutengeneza keki, maandazi, biskuti, tambi na bidhaa nyingine,” anasema Mwanaisha.

Aidha, anasema wanatengeneza pia chips na kwa kuukamua muhogo, majimaji yake yanatoa wanga (starch) ambao hutumika kutengeneza dawa za madoa, gundi katika samani, rangi za awali za ukuta na sukari (sugar syrup) na pia ni lishe nzuri.

“Haya yote yamewezekana kupitia katika mradi wa Green Voices, ambao unalenga kuwainua wanawake Tanzania, tunashukuru kwa sababu Kitanga sasa siyo kijiji kinachodharaulika kutokana na udongo wake mwekundu, bali kimekuwa kituo cha mafunzo kwa akinamama wengi wa wilaya ya Kisarawe ambao nao wamehamasika kupanua mashamba yao ya mihogo pamoja na kulima mtama ambao unastahimili ukame,” anafafanua.

Fikra Pevu ilitembelea kijiji hicho hivi karibuni na kukuta wananchi wakiendelea na maandalizi ya mashamba huku akinamama hao wakisindika muhogo ili kutengeneza unga na bidhaa nyingine huku wakiungwa mkono na wanaume.

Hata hivyo, mshiriki kiongozi wa kikundi hicho cha akinamama, Abia Magembe, anasema haikuwa kazi rahisi kubadili fikra za akinamama hao katika kuliongezea thamani zao la muhogo, kwani wengi walidhani wanapoteza muda wao kuliko wanavyouza mihogo mibichi.

Bi. Magembe anasema kwamba, alianza kuwaelekeza faida mbalimbali za muhogo mbali ya zile zinazojulikana kama kutafuta mbichi, kuchemsha ama kupika kama futari.

“Wengi hatuelewi kwamba muhogo unaweza kuongezewa thamani na kuzalisha bidhaa zaidi ya 300 achilia mbali kuutafuna mbichi, kuuchemsha au kuuchoma; unga wake kwa ajili ya lishe, majani yake kama mboga ya kisamvu na dawa pamoja na miti yake inapokauka kutumika kama kuni,” anasema Bi. Magembe.

Bi. Magembe, ambaye yeye pamoja na akinamama wengine 14 walipatiwa mafunzo jijini Madrid, Hispania kupitia taasisi ya Foundacion Pur Africaine Mujeres (Foundation for Women of Africa), ambayo iko chini ya Makamu wa Rais mstaafu wa Hispania, María Teresa Fernández de la Vega, anasema anashukuru kuona sasa si akinamama tu, bali wanakijiji wote wamehamasika katika kilimo cha muhogo.

“Hapa wanatengeneza bidhaa nyingi zenye ubora kama chapatti, maandazi, skonzi, biskuti, tambi, cassava chop, keki na nyinginezo nyingi… tumeliokoa zao na muhogo ambalo licha ya kuwa na manufaa makubwa kwa jamii, lakini limekuwa likidorora hata katika soko la vyakula. Hivi sasa muhogo hauwezi kuozea shambani, wala hauuzwi kwa walanguzi na wananchi wanaona umuhimu wa zao hilo,” anasema Bi. Magembe, maarufu kama ‘Malkia wa Muhogo’.

Bi. Magembe, ambaye ni ofisa mstaafu wa kilimo, anasema zao la muhogo sasa limepata thamani kubwa kijijini hapo na wana uhakika wakulima wa wilaya ya Kisarawe wanaweza kugeukia miradi kama hiyo ili kuongeza mnyororo wa thamani.

Yeyé binafsi anasema kwamba, amekuwa akijihusisha na kilimo cha mazao yanayostahimili ukame kwa miaka mingi, na ndiyo sababu baada ya kupata mafunzo akaamua kwenda kuwapati stadi akinamama wa Kisarawe ili waweze kujikwamua kiuchumi.

“Nimelazimika kununua shamba la ekari 10 hapa kwa ajili ya kilimo cha muhogo, nataka liwe shamba la mfano na kwa kufanya hivyo wananchi hawawezi kukata tamaa na kilimo hiki,” anasema na kuongeza kwamba, mbali ya kuendelea kuwaelekeza akinamama hao, lakini anakusudia kufungua kiwanda kidogo kijijini hapo ili wananchi wawe na soko la uhakika.

Silvera Mujuni, Ofisa Chakula na Lishe wa Wilaya ya Kisarawe, ameiambaia Fikra Pevu kwamba wilaya hiyo ina fursa kubwa ya kusindika na kuchakata mazao mengi yatokanayo na muhogo kwa kuwa zao hilo ndilo kuu kwa chakula na biashara.

Anasema, ardhi katika vijijini vingi vya wilaya hiyo inastawisha muhogo kwa wingi, hivyo ikiwa wananchi watajizatiti na kujifunza namna ya kuchakata bidhaa za muhogo wanaweza kupata faida kubwa kiuchumi.

“Muhogo ndilo zao kuu katika maeneo mengi ya wilaya hii ambayo haiwezi kustawisha mazao mengine kama mahindi, hivyo ni vyema wananchi wakajifunza utengenezaji wa bidhaa mbalimbali zinazotokana na zao hilo,” anasema Bi. Silvera ambaye aliwafundisha akinamama hao namna ya kutengeneza bidhaa mbalimbali zitokanazo na muhogo.

Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji wa kijiji hicho, Wazir Yakoub Wazir, amewataka akinamama hao wasajiliwe rasmi ili waweze kunufaika na mikopo inayotolewa na serikali na taasisi nyingine za binafsi, hususan fungu la asilimia 30 ambalo hutolewa na halmashauri kwa miradi ya maendeleo ya wanawake na vijana.

“Ofisi yangu iko wazi wakati wote, mkitaka kwenda kusajiliwa wilayani hata leo niko tayari kuwasaidia, nawaombeni mje niwasaidie hata namna ya kuandaa katiba ya kikundi pamoja na taratibu nyingine,” alisema.

Diwani wa Kata ya Msimbu, Anna Lilomo, kwa kushirikiana na diwani mwenzake wa viti maalum Mossy Sultan Kufurumbaya, anasema watawapigania akinamama hao kwenye vikao vya Baraza la Madiwani ili waweze kupatiwa misaada na mikopo.

“Bahati nzuri sisi hapa ni madiwani wanawake, kwa hiyo tutalipeleka suala la akinamama hawa kwenye Baraza la Madiwani na kuelezea umuhimu wa kuongeza thamani kwenye zao letu la muhogo ili limkomboe mkulima,” alisema Diwani Lilomo.

Mratibu wa Mradi wa Green Voices nchini Tanzania, Bi. Secelela Balisidya, anasema anafarijika anapoona wanawake wakihamasika kushiriki shughuli za maendeleo, hasa ujasiriamali unaolenga kupambana na mabadiliko ya tabianchi.

“Suala la kuhakikisha usalama wa chakula, kutokomeza umaskini, kuwawezesha wanawake kiuchumi na mapambano dhidi ya tabianchi ni mambo yaliyopewa kipaumbele katika Malengo Endelevu ya Dunia, hivyo wanawake wanaotekeleza miradi ya Green Voices wanayatekeleza malengo hayo kwa wakati mmoja,” anasema Secelela.

Naye Naibu Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jaffo, ambaye pia ni Mbunge wa Kisarawe, amesema yuko tayari kushirikiana na wanawake wanaosindika muhogo katika Kijiji cha Kitanga pamoja na wilaya nzima ya Kisarawe kuhakikisha wanajikwamua kiuchumi kutokana na zao hilo.

“Katika kipindi ambacho taifa linakabiliwa na ukame, tatizo ambalo limezikumba nchi nyingi duniani, kilimo kinachoendana na mabadiliko ya tabianchi ni muhimu sana, hivyo nitahakikisha wananchi wa Kisarawe wanazingatia kilimo cha mazao kama muhogo ili wajikwamue kiuchumi,” alisema.

Julai 11, 2016 wakati wa uzinduzi wa mradi wa Green Voices kwenye Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, alimhakikishia mfadhili wa taasisi hiyo, Maria Teresa de la Vega kwamba serikali iko tayari kushirikiana na akinamama kwenye mradi huo pamoja na miradi mingine yenye kuwaletea maendeleo.

“Serikali yangu itahakikisha inakuwa bega kwa bega kusaidia miradi hiyo iwe endelevu ili kuunga mkono juhudi za utunzaji wa mazingira na kupambana na mabadiliko ya tabianchi, kuongeza uhakika wa chakula, kuwakwamua wananchi na umaskini pamoja na kuongeza ajira, hasa kwa wanawake,” alisema.

Muhogo ni mkombozi

Muhogo hustawi mahali popote penye hali ya joto na mvua ya wastani na hustawi vizuri kwenye udongo wa tifutifu na kichanga.

Muhogo hustawi vizuri katika maeneo yaliyopo kwenye mwinuko wa meta 0 – 1500 kutoka usawa wa bahari. Vile vile muhogo hustawi vizuri kwenye maeneo yanayopata mvua ya wastani wa mm 750 – mm1200 kwa mwaka.

Mihogo huchukua kati ya miezi 6-8 hadi kukomaa na kufaa kuliwa. Mihogo inaweza kubaki shambani hadi miaka miwili au mitatu bila ya kuharibika kutegemea na aina ya mbegu.

Baa la njaa ni tatizo kubwa linalozikumba nchi nyingi barani Afrika, Tanzania ikiwa miongoni mwazo, lakini licha ya watu kuhimizwa kulima muhogo, bado wanalipuuza zao hilo na kuliona kama zao fulani la mizizi tu.

Katika mikoa kama Lindi na Mtwara ambayo kwa miaka mingi inalima kwa wingi muhogo, chakula chao kikuu kilikuwa ugali wa muhogo.

Licha ya kudharauliwa kwa zao hilo, lakini siyo ajabu ukakuta mlo wa siku hiyo umetokana na muhogo kasoro chumvi na nazi, kwani inawezekana kuni zilizopikia ni matawi ya muhogo, ugali wa muhogo na kisamvu cha muhogo!

Kilimo cha muhogo siyo tu kitasaidia kukuza pato la mkulima, lakini kinaweza pia kuokoa mazingira pamoja na kuisaidia Tanzania kuokoa karibu Dola za Marekani 20 milioni sawa na Shs. 42 bilioni zinazotumika kuagiza chakula nje.

Takwimu za kilimo cha muhogo duniani zinaonyesha kuwa, Afrika ni bara la tatu duniani kwa kuzalisha zaidi muhogo ambapo huzalishaji takriban tani milioni 102.6 kila mwaka.

Tanzania ni nchi ya nne kati ya wazalishaji wakubwa wa muhogo barani Afrika baada ya Nigeria, Ghana na Kongo DRC ambapo inaelezwa kwamba karibu ekari 670,000 za ardhi ya kilimo zinatumika kuzalisha muhogo, zao linalochangia karibu asilimia 15 za chakula kwa nchi nzima ambapo karibu kaya 1,213,958 huzalisha muhogo nchini.

Mikoa inayozalisha muhogo kwa wingi ni Mwanza, Mtwara, Lindi, Shinyanga, Tanga, Ruvuma, Mara, Kigoma, Pwani na maeneo yote ya Zanzibar. Ukanda wa Ziwa ni wazalishaji wakubwa zaidi ikifuatiwa na ukanda wa kusini. Mkoa wa Ruvuma huzalisha kati ya 5-10% ya uzalishaji wote Tanzania. 

Muhogo ndilo zao la pili kwa kuchangia pato la taifa kwa asilimia 19 baada ya mahindi.

Taarifa ya Shirika la Utafiti wa Viwanda na Maendeleo ya Mazao ya Chakula Tanzania (Tirdo) inaonyesha kuwa zao la muhogo linastawi kirahisi.

Hii ni pamoja na kuvumilia ukame na halishambuliwi na magonjwa au wadudu wanaoathiri mazao mengine na pia muhogo unaweza kutoa mazao mengi katika ardhi duni ambayo mazao kama mahindi hayawezi kustawi.

Kwa mujibu wa TIRDO, muhogo ni zao la pili kuwa na wanga mwingi baada ya viazi vitamu ambavyo vina asilimia 20 hadi 30 ya wanga na kwamba asilimia 84 ya zao hilo hutumika kama chakula cha binadamu.

 

1 Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *