Mafia: Minazi hatarini kutoweka, uchumi wa kisiwa kutetereka

Jamii Africa

TAMBO nyingi zimesikika kuhusu umuhimu wa nazi. Wapo wanaoipa sifa kubwa nazi kwa kuwa siyo zao la msimu.

Kwamba nazi ni zao linapatikana muda wote na kuwa na matumizi anuai.

Wengine wanatoa sifa kwa nazi kuwa ni kiungo muhimu kuongeza ladha ya chakula.

Hawakosekani wale wanaotamba kuwa nazi ina mafuta yenye ubora wa hali ya juu. Na wapo wanaoamini, maji ya madafu ni dawa.

Sifa zote hizi zinabeba ukweli kwamba nazi ni zao maarufu duniani. Kwamba mazao yake usipokutana nayo jikoni, utayakuta duka la dawa; mafuta mazuri ya ngozi na nywele, utayakuta madukani; maji ya madafu na pia mapambo; bangili za gamba la nazi.

Ni kutokana na sifa hizi, katika Tanzania na maeneo jirani, ukitaja nazi, basi hutasita kugusa maeneo inakolimwa na nazi kuvunwa kwa wingi.

Moja ya shamba la minazi Kisiwani Mafia

Sehemu hiyo ni Kisiwa cha Mafia, mkoani Pwani.

Kilimo cha minazi mbali na kuwa tegemeo la idadi kubwa ya wakazi wa kisiwa hicho wapatao 46,438 kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012, nazi za Mafia zinazotegemewa na wakazi wa Dar es Salaam na Zanzibar.

Hali kadhalika nazi zinazopatikana kisiwani Mafia pia husafirishwa hadi Mombasa nchini Kenya pamoja na Kisiwa cha Comoro, jambo linalolifanya zao hilo kuwa tegemeo hata kwa watu ambao si wakazi wa Mafia.

Kwa maana nyingine, kilimo cha minazi ndiyo uti wa mgongo wa Mafia kilichopo umbali wa kilometa 131 au maili 81, Kusini mwa Jiji la Dar es Salaam.

Machapisho mbalimbali yanaeleza kuwa, mnazi ambao kitaalamu hujulikana kama Cocos nucifera uliingizwa kisiwani humo mnamo karne ya 16 wakati wa utawala wa Waarabu.

Kuingia kwa nazi Mafia

Inaelezwa kuwa, Waarabu ndiyo waliosambaza zao hilo katika maeneo mbalimbali nchini hasa ukanda wa pwani kama vile Tanga, Bagamoyo, Unguja na Pemba kwa kutaja baadhi.

Tangu kipindi hicho hadi sasa, zao hilo limekuwa tegemeo la kiuchumi kwa wananchi wa Mafia, ambapo ukiacha mashamba rasmi, kila nyumba ina wastani wa minazi miwili au mitatu.

Pamoja na umuhimu wake, zao hilo sasa lipo hatarini kutoweka kutokana na sababu mbalimbali.

Ukataji mbao

Kwa mujibu wa Kombo Shomari, mkazi wa Kijiji cha Kanga wilayani humo anasema, ukataji wa minazi kwa ajili ya kuzalisha mbao unatishia uhai wa zao hilo.

Geriad Mgoba, Ofisa Kilimo wa Halmashauri ya Wilaya ya Mafia.

Anasema kutokana na tatizo la mbao kisiwani humo baadhi ya watu wameanza kukata minazi na kuzalisha mbao kwa ajili ya kutengeza samani na ujenzi.

“Watu wameanza kukata minazi kuzalisha mbao, hali hii isipodhibitiwa muda mfupi ujao, kilimo cha nazi Mafia kitabaki historia,” anasema Shomari.

Anaeleza anaiambia FikraPevu kuwa kuna uwezekano wa kuongezeka kwa kasi ya ukataji wa minazi kwa ajili ya mbao kutokana na mwamko wa wananchi hasa katika ujenzi wa nyumba za kisasa, hivyo kuongeza mahitaji ya mbao.

Shomari anasema kuwa, “Mafia hakuna miti mikubwa ya kupasua mbao, mbao zinaletwa kutoka maeneo mengine nje ya hapa kama vile Dar es Salaam, hivyo ni rahisi mtu kukata mnazi wake kupasua mbao kwa ajili ya kupunguza gharama za ujenzi”.

Kwa upande wake, Omari Shaabani mkazi wa Chunguruma anaiambia FikraPevu kuwa kupanuka kwa shughuli za ujenzi kisiwani humo pia kumechangia mashamba ya minazi kugeuzwa viwanja.

Anasema baadhi ya minazi imekuwa ikikatwa kuwawezesha watu kupata viwanja kwa ajili ya ujenzi wa makazi, jambo ambalo husababisha athari kwa kilimo hicho.

Mingi imezeeka

Mbali na tatizo la ukataji wa minazi kwa ajili ya mbao au kupata viwanja kwa ajili ya ujenzi wa makazi, sababu nyingine inayochangia kulifanya zao la minazi kuwa katika hatari ya kutoweka ni kuzeeka kwa minazi mingi kisiwani humo.

Mzee Thabiti Mfaume, mkazi wa Kichangachui anasema idadi kubwa ya minazi kisiwani humo kwa sasa imeezeka.

Anaieleza FikraPevu kuwa minazi mingi iliyopo ina na umri kati ya miaka 70 hadi 100 na kwamba baadhi yake hata uzalishaji wake wa nazi umepungua.

“Minazi mingine imezeeka, mimi nina miaka 70 mingi nimeikuta imepandwa na mingine inapandwa nilikuwa naiona nikiwa mdogo, kama mimi nipo hivi yenyewe itakuwa na hali gani,” anaeleza Mzee Mfaume.

Anaongeza kuwa, “zamani mnazi mmoja ulikuwa na uwezo wa kupata hata nazi 200 kila unapovuna (Jangusho), lakini hivi sasa mnazi mmoja unaweza kupata nazi 50 hadi 70, kwa sababu imezeeka na mingine haina matunzo mazuri”.

Kauli yake inaungwa mkono na Fatuma Athumani mkazi wa Bwejuu kupitia FikraPevu ambaye anasema mbali na kuzeeka kwa minazi, pia hakuna utashi miongoni mwa vijana wa  kujiingiza kwenye kilimo hicho.

Anasema mashamba mengi yaliyopo wamiliki wake walio wengi wameyarithi kutoka wazazi au babu zao, na kwamba hakuna vijana wanaojiingiza katika kilimo cha minazi kwa maana ya wao kufungua mashamba mapya.

Anasema sababu kubwa inayowafanya kutojiingiza katika kilimo hicho wengi wao wana mtazamo kwamba inachukua muda mrefu hadi kutoa mazao hivyo watachelewa kupata matunda yake.

Uvunaji wa nazi

FikraPevu kupitia machapisho mbalimbali na wazee wa Mafia, inathibitisha kuwa zao la mnazi huchukua kati ya miaka mitano hadi sita tangu inapopandwa hadi kuanza kuvunwa, baada ya hapo huweza kuvunwa kila baada ya miezi mitatu, uvunaji ambao hujulikana kama jangusho.

Hakuna upandaji mpya

Wakati idadi kubwa ya minazi kisiwani Mafia ikiwa imezeeka inaelezwa kuwa, hakuna kasi kubwa ya kupanda minazi mipya au kurudishia ile iliyokufa (gap filling).

Kassimu Matimbwa mkazi wa Kilindoni anaiambia FikraPevu kuwa kasi ya kuzeeka kwa minazi kisiwani humo haiendani na upandaji wa minazi mipya ili kulifanya zao hilo kuendelea kuwa endelevu kwa miaka mingi ijayo.

Anasema kama wananchi kisiwani humo wataendelea na hali iliyopo sasa ya kutopanda minazi mipya na kurudishia ile iliyokufa kuna uwezekano wa kupotea kwa zao hilo, hivyo kusababisha hali ngumu kwa wananchi kiuchumi.

“Minazi mipya inayopandwa ni kidogo kuliko inayozeeka, hata pale ambapo mnazi umekufa wakulima hawana utaratibu wa kurudishia mnazi mpya, ukipita katika mashamba utaona kuna minazi mingi imekufa na haijarudishiwa,” anaieleza FikraPevu.

Anasema endapo hakutakuwa na juhudi za makusudi za kuokoa kilimo cha minazi, kuna hatari ya zao hilo kisiwani Mafia kutoweka kama ambavyo zao la korosho lilivyotoweka.

Matimbwa anasema hadi kufikia mwanzoni mwa miaka ya 2000, wilaya ya Mafia ilikuwa miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa korosho mkoani Pwani lakini matatizo mbalimbali kama kukosekana kwa soko la uhakika na kutopandwa miche mipya kumechangia kufa kwa zao la korosho.

Soko limetawaliwa na walanguzi

Ukiacha tatizo la kuzeeka kwa minazi, ukataji mbao na kutopandwa kwa miche mipya, changamoto nyingine inayolikabili zao hilo ni soko lake kutawaliwa na walanguzi (middle man).

Nazi zikiwa zimevunwa.

Mkazi wa Kigamboni kisiwani humo Abdulrahmani Mbonde anaiambia FikraPevu kuwa pamoja na kwamba Mafia inazalisha nazi nyingi lakini soko lake limeshikwa na walanguzi hivyo kushindwa kutoa tija ya kutosha kwa wananchi hasa wakulima.

Anasema hakuna mfumo rasmi wa kuuza nazi badala yake wanunuzi wanafika kwa wakulima au kuwatumia madalali kununua na kusafirisha maeneo mbalimbali utaratibu ambao hauna tija hata kwa halmashauri ya wilaya kwa kuwa nazi nyingi hutoroshwa bila kulipiwa ushuru.

“Nazi ya Mafia inalika maeneo mbalimbali kama Dar es Salaam na Zanzibar, lakini soko lake limeshikwa na walanguzi, wao ndiyo wanapanga bei, tena nazi nyingi husafirishwa kwa siri ili kukwepa ushuru,” anasema.

Mbonde anasema kukosekana kwa usafiri wa uhakika kati ya Mafia na maeneo mengine ya nchi kunachangia walanguzi kushika hatamu katika biashara ya nazi na hata kutoroshwa kwa kutumia usafiri wa majahazi.

Kwa mujibu wa takwimu za ofisi ya kilimo na mifugo katika Halmashauri ya Wilaya ya Mafia katika msimu wa kilimo wa mwaka 2015/16 jumla ya tani 37,000 za nazi zilivunwa.

Kiasi hicho ni ongezeko la tani mbili ikilinganishwa na tani 35,000 zilizovunwa katika msimu wa kilimo wa mwaka 2013/14 kisiwani humo.

Kauli ya serikali

Ofisa Kilimo wa Halmashauri ya Wilaya ya Mafia, Geriad Mgoba anakiri zao hilo kukabiliwa na changamoto nyingi ambazo zinatishia uhai wake.

Anazitaja changamoto hizo ni kuwepo kwa mashamba pori (mashamba ya minazi yasiyohudumiwa), ukataji mbao na kutopandwa kwa miche mipya ya minazi.

Mgoba anafafanua kwa FikraPevu kuwa halmashauri imeanza kuchukua hatua zinazolenga kukifanya kilimo cha minazi kuwa endelevu kisiwani humo.

Anazitaja baadhi ya hatua hizo ni kuhamasisha wakulima kupanda miche mipya katika maeneo ambayo minazi imezeeka (gap filling).

Ofisa kilimo huyo anaeleza kuwa, tayari halmashauri imeandaa miche 1,000 ya minazi aina ya Africa Tall Giraffe ambayo itagawiwa kwa wakulima.

“Africa Tall Giraffe ni aina ya mbegu za minazi ambazo huchukua kati ya miaka mitano hadi sita kati ya kupanda na kutoa mavuno, tunawashauri wananchi wapande hizi kwa kuwa zinakaa miaka mingi na zikiendelea kutoa mavuno mazuri,” anasema Mgoba.

Ofisa kilimo huyo anabainisha kuwa, miche hiyo itagawiwa kwa wananchi wenye mashamba ya minazi ili waweze kurejeshea ile iliyokufa na kwamba mkakati huo pia unakwenda sanjari na kuhamasisha wakulima kuanzisha vitalu vya mbegu za minazi.

Anasema halmashauri inafahamu tishio linalokikabili kilimo cha minazi na kwamba imechukua hatua mbalimbali kukabiliana na hali hiyo.

Mgoba anaiambia FikraPevu kuwa baadhi ya hatua zilizochukuliwa ni pamoja na kupiga marufuku minazi kukatwa mbao ambapo mwananchi anatakayebainika anachukuliwa hatua ikiwemo kufikishwa mahakamani, kuanza kuzalisha miche na kuigawa kwa wananchi na kutoa elimu ya kilimo bora cha minazi.

Kwa mujibu wa ofisa kilimo huyo juhudi za halmashauri hilo ndiyo zimechangia kuongezeka kwa uzalishaji katika msimu wa kilimo wa mwaka 2015/16, kutokana na wananchi kuhamasishwa kufyeka na kupalilia minazi ili kuondoa mashamba pori.

Kwa upande wa soko, Mgoba alieleza kuwa, zao hilo linakabiliwa na changamoto kubwa kwa kuwa hakuna chombo rasmi kinacholisimamia kama ilivyo korosho au kahawa, jambo ambalo hutoa mwanya kwa walanguzi kufaidika na biashara ya nazi.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *