Ukizunguka vijijini ambako ndiko hasa kilimo kinaendeshwa, unaweza kustaajabu na kujiuliza endapo bado upo katika nchi ile ile yenye mipango na mikakati mingi yenye kuvutia na kauli mbinu za kila namna. Uhalisia ni tofauti sana na kinachohubiriwa. Kilimo kimepewa kisogo, mkulima ametelekezwa na kusahauliwa kabisa. Huo ndio ukweli mchungu.
Ni aibu na simanzi kuona mpaka karne hii wakulima ambao wana utashi na ari ya kushiriki katika shughuli za kilimo (ikiwemo ufugaji na uvuvi) wanakosa pembejeo za kilimo. Licha ya fedha zao mkononi; bidhaa haimo madukani. Hata uwepo wa maduka ya zana za kilimo na mifugo vijijini ni kitendawili.
Na mahala ambapo kuna maduka, tunadiriki kuleta pembejeo feki. Tunadiriki kufanya ufisadi katika pembejeo! Na zaidi kukosa uongozi wa kuhakikisha pembejeo na zana za kilimo zinaenda sambamba na msimu wa kilimo chenyewe! Bado tunaibuka usingizini na kughani matamanio tusiyoweka katika uhalisia wa kupata matokeo makubwa sasa!
Ni kweli, kwa miaka ya hivi karibuni kumekuwa na juhudi za dhati na matamanio ya kiserikali ya kuimarisha kilimo. Lakini kwa kiasi kikubwa zinagonga mwamba. Bado rushwa na wizi vimekithiri katika pembejeo za kilimo zinazoelekezwa kukwamua kilimo huku viongozi wakiangalia au kushiriki katika dhuluma hiyo.
Viongozi wanaona soni kusimama na kumtetea mkulima, kutetea haki ya mvuja jasho anaowafanya washibe. Hakika ule usemi wa; “aliyeshiba hamjui mwenye njaa” unajidhihirisha katika watawala wetu. Ndiyo, ni watawala na si viongozi tena kwa kukosa kujali wale ambao wanapaswa kuwapigania.
Ni kweli; kumtetea mkulima yahitaji uimara hasa kwa jamii inayoongozwa na wanaojiita "watoto wa wakulima" ambao wamesahau wakulima ila makini katika kukumbuka kupiga. Wenye uthubutu wakukiri hadharani tena katika mhimili mtukufu kuwa wameshachoka (sijui wamechoka kuongoza?) na hivyo; "wapigwe tu"!
Na huko ndiko ziliko fikra, nguvu na maarifa yao wanayaelekeza (kupiga) na kusahau kuhakikisha kuwakwamua wakulima ambao ndio wengi nchini na wenye kuishi katika hali duni.
Hao ni wao; ila kila mwananchi anapaswa asijisahau. Tunapaswa kutowasahau wakulima, wafugaji na wavuvi. Shibe yetu ni kutokana na jasho na kazi ngumu wazifanyazo kila uchao katika mazingira magumu sana.
Licha ya changamoto na ugumu huo wote wanaendelea kuzalisha, bado hawafanyi mgomo wa kulima au kufuga. Au hata kuamua siku kugoma kuuza mazao yao; tena hasa kuwauzia wananchi katika miji mikuu.
Lakini kila uchao tumewapa kisogo. Hatujali hata kuimarisha upatikanaji wa zana na pembejeo za kilimo ili tuweze kuzalisha na kupata zaidi na zaidi ambacho ndicho kitufae sote na kupata shibe.
Tuchukue mfano; asasi zisizo za kiserikali (AZAKI) mbalimbali ambazo zina uchache wa kibajeti kulinganisha na bajeti ya taasisi za kiserikali husika zinaweza kuwasimamia na kuwasaidia wakulima na wafugaji kwa kiwango cha kupigiwa chapuo. Kwanini? Hapo kuna funzo kuu! Msingi si udogo wa bajeti bali ni udhihilishwaji wa dhamira, ari na msukumo unaowekwa na watendaji na viongozi katika kuhakikisha ustawi na kukuwa kwa kilimo na ufugaji nchini si wa kiwango cha kuridhisha. Hawamaanishi kile wanachokihubiri!
Hivi karibuni, niliweza kutembelea na kujionea juhudi na mchango wa shirika la ActionAid-Tanzania ambalo lilishirikiana na vikundi na AZAKI za Pemba mathalani taasisi ya wakulima wa karafuu (ZACPO) ambapo walisimamia kuhakikisha bei ya zao la karafuu inakuwa kwa maslahi ya wakulima na kumudu kuipandisha toka iliyokuwapo TZS 3,500/- kwa kilo moja hadi TZS 13,000/-. Ongezeko ambalo linakuwa faraja hasa kwa wakulima na kuwapa hata shime katika uzalishaji. Au kutetea bei ya mwani ambapo awali ilikuwa TZS 120/- kwa kilo moja hadi kufikia TZS 400/- kwa kilo moja.
Mifano kama hii ipo mingi; ingawa bado kwa upekee wa mchango wa AZAKI haitoshi. Mchango wa AZAKI mbalimbali zinadhihirisha inawezekana kuleta mabadiliko chanya na yenye tija kwa sekta ya kilimo na hasa kumkwamua mkulima hasa wakulima wadogo wadogo.
Ni ukweli taasisi za kiserikali kama SIDO na nyinginezo zimekuwa zikiendesha mafunzo na kuwajengea uwezo hasa wakulima kuhakikisha wanazalisha mazao na kuyaweka katika kiwango cha hali ya juu tayari kwa kutumika “fine products”. Lakini bado wafanyabiashara na wawekezaji hawajawekeza nguvu za kutosha kuhakikisha bidhaa za kufanikisha tunazalisha na kutengeneza mazao yetu katika hali ya kutumika “fine products” zinapatikana kwa urahisi na unafuu hasa vijijini. Kwani wakulima wengi wamekuwa na kilio cha muda mrefu cha ukosefu wa vifungashio na vifaa vingine ambavyo ni nyenzo muhimu katika kuhakikisha mazao yao yanaingia sokoni katika hali itakayowapa faida zaidi kuliko sasa.
Lazima tuseme inatosha! Tuseme wakati ni sasa kuhakikisha tunahakikisha kilimo chetu kinawakwamua hasa wakulima wadogo wadogo. Kila mwenye shibe ahakikishe anafikiri mbinu ya kuhakikisha mkulima anakwamuka katika hali duni aliyopo. Na kwa viongozi; kuhakikisha wanasimamia kwa ukaribu utekelezaji wa sera na mipango tulizojiwekea ili tupate matunda halisi tunayo yatamani.