Pengo la walionacho na wasionacho linavyowanufaisha wanasiasa

Jamii Africa

Tanzania imekuwa na ukuaji mzuri wa uchumi lakini changamoto kubwa ni kuongezeka tofauti ya kipato kati wananchi wa kipato cha chini na matajiri hali inayoweza kuathiri mchakato wa kufikia uchumi wa viwanda.

Tofauti hiyo ya kipato inasababishwa hasa na kutokuwa na usawa katika ugawaji wa rasilimali za taifa, huku sehemu kubwa ya utajiri wa nchi ikienda mikononi mwa watu wachache ambao wana nguvu ya kisiasa na kiuchumi.

Ikiwa watu wachache wanamiliki uchumi wa taifa na njia kuu za uzalishaji na kuiacha idadi kubwa ya watu hawana umiliki au wanamiliki sehemu ndogo ya keki ya taifa huzua matatizo mengi yasiyoisha ambayo yanaweza kuligharimu taifa ambalo limeimarisha utulivu na amani kwa muda mrefu.

 Umaskini haukwepeki lakini ni kwa kiasi gani utajiri na rasilimali za taifa zinawanufaisha wananchi wote kwa usawa bila kuacha manung’uniko kwa wananchi ambao hutengeneza chuki dhidi ya viongozi waliowaweka madarakani. 

Kelele hizi zinazopigwa leo na viongozi wetu kuwa tudumishe na kuilinda amani ya nchi bila kuwapatia wananchi haki zao itakuwa ni bure kwasababu amani ni zao la haki. Mwananchi wa kawaida atadumisha amani kama anaona haki ipo na anapata kile anachostaili.

Tofauti ya kipato kati ya walionacho na wasionacho ambayo ianaongezeka siku baada ya siku haiwezi kudumisha amani kwa maneno matupu yasio na vitendo. Vijana wengi leo hawana ajira na wananchi wanalalamika na kuumia kwa sababu watu wachache wanatumia rasilimali za nchi kwa manufaa yao binafsi.

Tafiti mbalimbali zinaonyesha uwiano wa kipato katika matajiri na masikini sio mzuri.  Tofauti ambapo ni zaidi ya 1 kwa 50. Mathalani  ikiwa mtu wa juu anapata mshahara millioni tano(5000000/-) basi mtu wa chini anapata shilingi laki moja (100,000/-). 

Tofauti hiyo ni kubwa na ina athari kwa uchumi ikizingatiwa kuwa mzunguko wa mapato huishia mikononi mwa watu wachache huku kundi kubwa la watu likitaabika.

Tatizo liko wapi?

 Suala hili la tofauti kubwa ya kipato ni la kihistoria. Mwalimu Julius Nyerere wakati anaingia madarakani mwaka 1961 alikuta tofauti kubwa ya kipato kati ya wasionacho na walionacho ambayo inalingana na hali ilivyo sasa ambayo viongozi wetu wamejisahau kuwa wanatengeneza jamii ambayo itafika wakati itakuwa vigumu kutawalika.

Mwalimu Nyerere kwa busara na moyo wa kizalendo aliokuwa nao hakukubali hali hiyo iendelee lakini alifanya mabadiliko makubwa katika mfumo wa kuongoza nchi ili kila raia apate haki sawa katika matumizi ya rasilimali za nchi. Alifanikiwa kupunguza uwiano wa kipato hadi kufikia 1 kwa 6 (1:6)  ikiwa  mtu wa juu anapata laki sita (600,000/-) basi mtu wa chini alipata shilingi laki moja (100,000/-).

Mnamo mwaka 1967 wakati wa utekelezaji wa sera ya ujamaa uliposhika kasi, ilisisitiza usawa na haki kwa wananchi wote bila kujali nafasi zao katika jamii. Uongozi bora Mwalimu Nyerere ukaleta mageuzi makubwa katika maisha ya wananchi mbayo kwa kiasi kikubwa yalikuwa yanafanana na kazi kubwa ilikuwa kuimarisha utaji wa huduma za jamii.

Tofauti hiyo ndogo iliwafanya watu waishi kwa amani na mshikamano huku wakishiriki kutatua matatizo ya nchi na kuleta maendeleo.  Lakini baada ya Mwalimu Nyerere kuondoka madarakani, viongozi waliofuata wakakubali kuingiza nchi katika mfumo wa kibepari ambao unawapa watu uhuru wa kumiliki mali watakavyo bila kuingiliwa na mtu, ndipo tofauti ya kipato ikaanza kujitokeza.

Kutokana na uhuru ulioletwa na ubepari, viongozi walioaminiwa kuwa watalinda maslai ya watanzania bila kujali nafasi zao katika jamii, walibadilika na  kutumia mali ya umma kujitajirisha wao na familia zao.  

Wengi wakajiuzia mashirika ya umma, wakagawana ardhi kama njugu na kuwalazimisha watu kuondoka katika maeneo ambayo yalikuwa na rutuba nzuri wakidai wanawapa wawekezaji wayaendeleze na kuleta maendeleo katika taifa.

Hata hivyo, viongozi hao wanasiasa wanaendeleza siasa za ubaguzi katika upatikanaji wa huduma za jamii ambapo zinatolewa kama hisani na sio haki ambazo wanatakiwa kuzipata.

Tofauti ya kipato bado inaongezeka na hili linachukuliwa kama suala la kawaida kwasababu hutuoni jitihada za viongozi kuleta usawa katika jamii na nchi inazidi kutafunwa na  hivyo kuhatarisha usalama wa nchi.

Wengi wanaona kama nchi bado ina amani na mambo yanaenda vizuri lakini kwa wadadisi wa mambo wanapatwa na mashaka na jinsi athari za kuongezeka kwa tofauti ya kipato zinavyoweza kuligharimu taifa.

Athari inayojitokeza kwa kasi ni ongezeko kubwa la vijana wasio na ajira ambao hata wakijaribu kujihusisha na biashara ndogondogo katika maeneo mbalimbali bado vigogo wa  nchi huwafuata na kuwaondoa katika maeneo ya biashara. 

Tumeshuhudia vurugu kubwa za wafanyabiashara katika majiji ya Mwanza na Mbeya wakipambana na polisi na kusababisha uharibifu wa mali na vifo kwa baadhi ya watu. Wengi wao ni vijana ambao wameshindwa kuendelea na masomo au wanatoka katika familia za masikini.

Ni wakati sasa kwa watanzania kuamka na kukataa hali hii iendelee kwa sababu nchi hii ni yetu na  tuna haki ya kutumia rasilimali zetu kwa maendeleo ya watanzania. Tukiacha mambo yaendelee kama yalivyo tunatengeneza bomu ambalo madhara yake yatakuwa ni makubwa na hakuna ambaye ataweza kuirejesha nchi katika hali ya mshikamano kama ilivyo sasa.

 Tujifunze kutokana na makosa ya wenzetu na tukumbuke kuwa amani ni zao la haki na upendo katika jamii na sio maneno yasiyo na vitendo.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *