Kilio cha wapanda pikipiki kwa askari wanaolinda mgodi wa Shanta

Kulwa Magwa

BAADHI ya wapanda pikipiki wa kijiji cha Sambaru, mkoa wa Singida, wamesema wamekuwa wakikamatwa na baadhi ya askari wanaolinda mgodi wa Shanta ambapo huwapotezewa muda na kuwatoza rushwa ili wawaachilie.

 Kwa mujibu wa wapanda pikipiki waliozungumza na mwandishi wa habari hii, kuna wakati wanalazimika kutumia njia za vichochoro kukwepa kukamatwa na askari hao.

 Suleiman Hamis, alisema amekuwa akikwepa kukutana na askari hao uso kwa uso anapokuwa na pikipiki kwa kuwa wanapomsimamisha humbana maswali ambayo huyachukulia kuwa kero kwake.

“Hawa askari wapo hapa kulinda mgodi, hatukatai kwamba wanapaswa pia kuhakikisha usalama wetu, lakini wakikukamata na pikipiki huwezi kuondoka hivi hivi bila kuwaachia chochote (rushwa). Sasa hilo ndilo jukumu lililowaleta hapa?” alihoji Hamis.

Naye Yusuph Mdizi, mkazi wa kijiji jirani cha Londoni, wilayani Manyoni, alisema askari hao wanapokuwa wameegesha gari lao pembeni mwa barabara kuu, ni nadra wapanda pikipiki kupita sehemu hiyo.

Alisema, ukamataji wa pikipiki umekuwa ukiwakera na kuwapotezea muda, ambapo hulazimika kutoa chochote ili waachiliwe waendelee na shughuli zao.

“Mimi nimekamatwa mara nyingi sana na hao askari ila kila wakikukamata utasikia wanakuambia bwana bila chochote huondoki. Yaani jamaa zetu hawa ni kero kubwa kwetu watu wa pikipiki, “alisema mpanda pikipiki huyo.

Kwa upande wake, Hassan Mtigoo, alisema hivi karibuni kuwa akiwa na abiria, alisimamishwa na askari wawili waliokuwa njia panda ya kwenda ‘saiti’ ya kampuni hiyo ambao walimuomba leseni na alipowapa walimtaka ampeleke mtu aliyekuwa naye kisha arejee kwa mahojiano.

Alisema, baada ya kumfikisha abiria aliyekuwa akimpeleka Ikungi (umbali wa kilometa 53) alirejea na kuwakuta askari hao ambao walimtaka awapatie fedha kwa maelezo kuwa vioo vya taa za nyuma za pikipiki yake vilikuwa vimepasuka.

“Nilitoa sh. 10,000 wakaniambia niende zangu, lakini wakanionya lazima niweke taa mpya ili wasinikamate tena. Hilo ni kosa, lakini hiyo waliyoniomba nayo si rushwa?”alisema Mtigoo.

Naye Herbert Bisanga wa Londoni, alisema kila anapokuwa na pikipiki yake, macho yake huangaza walipo askari ili asimkamatwe.

Alisema amewahi kukamatwa na askari mara nyingi akiwa na pikipiki anayotumia kusafirishia mawe na mchanga wa dhahabu kupeleka kusagiwa na kuosha, na mar azote alilazimika kutoa ‘kitu kidogo’ kuachiwa.

“Hatuwalaumu sana hao askari maana mazingira yetu tunayoishi yanawashawishi waombe fedha kwa kuwa wanajua hili ni eneo la machimbo ya dhahabu na kila wanayemuona na pikipiki wanaamini ana hela wakati wao hawana kitu, “alisema Bisanga.

waendeshaji

PICHA: Wachimbaji wadogo Herbert Bisanga na Hassan Said, wakionyesha eneo 'hatari' ambalo hawapaswi kufika ambalo liko chini ya Shanta Mining. Eneo hilo linalindwa na polisi na walinzi wa kampuni binafsi ya Venture Sucurity

Elifuraha Japhet wa Mang’onyi alisema, hajawahi kukamatwa na askari hao, lakini baadhi ya wapanda pikipiki wenzake hukamatwa na kutozwa fedha bila risiti.

Alisema, mara nyingi matukio ya ukamataji pikipiki hufanyika katika maeneo yaliyo jirani na mgodi, maana ndiyo yanayokuwa chini ya ulinzi wa askari hao.

Mchimbaji mdogo, Hassan Said, alisema miezi michache iliyopita alikamatwa akiwa na pikipiki alipokuwa akisafirisha mawe ya dhahabu kwenda kuyasaga katika eneo la Londoni, ambapo askari waliyataifisha na kumuacha aondoke na pikipiki yake.

“Niliumia sana moyoni maana lile lilikuwa jasho langu ambalo nimelihangaikia, hali imepoa kidogo siku hizi maana zamani pikipiki ikikamatwa mpaka uirejeshe ilikuwa kazi kweli, “alisema.

Said alisema pikipiki zilipokuwa zinakamatwa zilipelekwa katika ‘saiti’ ya Shanta ambapo ziliwekwa mpaka wamiliki walipozifuatilia na wakati mwingine kuzipata baada ya kutoa rushwa.

“Hilo (suala) nalo lilijenga maswali vichwani mwetu, yaani mtu unakamatwa halafu unapelekwa na pikipiki yako pale Shanta, hivi pale ni kituo cha polisi? Ndiyo maana watu wengi wanahisia mbaya kuhusu mgodi huo, “anasema Said.

Akizungumzia suala hilo, Khamis Shaaban, alisema tofauti na zamani, siku hizi ni mara chache amekuwa akiona wapanda pikipiki waliobeba mkaa ndio wanaokamatwa na polisi.

Alisema, baadhi ya watu wanaokamatwa huwa wamebeba magunia ya mikaa hiyo wakiitoa porini kuipeleka vijijini au Ikungi.

“Wanapokamatwa nasikia wanatozwa hela, utasikia huyu anasema ametoa sh.10,000 mwingine atakuambia sh.5,000. Hao wanakamatiwa njiapanda ya kwenda ‘saiti’ ya kampuni maana pale ndipo askari wanakuwepo muda mwingi, “ alisema Shaaban.

shaaban

PICHA: Meneja wa Wachimbaji Wadogo wa Sambaru, Stanley Shaaban, akizungumzia ukamataji wa pikipiki unaofanywa na baadhi ya askari wanaolinda mgodi wa Shantaa Mining, katika eneo la Sambaru, mkoani Singida

Idd Salum alisema, baada ya ‘saiti’ ya Shanta Mining kuvamiwa na watu na wasiojulikana na kuharibiwa mali zake, Februari mwaka huu, wapanda pikipiki wengi walikuwa wakikamatwa na polisi na walinzi wa mgodi ambapo waliachiwa baada ya kuhojiwa.

“Siku hizi nasikia mara chache, lakini wapo wanaolalamika kuwa wanakamatwa ila sio kama zamani,“ alisema Salum.  

 Akizungumzia suala hilo, Meneja wa Wachimbaji Wadogo wa Sambaru, Stanley Shaaban, alisema kwa muda sasa hajasikia wala kupata malalamiko ya wapanda pikipiki wanaolalamikia kukamatwa na askari, lakini kipindi cha nyuma ilikuwa kero mojawapo kubwa katika sehemu hiyo.

Hata hivyo alisema katika siku za hivi karibuni askari wamekuwa wakipiga mara kwa mara risasi hewani nyakati za usiku katika eneo lililozuiliwa wachimbaji wadogo kuchimba, suala ambalo limekuwa likizidishia hofu miongoni mwao.

Alisema, kati ya Oktoba 7 hadi 10, mwaka huu, askari hao walifyatua risasi mara nne nyakati za usiku katika eneo lililoko jirani na eneo wanalochimba.

Shaaban alisema, walipoanza kufanya hivyo, kesho yake asubuhi walifika katika kituo cha wachimbaji wadogo kilichoko kando ya eneo hilo ambapo walimueleza kuwa ufyatuaji huo wa risasi umekuwa ulilenga kufukuza  wavamizi waliokwenda kuchimba dhahabu katika sehemu inayomilikiwa na Shanta.

Alisema, baada ya kumueleza hivyo, walimtaka aorodheshe majina ya wachimbaji wote kwenye karatasi na kuwakabidhi, pamoja na kumtaka awaambie wachimbaji  kuwa kila mmoja awe mlinzi wa mwenzake, vinginevyo wangesambaratisha kambi yao.

“Sisi kwenye kambi yetu tangu tulipopigwa marufuku tusichimbe sehemu hiyo, hakuna mtu hata mmoja aliyewahi kusogelea na hata wao nimewahakikishia hivyo, kwani watu hawaogopi kufa? Hakuna mtu anaweza kwenda sehemu ambayo ina moto, “alisema Shaaban.

Shaaban alisema risasi zimekuwa zikisikika mara kwa mara sehemu hiyo, lakini hazijawahi kusababisha madhara makubwa kwa wachimbaji.

“Ni mara moja tu watu walitimulia mbio usiku waliposikia risasi zinapigwa na baadhi yao wakaumia kwa sababu walijikwaa kwa kuparamia miti na visiki, lakini hakuna vifo au majeraha makubwa ya kutisha yaliyotokea, “alisema.

pikipiki

PICHA: Pikipiki ikiwa imefichwa nyumba ya ukuta wa nyuma jirani na 'saiti' ya Shanta Mining. Mpaka pikipiki hiyo aliamua kuificha ili asikamatwe na polisi wanaolinda sehemu hiyo alipompeleka mwandishi wa habari hii kuonana na uongozi wa kampuni hiyo

Mfanyakazi wa Shanta Mining aliyezungumza kwa sharti la kutotajwa jina lake, alisema uhusiano wao na wanakijiji sio mzuri sana kutokana na malalamiko ya wananchi kutotekelezwa na mwajiri wao.

Alisema, tangu tukio la uvamizi katika mgodi huo lililotokea Februari, mwaka huu,  walilazimika kuimarisha ulinzi ambapo hali hiyo imetofasiriwa na baadhi ya wanakijiji kuwa inalenga kuwanyanyasa.

“Mbona watu wanapita tu katika eneo hili (jirani na mgodi) ila mtu akiwa na makosa na tunamjua kwa vyovyote vile hapa hawezi kupita. Tutamkamata. Unajua wapo watu waliwahi kutushambulia siku za nyuma tunawajua na hata polisi wanajua matukio hayo, hivyo hao hatuna urafiki nao, “alisema mfanyakazi huyo.

Naye mlinzi wa kampuni binafsi ya Venture Security inayolinda mgodi huo, ambaye hakutaka kutaja jina, alikanusha kuwa kuna ukamataji wa wapanda pikipiki katika maeneo yanayozunguka mgodi.

Alisisitiza kwamba wanachofanya ni kuimarisha ulinzi kila uchao kwa kubuni mbinu mbalimbali za kukabiliana na wavamizi.

“Huko mtaani tunazungumzwa vibaya sana wakati mwingine hata kwenda kutembea tunapata wakati mgumu, mimi huwa sitoki mpaka ninapochukua likizo nakwenda Singida mjini,”alisema mlinzi huyo akimaanisha kuwa muda mwingi anautumia kambini.  

Mtendaji wa Kijiji hicho, Bernard Nkhomee, alisema imepungua kutokana na ushirikiano mzuri ulioanzishwa na serikali ya kijiji, pamoja na jeshi hilo ili kulisaidia kutekeleza majukumu yake kwa urahisi.

Nkhomee alisema, baada ya tukio la uvamizi katika mgodi lililofanywa na watu aliodai wanatoka vijiji jirani, askari walikuwa wakiendesha upekuzi wa mara kwa mara barabarani na kijijini, lengo likiwa kusaka vielelezo vya ushahidi wa kesi walizowafungulia watuhumiwa, pamoja na vitu vilivyoporwa mgodini.

“Na pia ni muda mrefu kidogo sijaona wala kusikia malalamiko ambayo ni rasmi kutoka kwa wananchi, japokuwa yale malalamiko ya barabarani yanasikika sana. Tunajitahidi kuzungumza na wenzetu hawa (wa Jeshi la Polisi) ili wasiwe wanawabughudhi wananchi,  alisema mtendaji huyo.

Alikiri kuwa hata hayo malalamiko wanayosikia ‘barabarani’ yanawaumiza viongozi wa kijiji, ndiyo maana katika vikao wanapokutana na viongozi wa juu hulizungumzia suala hilo.

“Lakini (malalamiko) yakiwa makubwa tunaweza kumwambia OCD (kamanda wa polisi wa wilaya) maana yeye ndiye anayewajibika kusaidia kutatua malalamiko haya. Kwa sasa tungali tumeridhika kwamba hatujapata malalamiko ambayo ni rasmi, “ alisisitiza.  

Hata hivyo, Nkhomee alipoelezwa kuwa wapo watu wake wanaolalamika, alisisitiza kuwa bado hawajamfikisha madai yao na kuwataka wayawasilishe ili hatua ziweze kuchukuliwa.

“Kama nilivyosema awali hakuna malalamiko yaliyotufikia yakiwa rasmi na kwa kuwa tunafanya kazi kiofisi, mtu akituletea malalamiko tutafuata taratibu za kisheria ili aweze kupata haki yake, “alisisitiza mtendaji huyo.

Uchunguzi uliofanywa kwa baadhi ya wapanda pikipiki ulionyesha wanapokutana na gari la polisi linalofanya doria katika sehemu zinazozunguka mgodi huo, hulazimika kupita njia za panya au kwa kasi mahali walipo askari hao.

Oktoba 11, mwaka huu, mwandishi wa habari hii alikodi pikipiki kwa ajili kumpeleka ilipo ‘saiti’ ya kampuni hiyo, ambapo baada ya kufika njia panda ya kwenda mahali ilipo ‘saiti’ ya Shanta Mining, mpanda pikipiki alisimama na kumtaka (mwandishi) aende mwenyewe kwa hofu kuwa angekamatwa.

Mpanda pikipiki huyo alikataa katakata kumpeleka hata pale mwandishi huyo alipomwambia hawezi kukamatwa kwa kuwa mtu aliyempakia angeweza ‘kusaidia’.

Kutokana na hali hiyo, mwandishi alilazimika kutembea umbali wa takribani mita 1,500 hadi lilipo geti la kampuni hiyo, na baada ya kumaliza shughuli iliyompeleka alirejea na kuanza kumsaka mpanda pikipiki huyo kwa njia ya simu, maana alikuwa ameihifadhi pikipiki yake pembeni mwa ukuta wa nyumba iliyoko jirani na sehemu hiyo.

Mara ya pili, Oktoba 22, mwaka huu, mwandishi huyo alikodi pikipiki nyingine T 231 ABG ambayo ilimpeleka mpaka sehemu ya awali, ambapo mpanda pikipiki aligoma kumfikisha mahali yalipo makao ya kampuni hiyo kwa maelezo kuwa angekamatwa na pikipiki yake.

Jitihada za kumshawishi mpanda pikipiki huyo ziligonga mwamba na kuna wakati alimwambia mwandishi kama alikuwa na ajenda ya siri kutaka akamatwe, basi alikuwa tayari kumuacha sehemu hiyo na kuondoka zake.

Akizungumzia suala hilo, ofisa mmoja wa kampuni hiyo, Jeremiah Ndandu,  alisema wapanda pikipiki wengi wanakwepa kupeleka wageni sehemu hiyo kutokana na sababu zao binafsi.

Awali ofisa huyo alimuuliza mwandishi wa habari hizi iwapo alikuwa na usafiri uliompeleka sehemu hiyo, lakini alipoambiwa kuwa alikwenda na pikipiki iliyomshushia njia panda ya kwenda sehemu hiyo, alishangaa.

“Vipi mbona huna usafiri? (alipoelezwa) hawa watu ni waongo, mtu hawezi kukamatwa hapa kama hana kosa. Nakuomba mpigie simu akufuate hapa, aje apaki hata kama ni kwa dakika moja uone kama atakamatwa ili uweze kutoka na ujumbe mzuri,“ alisema ofisa huyo. Hata hivyo kwa kuwa mwandishi hakuwa na namba ya mpanda pikipiki huyo wa pili hakuweza kumpigia.  

Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Singida, Linus Sinzumwa, alisema ofisi yake haijapokea lalamiko kuhusu baadhi ya askari wanaokwenda kulinda mgodi huo kujihusisisha na vitendo visivyofaa, lakini alisisitiza kufuatilia suala hilo ili aujue undani wake.

Alisema huenda lawama hizo zinatolewa na watu wenye makosa ambao hukwepa askari ili wasichukuliwe hatua za kisheria.

“Sioni sababu kama mtu hana kosa amkwepe askari, sioni. Nachoweza kusema mimi nitauliza, nitafuatilia ili nijue, lakini kwa hakika hakuna tatizo kama hilo. Watu wa Sambaru na vijiji vingine najua wanaishi vizuri na askari wetu na wanawapa ushirikiano mzuri sana, “alisema.

Kuhusu askari kulinda mgodi huo sambamba na kampuni binafsi ya ulinzi, Sinzumwa alisema Shanta Mining iliwahi kuvamiwa, kuharibiwa mali zake na kuchomwa moto kwa baadhi ya vitu, suala ambalo liliifanya serikali iimarishe ulinzi sehemu hiyo.

Kamanda huyo alisema ni utaratibu wa kawaida wa Jeshi la Polisi kulinda sehemu zenye uwekezaji mkubwa ili wahalifu wasiharibu shughuli zinazofanyika sehemu hizo.

 “Ndiyo maana hata pale Mang’onyi (kijiji jirani na mgodi) tunajenga kituo cha polisi ili kuwahudumia wananchi, lakini vilevile ili kulinda uwekezaji unaofanyika pale mgodini, “ alisema Sinzumwa.

Jeshi la Polisi linasaidiana na kampuni binafsi ya ulinzi kulinda mgodi na maeneo yanayouzunguka baada ya mgodi huo kuvamiwa na kundi la watu waliodaiwa kuwa wakazi wa vijiji jirani, ambao waliharibu baadhi ya mali na kupora vitu mbalimbali. 

Uvamizi huo ulisababisha serikali iongeze ulinzi ili kuimarisha usalama katika maeneo yote yanayozunguka mgodi huo. Kufuatia uharibifu huo, watu kadhaa walikamatwa na sita miongoni mwao walifunguliwa kesi ya jinai namba 38 ya mwaka 2012 ambayo inaendelea kusikilizwa katika Mahakama ya Wilaya ya Singida.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *