Kuongezeka kwa Majengo katika Shule ya Msingi Endiamtu na changamoto ya matumizi ya vitabu

Belinda Habibu

Majengo matano yamejengwa kwa wakati mmoja, kwa nguvu za wananchi wakishirikiana na serikali ili kutatua tatizo la upungufu wa vyumba vya madarasa katika shule ya msingi ya Endiamtu iIiyoko Mererani.

Mwalimu mkuu wa shule hiyo, Bi Eveta Kyara alisema hayo wakati wa mahojiano maalum na mwandishi wa habari hii ofisini kwake.

Aliongeza kuwa hapo awali walikuwa na madarasa mawili tu na iliwalazimu kuwawekea wanafunzi ratiba ya kusoma kwa zamu kwa makundi.

“Kundi hili wakisomea darasani kundi jingine linasomea chini ya mti,kulikuwa hakuna utulivu si tu kwa wanafunzi bali hata kwa waalimu” alisisitiza mwalimu Kyara.

Pamoja na kuwepo kwa hali hiyo, matokeo ya mtihani wa darasa la nne yaliyopatikana ofisi ya mwalimu mkuu yalionyesha wanafunzi kufanya vizuri kwa kupata alama za daraja  A na B isipokuwa wanafunzi watatu tu walipata daraja C.

Alisema sababu nyingine iliyosababisha wanafunzi kufaulu kwasababu  wanapata chakula shuleni hapo walichofadhiliwa na WFP.

Naye mwenyekiti wa bodi ya shule hiyo bwana Suleiman Mmbaruku amesema kwa ujumla shule sasa imetulia katika hali ya ufundishaji kwani hapo awali wanafunzi walikuwa wanapokezana kuingia madarasani, ambayo yalikuwa mawili na sasa yapo saba baada ya matano kuongezwa kwa mpigo.

Pamoja na hali ya kitaaluma ya kuridhisha hivi sasa, Mwalimu Kyala pia amezungumzia tatizo la mitaala kwa shule ya msingi na hasa ubadilishwaji wa vitabu kwa mfano alisema wengine wanaambiwa watumie kwa upande wa kiingereza wizara inawataka watumie vitabu vya OXFORD na shule zingine wameambiwa watumie vitabu vya taasisi.

“Kinachotushangaza matumizi hayo ya vitabu yanafanyika ndani ya kata moja” alisema mwalimu Kyala.

Ameongeza uwiano kwa sasa kati ya wanafunzi na kitabu ni 1:8 yaani kitabu kimoja kwa wanafunzi wanane ila kwa darasa la kwanza wameboresha lakini kwa kitabu kimoja kwa wanafunzi 4 ili wazoee vitabu.

“Walimu wa hapa tumeamua kutumia vyote kwa kuwa kila kitabu kina umuhimu wake  utakuta huku kuna vitu ambavyo huku havipo lakini vyote ni muhimu na walimu tunatumia zaidi ubao.”anasisitiza mwalimu Kyala.

Akizungumza katika hotuba yake ya mwisho wa mwezi mwaka 2012,raisi wa Tanzania, Mh.Jakaya Mrisho Kikwete alisema uwiano wa kitabu kwa mwanafunzi ni kitabu kimoja kwa wanafunzi watatu kwa shule za msingi na kitabu kimoja kwa wanafunzi 3 kwa shule za sekondari.

Ameongeza kuwa mwaka 2009,uwiano wa kitabu na mwanafunzi ni kitabu kimoja kwa wanafunzi watano  kwa shule za msingi na kitabu kimoja kwa wanafunzi wanne  kwa shule za sekondari.

Shule ya Endiamtu imeanzishwa mwaka 1997 ikiwa na vyumba viwili vya madarasa ila kwa mwaka 2012 ila kwa sasa vipo vyumba saba baada ya kuongezwa na inawanafunzi kuanzia darasa la kwanza hadi la sita wapatao 464.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *