Kipundupindu, rafiki wa Dar es Salaam anayehamia Dodoma

Jamii Africa

PAMOJA na kuendelea kwa harakati za serikali kuhamia rasmi Dodoma, hofu ya kuongezeka kwa kero ya maji katika mji huo ni kubwa.

Hofu hiyo haitapungua, angalau kwa sasa, bali itaongezeka kwa kuwa ni dhahiri kwamba idadi ya watu wa mji huo, Makao Makuu ya Tanzania, inaongezeka, wakati miundombinu ya majitaka haijaongezeka wala kuimarishwa.

Sensa ya mwaka 2012 inaonesha makadirio ya watu waishio Dodoma kuwa ni zaidi ya milioni 2. Wakazi hawa wanakabiliwa na kero kubwa ya maji.

Dar es Salaam, ambayo kwa muda mrefu, kabla na hata baada ya uhuru, imekuwa ikibeba majukumu ya kuwa makao makuu ya nchi yetu, ikiwa na watu zaidi ya milioni 5 kwa sasa, ina kero kubwa ya maji.

Tayari wizara zote za serikali zimehamia Dodoma na Rais John Magufuli, amesema kuwa Ikulu itahamia rasmi huko hivi karibuni.

Kero ni kubwa kupatikana kwa majisafi na uondoaji wa majitaka Dodoma imedumu kwa muda mrefu, huku serikali ikiendelea kutoa ahadi ambazo hazijatekelezwa kuhusu kuwepo kwa uhakika kwa huduma hizo.

Mwezi Mei 8, 2016 wanakijiji wa Nala na vitongoji vyake, walimlazimisha Naibu Waziri wa Bunge, Sera na Vijana, Anthony Mavunde, kunywa maji machafu ishara ya kwamba kijiji hiko hakina huduma ya safi kwa muda mrefu.

Huu ni mfano mmoja wa maeneo mengi ambayo yana shida kubwa ya maji Dodoma.

Idadi ya watu ambao mamlaka ya maji safi na maji taka ya Dodoma uhudumia, bado ni ndogo ukilinganisha na ile ya Dar es Salaam, lakini pia idadi kubwa ni ile ambayo inapatikana mijini yaani Dodoma Mjini, kitendo cha serikali kuhamia huko inamaanisha mji unaweza ukapanuka mpaka sehemu zilizo nje ya mji.

Bado hakuna mipango ambayo inadhihirika kwa mji huo kuwekeza miundombinu ya maji ambayo itachukua muda mrefu kuweza kuhudumia watu wengi na kuepukana na makosa ambayo yamefanyika Dar es Salaam kutokana na watu na ujenzi wa nyumba  kuongezeka, pasipokuwa na utanuzi wa miundombinu ya maji ambayo inaendana na ukuaji wa mji ama ongezeko la watu.

Ongezeko la watu moja kwa moja litasababisha kuongezeko kwa majitaka ambapo Dar-Es-Salaam ni asilimia 10 tu ya miundombinu ya majitaka iliyopo ndiyo inahudumia idadi ndogo ya wakazi wake.

Haifahamiki ni kivipi Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dodoma (Duwasa) inaweza kujipanga kuepukana na kero kubwa ya maji kama ilivyotawala Dar es Salaam.

Endapo uwekezaji wa majitaka utaendelea kupuuziwa kama ilivyo Dar-Es-Salaam, magonjwa ya milipuko kama kipindupindu na homa za matumbo, hayataiacha Dodoma, nayo itakuwa kama sehemu ya magonjwa hayo kama inavyoonekana Dar es Salaam.

Ujenzi holela kwa baadhi ya maeneo jijini Dar es Salaam, usiozingatia ramani za mipango miji, umesababisha maeneo mengi kushindwa kufikiwa na miundombinu ya majitaka, hali ambayo inainyemelea Dodoma.

Mwito kwa Serikali Kuu na Serikali ya Mkoa wa Dodoma kuweka mipango madhubuti ambayo itaufanya Mji wa Dodoma kuwa wa kuvutia, safi, salama na kuepuka makosa ambayo yamefanywa katika Jiji la Dar es Salaam na kusababisha adha kubwa ya upatikanaji wa majisafi na kukwamisha usafirishaji wa majitaka, ambayo matokeo yake ni magonjwa kama kipindupindu.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *