Shinikizo la macho lawatesa watanzania, idadi ya watu wenye upofu nayo yaongezeka

Jamii Africa

Tafiti zinaonyesha Waafrika ni waathirika zaidi wa Ugonjwa wa Shinikizo la Macho (Glaucoma) kuliko watu wengine duniani. Huku watu wenye miaka kuanzia 40 huathirika zaidi na kuwaletea upofu. 

Aidha Serikali imesema kwa bahati mbaya asilimia 70 hadi 90 ya watu wenye ugonjwa huo, hawajijui kwamba wako kwenye hatari ya kupata upofu wasipopata matibabu ya uhakika.

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Faustine Ndugulile alisema hayo jijini Dar es Salaam wakati akizungumzia wiki ya maadhimisho ya utoaji wa elimu kuhusu ugonjwa huo.

Maadhimisho hayo yalianza Machi 11 na yataendelea hadi Machi 17, mwaka huu ambapo yamebeba kauli ya “Okoa uoni wa macho yako”.

Naibu Waziri, Dk. Ndungulile alisema, "Watu millioni 7.7 wana tatizo la kutoona vizuri huku tafiti zikionyesha bara la Afrika likiwa na waathirika zaidi wa Ugonjwa wa Macho na wanaoupata Ugonjwa huo ni watu wa umri wa miaka 40". 

Aliongeza kuwa ugonjwa huo hauna dalili kwa hatua za awali na unaweza kusambaa kwenye familia kwa kurithishana (Kama kuna mwanafamilia ana ugonjwa huu ni rahisi kwa mtu mwingine wa familia hiyo kuupata) na huambatana na tatizo la kutokuona mbali. 

Ugonjwa huo husababisha upofu kwa muda mfupi kutokana na kuanza kujitokeza katika umri mdogo na huwa na msukumo mkubwa ya viwango vya maji ndani ya jicho na  hali huwa mbaya kadiri umri unavyozidi kusogea.

Shinikizo la macho linajulikana kitaalam kama ‘Glaucoma’ na ndio chanzo kinachoongoza kusababisha idadi kubwa ya watu wasioona duniani.


Dk. Ndungulile alibainisha kuwa Tanzania inakadiriwa kuwa na watu milioni 1.7 wenye matatizo ya kutokuona vizuri, kunakosababishwa na matatizo mbalimbali ikiwemo kuwa na mtoto wa jicho, upeo mdogo wa macho kuona na shinikizo la macho.

Katika mwaka 2017,watu 13,240 tu waliohudhuria kwenye vituo vya tiba wakiwa na tatizo la shinikizo la macho, idadi hiyo ni ndogo ikilinganishwa na watu walio katika hatari ya kuwa na ugonjwa huo ambao wapo katika jamii na hawajagunduliwa.

“Ugonjwa huu wa shinikizo la macho ni moja kati ya kundi la magonjwa ya macho yanayoshambulia mshipa wa fahamu unaopeleka mawasiliano ya uoni kwenye ubongo yaani neva optiki ili kuweza kutafsiri kile kinachoonekana,” alisema Ndugulile.


 Glaucoma ni nini?
Hili ni tatizo la ongezeko la shinikizo la macho (eye pressure). Kimsingi macho huwa yana shinikizo  la 10mmhg mpaka 21mmhg lakini inapozidi hapo mgonjwa hutambulika kama mgonjwa wa shinikizo ya macho. Mara nyingi ugonjwa huu hurithiwa na hauonyeshi dalili zozote mpaka baadaye sana mtu anapokuwa mtu mzima. 
 
Ugonjwa huu huathiri mishipa ya fahamu inayohusika na kuona kitaalamu kama 'optic nerve' na mgonjwa asipopata matibabu kwa wakati anaweza kupata upofu wa moja kwa moja na asione tena.

Dalili za ugonjwa huu ni zipi? 

Watu walio kwenye hatari ya kuugua ugonjwa huu?

  • Watu ambao ukoo wao una wagonjwa huo
  • Watu wenye kisukari 
  • Watu wenye umri zaidi ya miaka 40
  • Watu wanaotumia aina fulani dawa ambazo hazipatani na macho 
  • Watu waliopata ajali na kuumia macho 
  • Watu wasioona vizuri 


Watanzania wametakiwa kufuatilia afya zao hususani magonjwa yanayohusu macho angalau mara moja katika mwaka ili kuweza kutambua juu ya mustakabali wa macho yao. 

Nchini Tanzania matibabu yanatolewa katika vituo vyote vya afya nchini kuanzia ngazi ya kanda mpaka ya taifa katika hospitali zote za serikali nchini ikiwemo dawa pamoja na upasuaji ikiwa mgonjwa utawahi mapema.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *