Siku ya Figo Duniani huadhimishwa kila Alhamisi ya pili ya mwezi Machi tangu ilipotambulishwa mwaka 2006. Mwaka huu iliadhimishwa Machi 8 pamoja na Siku ya Wanawake duniani ambapo ilibeba kaulimbiu ya ‘Figo na Wanawake, Tuwashirikishe, Tuwaheshimu na Tuwawezeshe’.
Maadhimisho ya siku ya figo yanafanyika huku uzito ukiwa umewekwa kwa wanawake zaidi kutokana na kudondokea kwenye siku ya wanawake ili kuwaunganisha wadau wa afya kuhakikisha wanawake wanaepushwa na athari za ugonjwa huo.
Ugonjwa wa figo huathiri wanawake milioni 195 duniani kote na kwa sasa ni sababu ya 8 inayosababisha vifo vingi vya wanawake ambapo husababisha vifo karibu 600,000 kila mwaka. Kila mwaka ugonjwa huu huua asilimia 10 ya idadi ya watu duniani kote.
Kimsingi ugonjwa wa figo (Chronic Kidney Disease) ni tatizo kubwa la kiafya duniani na husababisha figo kushindwa kufanya kazi na matokeo yake huleta vifo vya mapema.
Kisukari kimebainika kuwa sababu kubwa ya maradhi ya figo ambapo asilimia 44 ya maradhi mapya ya figo husababishwa na kisukari. Wataalamu wanaeleza kuwa unene uliokithiri ni miongoni mwa sababu kuu inayochangia watu wengi kuugua magonjwa huo.
Hali ikoje Tanzania?
Daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dk. Vincent Tarimo amesema wanawake wanaougua magonjwa ya figo, hukumbwa pia na matatizo ya uzazi, hasa kushindwa kushika mimba na wale wanaobahatika kushika mimba hujifungua kabla ya wakati.
“Magonjwa ya figo kwa wanawake yanaweza kuwekwa katika makundi makubwa mawili, kuna yanayohusiana na ujauzito na yasiyohusiana na ujauzito, ambayo yote huweza kuua,” alisema Dk. Tarimo.
Alisema katika yale yanayohusiana na ujauzito tatizo la shinikizo la juu la damu ndilo huchochea zaidi figo kuathirika na kufa. Ni muhimu mjamzito kuwahi hospitalini au kituo cha afya haraka, hasa anapoona damu inatoka ukeni.
“Tatizo hilo huweza kusababisha mama kutokwa na damu nyingi wakati wa kujifungua au kondo la nyuma kukatika na kuachia kabla ya uchungu wa uzazi kuanza au njia ya uzazi kufunguka", amebainisha Dk. Tarimo na kuongeza kuwa,
“Asilimia 30 hadi 40 ya wagonjwa waliopo wodini hapa Muhimbili idara ya kinamama ni wa saratani ya shingo ya kizazi, saratani hii inapozidi kuenea huenda kuathiri mirija ya mkojo, hushindwa kushuka kwenye kibofu, mkojo unaporudi nyuma huathiri zile figo na kufa".
Naye daktari bingwa wa magonjwa ya figo Muhimbili, Jaqueline Shoo, alisema hata baada ya kusaidiwa kujifungua, wengi hujikuta figo zao zimeumia kwa sehemu kubwa.
“Kila wiki tunapokea angalau mama mmoja katika Idara ya Magonjwa ya Figo ambaye amepata athari kutokana na mambo mbalimbali, ikiwamo tatizo la shinikizo la damu na ajali za mimba,” alisema.
Hatari ya kupata Ugonjwa wa figo ni kubwa zaidi kwa wanawake kuliko ilivyo kwa wanaume. Kwa mujibu wa tafiti mbalimbali ugonjwa wa figo unawakumba zaidi wanawake tofauti na wanaume ambapo hatari kwa wanawake kupata ugonjwa huo ni asilimia 14 ambapo kwa wanaume ni asilimia 12.
Hata hivyo, katika orodha ya matibabu idadi ya wanawake ni ndogo kuliko wanaume na hii inaweza kuelezwa kwa sababu kuu tatu. Kwanza ikiwa ni madhara ya ugonjwa wa figo huchelewa kuonekana ndani ya wanawake tofauti na ilivyo kwa wanaume.
Vikwazo vya kisaikolojia na kijamii kama uwezo mdogo wa kutambua ugonjwa mapema ambao hupelekea wanawake kuchelewa au kutoonekana kabisa kwenye matibabu. Pia ukosefu wa huduma za afya ni sababu nyingine inayozidisha tatizo katika maeneo mbalimbali duniani.
Upandikizwaji wa figo ndio umekuwa njia nzuri ya kutibu ugonjwa huo lakini idadi ya watu wanaojitolea kuwapa figo wagonjwa ni ndogo ambapo kwa mwaka jana pekee wagonjwa 261 wa figo walifariki wakisubiri kupandikiziwa figo.
Inaelezwa kuwa karibu watu nusu milioni wapo katika mpango wa uchujaji damu na mashine mbadala wa figo (dialysis) na huku wakiwa wameshawahi kubadilishiwa figo.
Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) wakishirikiana na wataalamu kutoka hospitali ya BLK ya New Delhi, India kwa mara ya kwanza walifanikiwa kufanya upasuaji wa kihistoria wa upandikizwaji wa figo.
Upasuaji huo ulifanyika Novemba 21, 2017 kwa mwanamke mwenye umri wa miaka 29 ambaye alipatiwa figo na ndugu yake na alikuwa katika hatua ya tano ya ugonjwa huo.
Kinga
Wataalamu wa afya wanashauri kufanya mabadiliko katika milo yetu na mtindo wa maisha kwa ujumla. Chakula chako kisiwe na mafuta mengi, zuia utumiaji kupita kiasi wa chumvi. Pendelea kula matikiti maji au tofaa (apples) na chakula chako kiwe na kiwango kidogo cha protein. Ongeza matumizi ya maji na ikiwezekana yasipunguwe glasi nane kila siku.
Hata hivyo, fanya mazoezi yanayokufaa hili kuweka uzito wako vizuri na kupunguza uwezekano wa kupata kisukari na utapiamlo, zuia matumizi ya pombe na kuacha sigara.