Jumatano ya Machi 21 mwaka huu katika jiji la Kigali, Rwanda lilifanyika tukio la kihistoria la kufufua ndoto na matumaini ya waasisi wa bara la Afrika yenye lengo la kuzileta nchi zote za bara hilo pamoja kwa sauti moja katika shughuli zote za maendeleo.
Tukio hilo la kihistoria lilikuwa ni kusainiwa kwa makubaliano ya uanzishaji wa eneo la huru la kibiashara la Afrika (Africa Continental Free Trade Area) ambalo linalenga kuleta mapinduzi ya kujikwamua kiuchumi na kuziunganisha nchi za bara hilo kuelekea soko la pamoja la bidhaa za kilimo na viwandani.
Makubaliano hayo yamesainiwa na nchi 44 za Afrika ambazo ziliwakilishwa na marais na mawaziri mbalimbali ambapo walikusanyika katika ukumbi wa mikutano wa Kigali kwa siku 2 mfufululizo kupitisha kanuni, maazimio na tamko hilo ambalo lilikuwa likisubiriwa kwa muda mrefu.
Vyanzo vya kuaminika kutoka katika mkutano huo vimeeleza kuwa viongozi waliohudhuria mkutano huo wanaamini kuwa hatua hiyo si kusaini tu makubaliano hayo lakini ni hatua muhimu ya kuthubutu kutekeleza mkakati mpana wa kufikia ile hatua kubwa ya kuifikia ‘’Afrika tuitakayo’’.
Malengo ya makubaliano hayo ni kutengeneza soko la pamoja la bidhaa, huduma na uhuru wa watu kwenda nchi yoyote bila vikwazo ili kuimarisha fungamano la kiuchumi la bara la Afrika. Pia itaenda sambamba na marekebisho ya sheria za kodi, forodha na mipaka ili kurahisisha mzunguko wa bidhaa na huduma kutoka nchi moja kwenda nyingine.
Makubaliano hayo yataendeshwa na chombo au taasisi ambayo itasimamia utekelezaji wa maazimio yote ili kuhakikisha changamoto zinazojitokeza zinatatuliwa kwa wakati. Kuanzishwa kwa eneo la kibiashara la Afrika kutachochea matumizi endelevu ya rasilimali za bara hilo na kukuza uchumi wa nchi moja moja.
Hata hivyo, makubaliano hayo ni mwanzo tu. Yapo mengi yanatakiwa kuwekwa sawa ikiwemo maslahi ya nchi na kanda ambazo zina makubaliano kama hayo. Pia mfumo mzuri wa forodha na kanuni za kusimamia shughuli hizo.
Akizungumza katika mkutano huo Rais wa Rwanda, Paul Kagame ambaye pia ni mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU) alisema kuwa, ufanisi wa makubaliano hayo utategemea zaidi utekelezaji wa mikataba ya umoja wa kanda ambayo imekuwepo kwenye bara hilo kwa miaka mingi sasa.
Kagame ameongeza kuwa kutekelezwa kwa makubaliano hayo kutategemea pia mabadiliko yanayoendelea kufanyika kwenye kanda hizo za kiuchumi barani Afrika ili kuwepo uhuru na wepesi wa kuyetekeleza bila kuingiliwa na maslahi mengine ya nchi moja moja.
Mkakati ni kuinua viwanda vya ndani na biashara miongoni mwa nchi za Afrika
Makubaliano hayo yana maana gani kwa Tanzania?
Makubaliano ya kuanzishwa kwa aneo la huru la kibiashara la Afrika linaweza kuinufaisha na kuididimiza Tanzania kwa namna tofauti. Nitaeleza hapa baadhi ya nadharia ambazo zinafungamana na kututenganisha katika mkataba huo wa Afrika.
Tukianza na manufaa ya kiuchumi na biashara, Tanzania ina nafasi nzuri kwasababu makubaliano hayo yamekuja wakati mwafaka ambapo nchi inatekeleza sera ya viwanda. Tutapata soko kubwa la bidhaa za viwandani ambalo linakaribia watu bilioni 1 katika nchi za Afrika. Soko la pamoja litachochea ukuaji wa kilimo na viwanda na matokeo yake ni kukuza pato la taifa na kuongeza ajira kwa watanzania na kuondokana na umaskini.
Jambo lingine ni kuimarika kwa diplomasia ya Tanzania katika nchi za Afrika. Serikali ya awamu ya tano imejikita zaidi kushirikiana na wanachama wa kanda za Afrika ikiwemo Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) kuliko nchi za magharibi. Hili limejidhihirishwa kwa rais John Magufuli kupunguza safari nje ya bara la Afrika ukilinganisha na mtangulizi wake Jakaya Kikwete ambaye alilalamikiwa safari nyingi.
Nchi nyingi za Afrika hazitofautiani sana kiuchumi na kisiasa. Hiyo ni fursa muhimu kwa Tanzania kujitanua na kujenga uchumi jumuishi na kuongeza mafungamano ya kibiashara yenye tija.
Pia tutakuwa katika nafasi nzuri ya kuvutia wawekezaji wa Afrika wenye ujuzi na teknolojia kuja nchini kuwekeza katika maeneo mbalimbali ya kiuchumi na matumizi endelevu ya rasilimali asilia ikiwemo gesi na madini.
Kwa kutambua hilo serikali imeanza ujenzi wa miradi mikubwa ya miundombinu ya barabara na reli ya kisasa (standard gauge) kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza na kisha kuelekea Rwanda, upanuzi wa bandari ya Dar es Salaam na ujenzi wa bomba la mafuta ghafi kutoka bandari ya Tanga hadi Uganda.
Maandalizi hayo yanafungua milango ya kukua kwa sekta ya kilimo na viwanda itachochea biashara katika nchi za Afrika.
Hata hivyo, kila jambo lina changamoto zake. Makubaliano hayo yanalenga kutengeneza soko la pamoja lenye mifumo inayofanana ya kodi, forodha na biashara; katika mazingira hayo mgongano wa maslahi ya kitaifa na yale ya kujenga Afrika moja hayataepukika.
Wadadisi wa mambo wanasema sera za viwanda za Tanzania zimeegemea zaidi kujenga uchumi wa ndani kwa kuzalisha bidhaa zitakazouzwa nchini. Hili linaweza likakwamisha utekelezaji wa mkataba huo ikizingatiwa kuwa Tanzania imeridhia mikataba mbalimbali ya kimataifa lakini bado haijanufaika. Mfano Mkataba wa AGOA na ule wa Ushirikiano wa Kiuchumi (EPA) na Umoja wa Ulaya (EU). Yote haijaonesha mafanikio yaliyokusudiwa kwa nchi.
Zaidi serikali imejiandaaje kuwawezesha wananchi wake kiujuzi, na teknolojia ili kuzalisha bidhaa zenye ubora zitakazoshindana katika soko la pamoja la Afrika. Pia taasisi na mifumo yetu ina uwezo wa kuhimili ushindani na mabadiliko ya kiuchumi ambayo yataambana na mkataba huo ili kukwepa kuwa soko la bidhaa za wengine.
Tunapoelekea kuijenga Afrika Moja yenye soko la pamoja, tutafakari kama nchi nafasi yetu katika kuimarisha uchumi wa bara hilo lakini pia tutanufaikaje na eneo moja la kibiashara.