Mdororo wa Uchumi? Kampuni kubwa 6 za Kigeni kupunguza Uwekezaji kwa kuelemewa na Mzigo wa Kodi

Jamii Africa

mkendao

Pichani ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Prof. Adofl Mkenda amekaririwa akisema lazima kuwepo na mageuzi mapya ambayo ni magumu, ili kuufanya uchumi kuwa imara.

Takribani makampuni sita makubwa ya kigeni yaliyowekeza hapa nchini yanafikiria kupunguza au kusitisha shughuli zake kwa sababu ya ukubwa na aina mpya za kodi zilizoanzishwa tangu Serikali ya Awamu ya Tani iingie madarakani.

Hii ni kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters lililowahoji baadhi ya wakurugenzi wakuu wa makampuni ya kigeni yaliyowekeza hapa nchini katika sekta ya madini, mawasiliano ya simu na usafirishaji kwa kutumia meli. 

Baadhi ya makampuni yanafikiria kuhamisha shughuli zake katika nchi jirani na baadhi yanafikiria kuondoka kabisa nchini.

Tanzania inategemea zaidi uwekezaji wa kigeni wa moja kwa moja, kuliko nchi nyingine katika Ukanda huu wa Afrika Mashariki, kutokana na ukubwa wa uchumi wake.

Tangu Rais Magufuli aingie madarakani ameanzisha mageuzi ya kiuchumi akiahidi kubadilisha uchumi na kuondoa Urasimu, Rushwa pamoja ili afanikiwe kutekeleza miradi mikubwa ya ujenzi wa Viwanda na Miundombinu.

Aidha, Hali ya Makampuni makubwa kuyumba kifedha pia inashuhudiwa nchini India baada ya hatua ya Waziri Mkuu, Narendra Modi kuwatangazia wananchi kwa kushtukiza Novemba 8 mwaka huu akiwataka watu wanaomiliki noti za rupia 500 mpaka 1,000 kuzirudisha kwenye mabenki kama hatua ya kupambana na Wakwepa Kodi na wale wanaomiliki fedha walizozipata kwa njia ya rushwa.

Hatua hiyo ya India tunaweza kuilinganishwa na agizo la Rais Magufuli la kuyataka Mashirika ya Umma kuondoa fedha zao ilizoziweka katika Mabenki ya Biashara nchini na kuzihamishia Benki Kuu(BoT). Hatua hii imepelekea Mabenki ya Biashara kupata mtikisiko wa kifedha sababu kwa muda mrefu walikuwa wakitegemea fedha hizo kujiendesha. Ikumbukwe, pia Rais Magufuli aliwahi kutishia kuzibadili noti endapo watu wataendelea kuzificha pesa.

Nchini India, agizo la ghafla la kurudisha kwenye mabenki fedha zilizokuwa mzunguko na kupewa noti mpya limepelekea mabenki kuyumba sababu yalikuwa hayajajiandaa na zoezi la kuchapisha noti mpya hivyo imepelekea fedha kupungua kwenye mzunguko kama inavyoashiria kutokea hapa nchini Tanzania.

Baadhi ya Makampuni na viwanda tangu kutangazwa kwa zoezi hilo yanashindwa kujiendesha sababu ya uhaba wa fedha kwenye mzunguko.

Mfano, nchini India malori 400,000 yamepaki sababu wamiliki wamekosa fedha za kuwapa madereva wanapokuwa safarini kwa ajili ya kununulia mafuta na mambo mengine.

Pia Viwanda vya miwa vimeshindwa kuwalipa wafanyakazi wake mishahara sababu ya ukosefu wa fedha. Lakini Serikali inasema hali hiyo ni ya mpito na zoezi hilo litakamilika ndani ya siku 21. Wataalamu wa Uchumi wanadai kuwa madhara ya agizo hilo la Waziri Mkuu kwenye uchumi yataendelea hata kwa zaidi ya miezi sita.

Mwaka huu Serikali imeongeza kodi katika utumaji wa fedha kwa kutumia Simu za Mkononi, Mabenki, Sekta ya utalii na usafirishaji wa mizigo. Kodi ya mapato kwa mwaka wa fedha 2014/2015, jumla ilikuwa Shilingi za Tanzania trillioni 9.8 ambazo ni sawa na Dola bilioni 4.5. Kwa mwaka wa fedha 2016/2017, serikali ina lengo la kukusanya kodi ya mapato zaidi ya trilioni 15.1, ikiwa ni ongezeko la zaidi ya asilimia 50.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Adolf Mkenda, amesema wameyasikia malalamiko yanayotolewa na milango iko wazi, lakini wanahakikisha kuwa kila mtu analipa kodi anayopaswa kulipa kwa kuzingatia haki. Amesema lazima kuwepo na mageuzi mapya ambayo ni magumu, ili kuufanya uchumi kuwa imara.

Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania-TRA, Richard Kayombo amesema ongezeko la kodi ya mapato lilihitajika kwa ajili ya kulipia miundombinu mipya nchini. Makampuni makubwa ya kigeni ambayo yamewekeza nchini Tanzania ni pamoja na yale ya Nishati, Uhandisi, Mawasiliano ya simu, Madini, na Usafirishaji kwa kutumia meli.
 

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *