Kugundua kwamba una saratani au ndugu yako ana saratani huwa ni kipindi kigumu sana maishani. Saratani imekuwa janga kubwa sana duniani na hujitokeza katika namna tofauti.
Saratani husababisha vifo vya watu zaidi ya milioni 8 kila mwaka. Na maradhi mapya milioni 15 hugundulika kila mwaka. Tafiti nyingi zimejitahidi kuboresha tiba pamoja na kutoa elimu kuhusu ugonjwa huu, lakini bado vita dhidi ya saratani ni ya kudumu na inayogharimu muda.
Saratani au kansa maarufu sana duniani ni; kansa ya matiti, mapafu, tezi dume, kansa ya kongosho, kansa ya koo lakini katika zote hizo kuna kiungo kimoja cha binadamu ambacho hakipo kwenye orodha nacho ni “Moyo”.
Je, umewahi kukutana na mtu mwenye saratani ya moyo? Ni kweli kwamba bado hujakutana naye. Je, hakuna saratani ya moyo?
Ukweli ni kwamba saratani ya moyo ipo, lakini matokeo yake ni machache sana na sababu za kuwa hivyo zaweza kukushangaza.
Ukweli kuhusu saratani au kansa
Watu wengi wanaposikia neno kansa hushtuka na kutamani hali hiyo isiwapate wao. Lakini ni vizuri sana kufahamu kuhusu ugonjwa wenyewe, na kujua kwa undani kuhusu mfumo wake kwenye mwili wa mwanadamu.
Kimfumo mwili una uthibiti wa kinga zake katika kuziweka sawa, kuondoa zilizochoka na kuzalisha mpya zenye afya. Lakini katika baadhi ya mazingira jambo hili huwa halifanyiki na seli huzidi kuzalishwa na kuongezeka na matokeo yake hutengeneza seli nyingi zisizoweza kufanya kazi.
Seli hizi zisipodhibitiwa, zinavuruga utendaji kazi wa seli zingine, kuchochea uzalishaji zaidi na baadaye kudhuru mfumo mzima wa ogani za mwili.
Saratani inaweza kusababishwa na kazi asilia za mwili, ni matokeo hatari yanayosababishwa na seli za mwili ambazo huchochea ongezeko la seli mwilini, na baadaye kuzifanya kuwa hatari au zifanye kazi tofauti na ile zinazotakiwa kufanya.
Seli hizo nyingi zilizozalishwa zinaposhindwa kudhibitiwa, husababisha kutokea kwa mkusanyiko mkubwa wa seli ambao hujulikana kama uvimbe (lakini hii haitokei kwenye saratani zote, mfano kansa ya damu).
Kuna aina 5 za saratani na zimegawanywa kutokana na sehemu ya mwili kansa inapotokea;
1. Kansa za mifupa
2. Kansa ya seli
3. kansa ya ngozi
4. Kansa ya damu
5. Kansa za mfumo wa fahamu
Japokuwa kansa imezoeleka kutokea kwenye baadhi ya viungo vya mwili kwa kiwango kikubwa lakini ukweli ni kwamba kansa inaweza kujitokeza sehemu yoyote ya mwili; utofauti ni kwamba ni rahisi kwa kansa kujitokeza zaidi kwenye baadhi ya sehemu za mwili.
Pamoja na kuwa kansa husambaa kutokana na mkusanyiko wa seli nyingi ulioshindwa kudhibitiwa na mwili, lakini ogani ya mwili yenye mfumo wa kuzalisha na kuondoa seli ina nafasi kubwa sana ya kupata kansa tofauti na ogani isiyo na mfumo huo au yenye kiwango kidogo cha kuzalisha seli. Kwa dhana hiyo sasa tuufikirie moyo…
Ogani yenye kazi kubwa
Linapokuja suala ya ogani zinazofanya kazi nyingi mwilini sio rahisi kuusahau moyo, ambao huanza kufanya kazi kabla hata hatujazaliwa na huendelea kufanya hivyo mpaka pale tunapokufa. Huwa hakuna mapumziko kwenye mioyo yetu, maana hutakiwa kudunda muda wote. Kutoa na kusukuma damu kwenye mishipa na mirija yote mwilini kuhakikisha kila kiungo kinafanya kazi vizuri.
Kwa utendaji huo usio na mapumziko mwaka mzima, moyo huwa hauna muda wa kuondoa seli za zamani kwa kuzalisha seli mpya. Hakuna muda wa kazi hiyo, hivyo seli za moyo mara nyingi huwa hazibadiliki labda pale panapokuwa na tatizo kwenye seli hizo ambazo zinahitaji marekebisho.
Kama tulivyosema mwanzo kansa hutokea na kusambaa kupitia mkusanyiko wa seli za mwili; hivyo kwa ogani ambazo hazizalishi seli mara kwa mara ni ngumu kwa kansa kupata nafasi ya kutokea.
Kwa sehemu zingine za mwili kama ngozi, matiti, tumbo na utumbo zenyewe mara nyingi huondoa seli za zamani kwa kuzalisha seli mpya. Umeng’enyaji wa chakula huwa ni mchakato mgumu wenye tindikali nyingi (acid). Pia fikiria ni mara ngapi umeondoa ngozi kavu kwenye viganja au mikono yako?. Hata seli za matiti husinyaa na kutanuka kutokana na utendaji kazi wa homoni mwilini.
Aina hizi za saratani (ngozi, matiti, utumbo n.k) ni maarufu kwasababu seli za maeneo hayo huzalishwa na kuondolewa mara kwa mara. Pia maeneo haya hukutana na vihatarishi vingi ikiwemo mionzi ambayo hukutana na ngozi. Pia visababishi vingine vya kansa ambavyo huwa tunaviingiza mwilini au kuvivuta kupitia mfumo wa upumuaji (mapafu).
Ni mara chache sana moyo kukumbana na mazingira kama haya na hii husababisha utokeaji wa kansa uwe mgumu kwenye kiungo hicho. Hivyo ni ngumu sana kwa moyo kupata kansa. Hata hivyo kwanini inatokea?
Utokeaji wa kansa
Kwa makadirio tafiti zinaonesha watu 34 kati ya 1,000,000 wana mfumo wa kansa ya moyo, ambayo imegawanywa katika makundi mawili: uvimbe mdogo na mkubwa wa moyo.
Uvimbe wa ‘Malignant’ ambao hujulikana kama uvimbe mdogo, ni kansa ambayo hujitokeza kwenye mishipa milaini ndani ya mwili wa mwanadamu. Matukio ya aina hii ya kansa ni machache sana, lakini kiwango cha uongezekaji wake ni kikubwa sana. Viuvimbe laini kutokea kwenye moyo huwa ni jambo la kawaida, na mara nyingi haviwezi kusababisha kifo kwa mtu mwenye navyo.
Njia kubwa ya kutokeza kwa kansa kwenye moyo ni kupitia uvimbe mkubwa kwenye kiungo hicho. Hii hutokea zaidi pale kansa inaposambaa kwenda kwenye moyo kutokea sehemu nyingine ya mwili.
Kansa inapokuwa, husambaa kwenda kwenye sehemu zingine za mwili kutokea kwenye sehemu ya msingi au chanzo ilipoanzia. Kwenye baadhi ya matukio ya kansa ya mapafu inaweza kusambaa kwenda kwenye moyo, hii ni kutokana na ukaribu wa viungo.Lakini pia kansa inaweza kusambazwa kwenda kwenye moyo kupitia mfumo wa damu.
Kansa ya figo, mapafu na matiti, pamoja na kansa ya damu, kansa ya ngozi na tezi (goita) mara nyingi husambaa na kuathiri moyo, kutokana na ukaribu wa viungo hivyo.
Japokuwa kansa ya moyo haipo kwa kiwango kikubwa lakini kiwango cha kupona ni asilimia 50 baada ya mwaka mmoja, sio jambo la kupuuzwa. Pale watu wanaposema kwamba hakuna kansa ya moyo kwasababu tu hawajawahi kukutana na mgonjwa wa kansa hiyo ni vizuri ukampatia maarifa haya mapya.