Sakata la dawa za kulevya Dar es Salaam lazima mjadala wa kufeli wanafunzi

Jamii Africa

MJADALA mkali ulioshika kasi kwenye vyombo vya habari  na mitandaoni,  kuhusu Mkoa wa Dar es salaam kushika mkia kwenye matokeo ya kidato cha nne kitaifa yaliyotangazwa Januari 31 mwaka huu, sasa umeyeyuka.

Sababu kubwa za kuyeyuka kwa mjadala wa elimu na matokeo hayo kuibuka kwa mjadala mwingine ulioanzishwa Februari 2, baada ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, kutaja majina ya watu wanaodaiwa kuuza au kutumia dawa za kulevya.

Katika shule 10 za mwisho kitaifa, Dar es Salaam iliingiza shule sita ambazo ni Kitonga, Nyeburu, Mbopo, Mbondole, Somangila Day na Kidete.

Kabla ya majina ya  watuhumiwa wa dawa za kulevya kutajwa, mjadala mkuu  katika vyombo vya habari ulikuwa kuhusu matokeo ya kidato cha nne na jinsi mkoa huu ulivyoshika mkia.

Mjadala huo ulishika kasi kupitia vyombo vya habari hususani mitandaoni hadi kupelekea tarifa kuwa kuna waalimu wameshushwa vyeo jambo ambalo lilidaiwa na Chama cha Waalimu kuwa kinyume cha sheria.

KUVULIWA VYEO WALIMU KWAYEYUKA

FikraPevu imelazimika kufika  kwenye ofisi ya Katibu wa Chama cha Waalimu, Mkoa wa Dar es Salaam, Abdallah Mkaula kwanza kufahamu jinsi mjadala huo ulivyofutwa na pili kufahamu hatua zilizochukuliwa dhidi ya Walimu ambao Watanzania walitangaziwa kuwa wameshushwa vyeo.

“Tumekaa na walimu, tumejadili hadi leo sisi hatujaona barua yeyote ambayo mwalimu ameandikiwa kushushwa cheo, ingawa mjadala wa hali ya elimu ulipaswa kuendelea.” anasema Mkaula.

KILICHOTOKEA BAADAYA MATOKEO

Februari 1 mwaka huu Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni Hashimu Mgandilwa aliagiza kuwa wakuu wa shule Kidete na Somangira wavuliwe madaraka baada ya shule zao kushika mkia katika matokeo ya kidato cha nne.

Alitoa tamko hilo kufuatia shule sita za Dar es Salaam kuwa miongoni mwa shule kumi za mwisho katika matokeo ya kidato cha nne  na shule mbili zipo katika wilaya ya Kigamboni ambazo ni Kidete na Somangira

HAKIELIMU YATOA USHAURI

FikraPevu pia imelazimika kufika kwa  Meneja wa Idara ya Utafiti, Uchambuzi na Sera kutoka HakiElimu, Bonaventura Godfrey kujua athari za mjadala wa elimu ya Dar es Salaam kufunikwa na sakata la dawa za kulevya  kwanza anasema si sawa mjadala ulivyochwa.

Mtafiti huyo wa masuala ya elimu anazungumza kwamba  “mustakabali wa elimu yetu unahitaji mjadala mpana na hii ndio ilipaswa kufanyika ili kujadili kwa nini Dar es Salaam shule nyingi zimeshika mkia kati ya 10 za mwisho.”

 “Tutakapojadili ndio tutathubutu kufanya tafiti na kubaini chanzo cha matatizo. Ufaulu wa asilimia 70 bado sio mzuri kwani asilimia 30 wamepata sifuri, lakini pia ufaulu wa daraja  I-III, bado ni robo ya watahiniwa na wanaobaki hawana tena uelekeo. Sasa hii ni shida na tunahitaji tujadili falsafa ya elimu yetu ni nini,anahoji mtafiti huyo wa HakiElimu, taasisi inayohusika zaidi na utafiti wa masuala ya elimu nchini.

Pia anasema tuweke malengo ya kutupeleka kwenye falsafa yakiwa na kanuni, miongozo na sheria. Hivyo tunapokuwa na tatizo kama hili lazima turudi mezani kutafuta tatizo na ufumbuzi na sio mihemko ya kushusha walimu vyeo au kuwawajibisha ilihali hakuna utafiti ulioonyesha kama mwalimu mkuu ndio tatizo.

Siri kubwa ni tuwe na mazingira bora ya kufundishia na kujifunzia na kila mtu awajibike kuanzia mwanafunzi, mwalimu, mzazi na hadi serikali.

 

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *