Kusafiri ndani ya treni (garimoshi) kuna upekee wake. Unashuhudia mandhari nzuri ya uoto wa asili, uwanda mpana wa ardhi usio na mwisho, miji mbalimbali yenye kila aina ya watu. Kitu kingine utakachokiona mara nyingi wakati ukitumia usafiri wa treni ni mawe madogo madogo (kokoto) kuzunguka reli ambapo treni inapita.
Lakini umewahi kujiuliza kwanini katika maeneo yote inakopita reli kuna kokoto au mawe madogo ya aina yake?
Kwanini mawe relini?
Tuanze kwa kujadili mawe madogo madogo ambayo unayoyaona karibu au yanayozunguka njia ya reli, ambayo kwa pamoja yanaitwa ‘track ballast’ (mawe ya relini). Kimsingi mawe hayo huzunguka vipande vinavyojulikana kama ‘railway sleepers’ na ni mfano wa chaga za kitanda ambazo hushikilia godoro lisianguke na kwenye reli ni hivyo hivyo ambapo hushikilia vyuma vya reli visiyumbe wala kutoka pale vilipo na kuhakikisha treni haitoki nje ya mstari uliowekwa na wataalamu.
Vipande hivyo ‘Railway sleeper’ vina umbo la pembe nne ambavyo kawaida huwekwa sambamba na njia ya reli. Kwa jina lingine hujulikana kama ‘railroad tie au crosstie’. Kwa kawaida vipande hivi hutengenezwa kwa mbao au zege, ambavyo hutumika zaidi nyakati hizi. Kazi ya vipande hivyo ni kushikilia reli isiyumbe na iwe kwenye muelekeo sahihi.
Railway Sleepers
Kwanini ni mawe ya aina hiyo tu?
Sio mawe ya aina zote ambayo wajenzi wanayatumia kwenye ujenzi wa barabara ambayo yanaweza kuwekwa kwenye reli. Ingekuwa hivyo basi reli isingefanya kazi. Kwa mfano, ukiweka mawe laini na ya mviringo kwenye barabara ya reli, halafu ukaruhusu treni ipite; mawe hayo yatatawanyika kwasababu yatashindwa kufanya kazi inayotakiwa ya kuimarisha uthabiti wa reli.
Kwa kutambua hilo, unahitaji mawe ya aina yake ambayo hayatasambaa sana, labda kama watoto au wanyama watayatoa yalipo.
Kuhakikisha mawe yanakaa yalipowekwa bila kutawanyika, wanatumia mawe yaliyochongoka na magumu yenye ukubwa kiasi. Ninaeleweka?
Hiyo ndio kazi pekee ya mawe ya relini?
Ni kweli kwamba mawe ya relini yanafanya kazi nyingi. Kwanza kabisa, yanasaidia reli kukaa mahali pake wakati treni yenye uzito mkubwa ikiwa inapita. Pia inazuia aina yoyote ya majani yasiote karibu na reli ambayo yanaweza kuufanya udongo uliopo chini ya reli kuwa dhaifu na kushindwa kuhimili uzito wa reli na treni.
Kazi nyingine muhimu inayofanywa na mawe ya relini ni kuzuia maji yasikusanyike au kukaa muda mrefu kwenye reli na kudhoofisha njia ya reli. Hiyo haimaanishi kuwa mawe hayo yanaingika njia ya reli dhidi ya maji kwa asilimia 100, la hasha! Haiwezekani lakini inawezesha mifereji ya maji chini na kuzunguka kwenye njia ili maji hayo yasikae muda mrefu na kudhoofisha uthabiti wa reli.
Njia rahisi ya kuzuia mtikisiko
Pamoja na kuwepo kwa mawe hayo bado treni hutoa sauti na mtikisiko mkubwa ambao unaweza kuleta usumbufu kwa watu waliopo ndani ya treni na wale wanaoishi karibu na reli.
Matumizi yaliyopitiliza ya usafiri wa reli yanaweza kuwa hatari kwa majengo ambayo yako karibu na njia ya reli kwasababu ya mitikisiko mikubwa inayotengenezwa wakati treni inapita kwenye reli.
Pia sauti kali husikika wakati treni inapita kwa kasi kwenye reli ambapo ni usumbufu kwa watu wanaoishi karibu na maeneo hayo.
Ili kupunguza mitikisiko hiyo, kuna njia rahisi ya kushikilia vyuma ambayo hufyonza mtikisiko na kupunguza sauti ya msigano wa vyuma. Inahusisha mpira aina ya EPDM (Ethylene Propylene Diene Monomer) kwasababu una uwezo mkubwa wa kuzuia joto, maji na kasoro nyingine ya kiufundi.
Matokeo yake, mitikisiko na kelele hupungua kwa kiasi kikubwa na kuwafanya watu waliopo ndani ya treni kufurahia usafiri huo.
Tunachojaribu kusema ili tueleweke… ni kwamba kutoa mawe yaliwekwa kwenye reli sio jambo zuri kwasababu yamewekwa kwasababu maalumu ya kuimarisha reli na kuwalinda watu wanaotumia usafiri wa treni.