WILAYA ya Kwimba mkoani Mwanza ni kati ya maeneo yaliyovuma kwa kilimo cha zao la pamba kabla na baada ya Uhuru.
Hata hivyo, zao hilo limepoteza mvuto miongoni mwa wakulima wilayani humo kiasi cha uzalishaji kushuka hadi kufikia tani 2,150 pekee msimu wa 2015/2016.
Uchunguzi wa FikraPevu umebeini kwamba, wilaya hiyo yenye jumla ya hekta 125, 332 zinazofaa kwa kilimo cha pamba ina uwezo wa kuzalisha zaidi ya tani 100, 000 iwapo eneo lote litalimwa kwa tija.
“Kwimba tumedhamiria na kumejipanga kufufua kilimo cha zao la pamba kwa sababu ardhi tunayo, nia tunayo na nguvu kazi pia tunayo,” ni kauli ya Mkuu wa Wilaya hiyo, Mtemi Msafiri
Wilaya imeunda Kamati Maalum ya kufufua zao la pamba kuanzia ngazi ya vijiji, kata hadi wilaya ambayo pia hushirikisha wajumbe kutoka Bodi ya Pamba nchini (TCB), Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama, Wakuu wa Idara, Maofisa Kilimo pamoja na Wakulima.
Akizungumza na FikraPevu wakati wa mahojiano maalum ofisini kwake mjini Ngudu yaliko makoa makuu ya wilaya hiyo, Msafiri anasema kwa kuanzia, wilaya imejiwekea malengo ya kuzidisha mara kumi uzalishaji wa msimu uliopita wa tani 2,150 hadi kufikia tani 25,000 kwa msimu huu.
“Kuna kaya zaidi ya 74,000 kwa wilaya nzima. Tumejiwekea malengo ya kila kaya kulima ekari moja ya zao la pamba na hii itatuhakikishia kulima ekari 74,000 hivyo kutupa malengo ya tani 37, 000,” anasema Msafiri.
Akifafanua, anasema kutokana na kaya 74,000, wilaya hiyo imejiwekea malengo ya kupata mavuno mazuri kwenye kaya 50,000 ambazo zitatoa tani zaidi ya 25,000 ya pamba.
Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa Wilaya, iwapo lengo hilo litafanikiwa, Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba itajihakikishia ongezeko la Shs. 870 milioni katika mapato ya ndani kutokana na ushuru wa pamba kulinganisha na Shs. 87 milioni za msimu uliopita.
“Tayari tumegawa tani zaidi 160 za mbegu kwa wakulima ambao wameonyesha hamasa ya kurejea kwenye kilimo cha pamba,” anasema mkuu huyo wa wilaya.
Katika mkakati huo, wajumbe 32 wa Kamati ya Ulinzi na Usalama na Wakuu wa Idara 44 wa Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba kila mmoja amelima ekari moja ya pamba na hivyo kufanya jumla ya ekari 76 katika Kijiji cha Kilyaboya inayotumika kama shamba darasa kwa wakulima wa Kata ya Ngudu.
Msafiri anasema mpango wa kufufua kilimo cha pamba wilayani humo pia unahusisha shule zote 156 za msingi kulima ekari moja ya zao hilo inayotumika kama shamba darasa kwa wakulima.
“Wanafunzi ndio wakulima wa baadaye. Hivyo ni vema kuwaandaa mapema kwa kuwapa elimu ya kilimo chenye tija kupitia shamba la shule ambalo ndilo pia hutumika kama shamba darasa kwa wananchi wa eneo husika,” anaeleza Msafiri.
Uzalishaji wa pamba washuka Mwanza 2008 hadi 2017
Takwimu zinaonyesha kwamba uzalishaji mkoani Mwanza umeshuka kutoka zaidi ya tani 370,000 msimu wa 2008/2009 hadi zaidi ya tani 150,000 pekee kwa msimu uliopita kama inavyonekana kwenye jedwali la uzalisha kwa kipindi hicho.
Kwa Mkurugenzi Mkuu wa TCB, Marco Mtunga, anasema miongoni mwa changamoto zinazoikabili sekta ya kilimo cha pamba ni huduma duni ya ugani, wakulima kutozingatia kanuni ya kupanda kwa nafasi, pamba kuchanganywa na mazao mengine na wadudu kutokana na ama wakulima kutopulizia dawa kwa wakati au viuadudu kukosa ubora.
Mapato nayo yashuka kwa kasi
Kama ilivyo kwenye uzalishaji, mapato yatokanayo na zao la pamba kwa msimu uliopita pia yameshuka kwa zaidi ya nusu kulinganisha na msimu wa mwaka 2010/2011.
Wakati msimu wa 2015/2016 Mkoa wa Mwanza uliingiza zaidi ya Shs. 12.9 bilioni (Dola za Kimarekani 5.9 milioni), msimu wa 2010/2011 zao hilo liliingizia mkoa zaidi ya Shs. 29.2 bilioni (zaidi ya Dola za Kimarekani 13.3 milioni).
Pamoja na Mwanza, mikoa mengine inayozalisha pamba ni pamoja na Geita, Simiyu, Shinyanga, Tabora, Mara, Kagera, Kigoma na Singida.
Huduma ya Ugani na udhibiti wa Maofisa Ugani
“Licha ya mazingira magumu kiutendaji yaliyokuwa yakiwakabili kipindi cha nyuma, baadhi ya maofisa ugani walijisahau na kugeuka kuwa wananchi wa kawaida katika maeneo yao kwa kujiingiza kwenye kilimo na biashara badala ya kuwashauri wakulima,” anabainisha Msafiri.
Ili kudhibiti hali hiyo na kusimamia uwajibikaji, umeanzishwa utaratibu wa kila Ofisa Ugani kuwa na daftari maalum la kumbukumbu (log book), inayoonyesha jumla ya wakulima katika eneo lake, aliowatembelea, muda na aina ya mazao wanayolima.
Mbegu na pembejeo kwa wakulima
“Kwa kushirikiana na Kituo cha Utafiti wa Kilimo Ukiriguru kilichopo Wilaya ya Misugwi, Bodi ya Pamba pamoja na makampuni ya kusambaza pembejeo tunahakikisha wakulima wanapata mbegu bora na zenye tija,” anasema Msafiri.
Anataja mbegu aina ya UK M08 isiyo na manyoya kuwa ndiyo inayofaa kulinganisha na ile ya UK 91 yenye manyoya anayosema imepitwa na wakati na hivyo kupunguza tija.
Kwa mujibu wa Mkaguzi wa Pamba Wilaya ya Kwimba kutoka TCB, Penina Range, mbegu ya UK M08 ikilimwa kwa tija hutoa kati ya tani 800 hadi 1,200 kwa kila ekari moja ya shamba la pamba.
Kilimo cha Skimu ya Umwagiliaji
Kutokana na Wilaya ya Kwimba kuwa miongoni mwa maeneo kame, uongozi wa wilaya hiyo unaelekeza nguvu kubwa kwenye kilimo cha umwagiliaji.
“Tunatarajia kutenga bajeti ya kufufua skimu za umwagiliaji za Shilanona na Kimiza ambazo hazifanyi kazi kwa sasa,” anasema Mkuu wa Wilaya.
Katika mpango huo, wilaya pia inakusudia kujenga mabwawa na mifereji ya umwagiliaji itakayotumika kwa kilimo cha umwagiliaji kwa kipindi chote cha mwaka badala ya kutegemea mvua.
Hivi sasa, skimu ya umwagiliaji ya Maliga pekee ndiyo inayofanya kazi wilayani humo.
Sababu zilizozorotesha kilimo cha pamba
Pamoja na kuelezea mikakati ya kufufua kilimo cha pamba, Mkaguzi wa TCB anataja baadhi ya sababu alizosema zilizorotesha kilimo cha zao hilo, siyo tu Wilaya ya Kwimba, bali nchini nzima, kuwa ni pamoja na usimamizi hafifu na kukosekana kwa huduma ya ugani.
Range anasema kama ilivyo kwenye sekta zingine, kilimo cha pamba kilikosa usimamizi imara kutoka kwa wadau kuanzia Serikali Kuu, Halmashauri, Maofisa Kilimo na Ugani na wakulima wenyewe.
Licha ya uchache wao kulinganisha na mahitaji halisi, Maofisa Ugani pia hawakufika kwa wakulima ama kwa kutotimiza wajibu au kukosa vitendea kazi, ikiwemo usafiri.
“Wakulima walikatishwa tamaa kwa kusambaziwa mbegu zisizoota na hivyo kuwatia hasara kwa kupanda zaidi ya mara moja na kutopata tija,” anasema Range.
Anasema hata pale mbegu zilipoota, viuadudu vilivyosambazwa kwa wakulima pia havikutoa tija na hivyo kupunguza uzalishaji na kuzidisha hasara kwa wakulima.
Mkaguzi huyo wa pamba anasema baadhi ya makampuni yaliyoingia mikataba ya kusambaza pembejeo kwa wakulima hayakutimiza wajibu na mahitaja ya mikataba yao.
Vile vile, mvua chache na zenye mtawanyiko usiotabirika pamoja na ukame katika baadhi ya maeneo yanayostahili kwa kilimo cha pamba, pia ni miongoni mwa sababu zilizozorotesha kilimo cha zao hilo.
FikraPevu imeelezwa kwamba, kufa au kuyumba kiutendaji kwa baadhi ya viwanda vya kuchambua pamba pamoja na kutengeneza nguo ni sababu kuu ya kuzorota kwa kilimo cha zao hilo.
Kwa mujibu wa Range, kuyumba kwa viwanda hivyo siyo tu kulipunguza bei ya pamba, bali pia kuliwakatisha tamaa wakulima kutokana na bei ndogo kulinganisha na gharama na muda wa kilimo.
TCB na mikakati ya kusaidia wakulima
Range anasema, Bodi ya Pamba Tanzania (TCB) kupitia makampuni ya kuchambua pamba imefanikisha upatikanaji wa pembejeo za kilimo.
“Chini ya uratibu na simamizi wa TCB, halmashauri na uongozi wa wilaya, makampuni haya yanatoa mbegu na viuadudu kwa wakulima kulingana na mahitaji na mikataba,” anasema Range.
Katika mkakati huo, makampuni hayo, ICK Cotton, SM Holding na African Ginneries pia zimetoa pikipiki kwa Maofisa Ugani kuwawezesha kuwafikia wakulima kwa ushauri.
Kwa mujibu wa mkaguzi huyo, licha ya kusambaza mbegu na viuadudu, makampuni hayo pia hulazimika kuwalipa fidia wakulima iwapo mbegu na viuadudu walivyosambaza havitaleta tija.
Halmashauri ya wilaya ambayo ndiyo huingia mkataba kwa niaba ya wakulima inalazimika kulipa asilimia 50 ya ushuru iwapo wakulima watashindwa kutekeleza wajibu.
Ubora wa pamba
Pamoja na kuhimiza na kufufua kilimo cha pamba, TCB pia imeelekeza nguvu katika usimamizi wa ubora.
Kwa mujibu wa Range, usimamizi wa ubora huanzia kwenye utoaji wa elimu na mafunzo mbalimbali kupitia semina kwa wakulima na makarani wa ununuzi kuanzia ngazi ya vijiji, wilaya na watendaji wa makampuni ya kuchambua pamba.