Jukumu la kumlea na kumtunza mtoto ni la wazazi wote wawili yaani baba na mama. Matunzo hayo yanaanza mama anapokuwa mjamzito mpaka siku ya kujifungua.
Katika siku za mwanzo za kuzaliwa mtoto, inashauriwa wawazi wote wawili kuwa karibu na mtoto ili kujenga msingi mahusiano mazuri ya upendo kwa kichanga. Ili jambo hilo lifanikiwe wazazi watalazimika kuacha majukumu mengine na kutumia muda mwingi kukaa na mtoto.
Dhana hiyo imeleta mjadala na mitazamo tofauti katika jamii hasa kwa wanaume ambao ni wafanyakazi wa kuajiriwa kwamba wanapaswa kuacha majukumu yao kwa muda na kuungana na mtoto. Hapo ndipo linakuja suala la kupata likizo ya uzazi kwa wanaume (paternity leave).
Kulingana na Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini ya mwaka 2004 ya Tanzania inatoa likizo ya siku tatu kwa mwanaume na miezi mitatu kwa mwanamke kwa ajili ya uzazi hasa mtoto akizaliwa.
Licha ya sheria mbalimbali duniani kutoa mwongozo wa likizo ya uzazi kwa wanaume bado kumekuwepo na mkanganyiko wa mawazo kuhusu dhana hiyo.
Wabunge nchini Nigeria wamekataa kupitisha muswada wa likizo ya hiari ya uzazi kwa wafanyakazi wa sekta ya umma na binafsi. Mswada huo ulioshindwa kusomwa kwa mara ya pili bungeni hivi karibuni.
Ili muswada uwe sheria nchini Nigeria, unatakiwa usomwe mara ya kwanza na ya pili, kisha utapitiwa na kamati ya Bunge na kusomwa tena kwa mara ya tatu kabla rais hajatia saini.
Kukataliwa kwa muswada huo kulitokana na sababu za asili na kitamaduni. Wakazi wengi wa Nigeria wanajihusisha na ndoa za wake wengi. Baadhi ya wabunge waliopinga muswada huo wanaamini kuwa mwanaume mwenye wake wengi atalazimika kuchukua likizo nyingi kwa mwaka ili kuwahudumia wake zake wakati wamejifungua.
Siyo mara ya kwanza kwa wabunge hao kuzuia miswada inayozingatia usawa wa kijinsia. Machi 2016, walizuia pia muswada ambao ulidhamiria kuondoa ubaguzi wa kijinsia kwenye siasa, elimu na ajira.
Mtazamo wa wabunge wa Nigeria hautofautiani sana na raia wa Marekani ambao wanaona mwanaume hapaswi kupewa kabisa likizo ya uzazi na wengine wanaenda mbali zaidi na kutaka hata mwanamke asipate kabisa likizo hiyo.
Kulingana na utafiti uliofanywa na taasisi ya Pew mwaka 2017 ulibaini kuwa mtu 1 kati ya 7 (asilimia 15) wa Marekani alisema akina baba wasipewe likizo ya uzazi kabisa. Na asilimia 3 ya raia wa Marekani wanafikiri kuwa hata mama aliyejifungua hapaswi kupewa kabisa likizo ya uzazi na malipo.
Mtazamo wa likizo ya uzazi kwa wanaume, pia umeganyika kulingana na vyama vya siasa. Utafiti huo unaeleza kuwa wanachama wa chama cha ‘Republican’ ambao wana mawazo huru wanasema likizo hiyo siyo lazima. Mwanachama 1 kati ya 4 (26%) wa Republican ambaye ni Mhafidhina anafikiri mwanaume hapaswi kabisa kuondoka kazini kwa ajili ya masuala ya uzazi.
Lakini asilimia 13 tu ya wanachama wenye msimamo wa kawaida wanakubaliana na dhana hiyo huku asilimia 91 ya wanachama wa chama cha ‘Democrat’ hawakubaliani na na wanaume kunyimwa likizo ya uzazi.
Pia imebainika kuwa upinzani wa likizo hiyo unakuwa mkubwa kadiri mtu anavyozidi kuwa mtu mzima. Mathalani Wamerikani wenye umri wa miaka 65 na kuendelea ambao kwa asilimia 36 walisema sio lazima kupewa likizo hiyo. Lakini wanaume waliopata watoto wachanga wanaona ni muhimu kupata likizo ili wajumuike na familia zao kuimarisha upendo.
Tanzania na Ulaya wasimama kidete
Wakati raia wa Nigeria na Marekani kwa sehemu wakipinga likizo ya uzazi kwa wanaume, wananchi wa Ulaya na Tanzania wanakubaliana na kuwepo kwa likizo hasa katika mtazamo wa usawa wa kijinsia.
Aliyewahi kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Fedha na Mipango ya Maendeleo ya Zanzibar, Omar Yussuf Mzee amewahi kusema kuwa likizo ya uzazi kwa akina baba pindi wake zao wanapojifungua inasaidia ulezi wa wazazi wawili baina ya mama na baba.
“Hatua hii itasaidia kuondokana na ile dhana kwamba suala la afya ya uzazi linamhusu mama pekee. Lakini hatua hii inategemewa iwe chachu ya kuwashirikisha akina baba katika harakati zote za huduma ya afya ya uzazi na mtoto,” alinukuliwa Waziri Mzee.
Kwa mujibu wa jalida la Business Insider, linaeleza kuwa nchi ya Sweden ndio ina sera nzuri ya likizo ya uzazi ambapo inatoa likizo ya siku 480 kwa wazazi waliopata mtoto kwa mara ya kwanza inayoambatana na malipo ya asilimia 80 ya mshahara wa kawaida.
Wanaume wametengewa siku 90 (miezi 3) likizo ya malipo ya uzazi. Wanaopewa kipaombele ni akina baba ambao wanapata mtoto kwa mara ya kwanza. Sweden wanaamini kuwa likizo hiyo inaimarisha uhusiano kati ya baba na mtoto wakati ambao wazazi wote wawili wameelekeza macho yao kwa kumlea.
Nchini Norway, akina baba wanapata likizo ya wiki 0 hadi 10, huku wanaume wa Finland wanapewa wiki 8 lakini mtoto akifikisha miaka 3 baba anaweza kuchukua likizo ya malezi. Akina baba wa Slovenia nao wana siku 90 za likizo ambazo huambatana na malipo ya asilimia 100 kwa siku 15 za mwanzo. Lakini likizo inaweza kuanza hata kabla mama hajajifungua.
Nchi za Ulaya zimefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuimarisha usawa wa kijinsia kwenye sekta ya afya ya mama na mtoto.
Licha ya mitazamo tofauti ya likizo ya uzazi kwa wanaume, tafiti nyingi zimethibitisha wazi kuwa likizo hiyo ni njia nzuri ya kurejesha na kuimarisha upendo na muunganiko wa familia.