PORI la wanyamapori la Liparamba lililopo wilayani Mbinga, mkoani Ruvuma sasa lipo kwenye ramani ya Dunia kwakuwa ni ushoroba wa wanyama kutoka Tanzania na Msumbiji kupitia mto Ruvuma.
Pori hilo lililopo mpakani lilikabidhiwa rasmi kwa serikali ya wilaya ya Mbinga, tarehe 5 Juni 2006. Lina ukubwa wa kilometa za mraba 570. Hii ni asilimia 6.4 ya eneo la wilaya ya Mbinga ambayo ina jumla ya kilometa za mraba 11,396.
Meneja wa Pori la akiba la wanyamapori Liparamba Hashim Sariko anasema pori hilo lenye urefu wa kilometa 23 lina utajiri wa madini ya dhahabu, kiwango cha juu cha uoto wa asili wa misitu minene ya miombo, yenye rangi ya kijani mwaka mzima.
Anabainisha kuwa hifadhi hiyo inapakana na Msumbiji kwa upande wa kusini, mto Ruvuma kwa upande wa mashariki, mito Lumeme na Lunyele inapita ndani ya hifadhi hiyo na Kaskazini inapakana na milima ya Goma la Mpepo ambayo ni miongoni mwa milima mirefu wilayani Mbinga.
Pori linapakana na vijiji saba ambavyo ni Liparamba, Ndondo, Mipotopoto, Mitomoni, Mseto, Mtua na Mpepai. Wakazi wa vijiji hivyo hawana mifugo inayokidhi mahitaji ya chakula na kitoweo; hali inayosababisha baadhi yao kuendesha uwindaji haramu katika hifadhi hii.
Wawindaji wanatumia bunduki, magobore na wakati mwingine hutumia njia ya kuchoma moto ndani ya hifadhi ili waweze kuwazingira wanyama na kuwaua kwa ajili ya mlo wa kawaida au kitoweo.
Ndani ya hifadhi ya Liparamba kuna aina mbalimbali za wanyama. Kuna palahala, swala mkubwa(tandala) , boko, pofu, mbawala, mbuzi mawe, ngolombwe mnyama ambaye anafanana na swala, chui, simba na fisimaji.
Wanyama wengine ni nyani-manjano, tumbili, nguruwe na ngiri. Vilevile kuna ndege wa aina mbalimbali wakiwemo njiwapori,kanga na kware
Meneja wa pori hilo Hashim Sariko anasema Siku za hivi karibuni wanyama kama tembo, pundamilia, nyati, nyumbu na mbwamwitu, wameonekana katika pori hilo.
Hapa ni ndani ya hifadhi ya wanyamapori Liparamba ambapo mto Lunyere unapita ndani ya hifadhi ,maji ya mto huu yanatumiwa na wanyamapori licha ya watalaamu kueleza kuwa maji ya mto huo yana sumu
Sariko anabainisha kuna baadhi ya wanyama wanahama kutoka Msumbiji na kuingia Tanzania kwa kuzingatia hifadhi hiyo iko mpakani mwa nchi hizi mbili.
Hifadhi hii inakabiliwa na uchomaji moto, uwindaji usioratibiwa, uchimbaji madini (dhahabu) na uoshaji madini hayo kwa zebaki inayoingia mtoni na uvamizi unaofanywa na wakulima ambao wameweka mashamba.
Sariko anasema kuwa Katika hifadhi hiyo zinapita barabara kuu mbili za Mpepai-Liparamba na Liparamba-Mitomoni. Katika mwingiliano huu, ndimo wanapita wawindaji wasio na vibali na wakulima wavamizi wa ardhi.
Kwa mujibu wa meneja wa hifadhi ya Liparamba kila mwaka, baada ya mavuno wananchi wanaozunguka hifadhi wamekuwa na kawaida ya kuchoma moto ambao huingia hata katika hifadhi, hali inayoathiri vibaya wanyama na viumbehai waliopo ndani ya hifadhi hiyo.
Sariko anayataja madhara ya moto katika hifadhi hiyo kuwa ni pamoja na kutekekeza malisho na makazi ya wanyama,kuunguza wanyama,kuunguza uoto kwenye vyanzo vya maji na kuharibu vyanzo hivyo.
“Changamoto moja kubwa ya hifadhi hii ni wanannchi wa vijiji vya Mipotopoto,Mseto na Mitoni wanalima mpakani na ndani ya hifadhi,katika kijiji cha Jangwani wanalima na kujenga ndani ya hifadhi,kinyume na sheria ya wanyamapori namba tano ya mwaka 2009,kifungu cha 15,17,18,40 na 74’’,anasema.
Sariko anabainisha zaidi kuwa ulimaji wa mazao ya kawaida mpakani na ndani ya hifadhi umechochewa na upatikanaji wa kitoweo kwa urahisi na ulimaji wa bangi katika maeneo yasiyofika kwa urahisi katika msimu wa mwaka huu yameharibiwa mashamba ya bangi zaidi ya ekari tatu ndani ya hifadhi pamoja na kuharibu mitego ya wanyama mbalimbali.
Mwanzilishi wa pori hilo mbunge mstaafu wa Mbinga Mashariki Ngwatura Ndunguru anasema Tanzania inalenga kuboresha utalii kusini na kwamba hivi sasa watalii wanachokifuata kaskazini pia wanaweza kukipata kusini kwa kuwa kuna utalii wa aina mbalimbali.
Ndunguru ambaye pia ni afisa mstaafu wa wizara ya maliasili na utalii anasisitiza kuwa katika kufikia malengo ya millenia,maendeleo ya miaka 25 ijayao ni mazingira na sio vifaa,barabara au majengo kutokana na ukweli kuwa Tanzania ni ya tatu Duniani katika biodervasity.
Joakimu Lipanga ni paroko wa parokia ya Liparamba. Anasema wananchi katika kijiji hicho wanasafisha mashamba yao kwa kuchoma moto hali inayosababisha moto kuingia hadi ndani ya hifadhi na kuunguza ikolojia yake.
Naye Sigilinde Nombo, mkazi wa Liparamba anasema tatizo la uchomaji moto ni kubwa na kwamba mara nyingi pori huungua na kusababisha wanyama kuhama na wengine kuungua na kubakia na majeraha au kufa.
Kuhusu uwindaji ambao haujaratibiwa, meneja mkuu wa pori hilo Bwana Sariko anasema hadi sasa katika operesheni kabambe waliyoendesha kuzunguka vijiji vyote vya kata za Liparamba na Tingi, wamefanikiwa kukamata magobore 29 yasiyomilikiwa kihalali.
Sariko anasema uongozi wa hifadhi hiyo umedhamiria kufanya doria endelevu eneo lote la vijiji vinavyozunguka hifadhi pamoja na ukaguzi wa mara kwa mara wa silaha katika eneo hilo.
Hata hivyo, katika kijiji cha Mitomoni, baadhi ya wananchi waliohojiwa walidai kuwa baadhi ya silaha zinazotumika kuulia wanyama mbugani, zinachukuliwa nchini Msumbiji kutokana na wananchi wa vijiji vya mpakani kuwa na mahusiano ya kutembeleana na kuuziana vitu mbalimbali.
Sera ya Taifa ya mazingira kuhusu sekta ya wanyamapori, Ibara Na.58 inaelekeza maliasili za wanyamapori kulindwa na kutumika kwa misingi ya tathimini makini hasa katika maeneo yenye shinikizo na aina za wanyama walio hatarini kutoweka.
Nayo sera ya taifa ya misitu kuhusu wanyamapori katika Kifungu Na. 4.3.3 inasema uvamizi, moto, uvunaji haramu na ujangili katika misitu ya hifadhi, vimechangia katika kupungua kwa wanyamapori na kwamba usimamizi hafifu wa misitu na upungufu wa miundombinu vimechangia katika kulikuza tatizo hilo.
Yote haya yanabaki kuwa changamoto kwa walinzi wa maliasili za taifa.