Sasa unaweza kutalii mikumi kwa miguu

Albano Midelo

HIFADHI zilizo nyingi za  wanyamapori zilizopo hapa nchini watalii wanaruhusiwa kuangalia wanyama  wakiwa ndani ya magari ya kubeba watalii kuhofia kushambuliwa na wanyama wakali kama simba,tembo faru au chui pamoja na wanyamapori wengine.

Hata hivyo hali ni tofauti kabisa katika hifadhi ya Taifa ya mikumi iliyopo mkoani Morogoro yenye wanyama wenye mvuto wa kipekee ambao wengi wanawafurahia kuwaona hata wanapopita katika barabara kuu ya Iringa Dar es salaam ambayo inapita kwenye hifadhi ya Mikumi.

Mtalii katika hifadhi ya Taifa ya mikumi anaweza kutembea kwa miguu kwa kusindikizwa na  na kiongozi wa watalii na askari wa kulinda usalama wao ili wasidhuriwe na wanyama wakali anasema mhifadhi mkuu wa Mikumi John  Shemkunde.

Anabainisha kuwa njia ya watalii kutembea kwa miguu kuangalia wanyama inavutia watalii wengi  wa ndani na nje ya nchi na kusisitiza kuwa  bado watalii wengi wanatumia magari kuangalia wanyamapori kwa kuongozwa na kiongozi wa watalii wanapotembelea hifadhi hiyo.

Anawataja baadhi ya wanyama ambao ni kivutio cha watalii katika hifadhi hiyo kuwa ni chui, simba, mbwamwitu, twiga, nyati, tembo, kongoni, tandala mdogo, pofu, nguruwepori pamoja na wanyama wengine wengi na kusisitiza kuwa mtalii wa ndani pia anaweza kuwaona wanyama wengine kama mamba,kiboko,nyumbu,swalapala,nyani,ngedere,mbega,fisi,pundamilia,palahala,aina mbalimbali za ndege wapatao 360,nyoka na wadudu.

Anabainisha zaidi kuwa hifadhi ya Taifa ya Mikumi ina vilima vinavyolizunguka bonde la mto Mkata na pia upo mlima unaoitwa Malundwe ambao ni sehemu ya safu ya milima maarufu ya Tao la Mashariki iliyopo mkoani Morogoro yenye misitu na bioanuwai kubwa na ya kipekee duniani ikiwemo mbuga ya bonde la mto Mkata.

Baadhi ya wananchi wakiwa ndani ya hifadhi ya Taifa ya Mikumi

“Tathimini ya eneo hili kubwa na la kipekee duniani ilifanyika Oktoba mwaka 2010 na kuonyesha kuwa zaidi ya asilimia 75 ya eneo hili limekuwa likitumiwa na wanyama kama mapito,karne na karne,lipo chini ya usimamizi wa Ranchi ya Mkata na Halmashauri ya wilaya ya Mvomero ‘’,anasisitiza Shemkunde.

Anabainisha zaidi kuwa hali ya mapito kwa wanyama waliopo katika hifadhi hiyo yanaonesha kuwa awali yalikuwa mapito ya asili ya wanyama yakiunganisha hifadhi za Taifa za Mikumi eneo la Wami-Mbiki,kusini mwa Mikumi na pori la akiba la Selous.

Hata hivyo kutokana na shughuli za kibinadamu kama vile kilimo na kuanzisha makazi maeneo hayo hivi sasa yamezibwa na kwamba kuna maeneo mawili tu  ya kaskazini mashariki mwa hifadhi ya Taifa ya Mikumi Twatwatwa ambayo yanatumiwa na wanyama kama eneo la mtawanyiko wa twiga,tembo,pongo,ngiri,swalapala,pundamilia,mbogo na fisi.

Sehemu kubwa ya eneo hili lipo chini ya mamlaka ya ya Ranchi ya Mkata ambapo sehemu ndogo ya chini ya asilimia 25 ipo kwenye eneo la Twatwatwa lilipo nje ya Ranchi hiyo.

Kuhusu sehemu ya kaskazini ya hifadhi ya Taifa ya Mikumi-Wami- Mbiki mhifadhi mkuu wa Mikumi anasema eneo hilo ni mapito ya wanyamapori kutokea Mikumi kwenda eneo la Wami-Mbiki  ambalo ni hifadhi ya jamii.

Akizungumzia mafanikio ambayo hifadhi hiyo imeyapata Shemkunde anabainisha kuwa idadi ya watalii wanaotembelea hifadhi hiyo imekuwa inaendelea kuongezeka kila mwaka kutokana na vivutio ambavyo vinapatikana katika hifadhi hiyo maarufu hapa nchini.

Kulingana na mhifadhi mkuu huyo katika kipindi cha   mwaka 2007/2008 na mwaka 2009/2010  zaidi ya watalii 52,000 kutoka nje ya nchi walitembelea hifadhi hiyo ambapo watalii wa ndani katika kipindi hicho walikuwa ni  zaidi ya 55,000

Anasema ongezeko la watalii wa ndani limetokana na  utekelezaji wa sera ya mamlaka ya Taifa ya hifadhi  za Tanzania TANAPA ya kutangaza na kuhamasisha utalii wa ndani nchini  kila mwaka ikiwa ni pamoja na kutumia maadhimisho,sherehe za Mei mosi,maonyesho ya biashara za  kimataifa nchini yaani Sabasaba,maonyesho ya wakulima yaani Nanenane pamoja na sikukuu nyingine.

Hata hivyo anasema idadi ya watalii wa nje ya nchi imeonyesha kuongezeka kwa kiasi kidogo mwaka 2008/2009 kutokana na kuyumba kwa  uchumi duniani na kusababisha watalii wengi wa nje kuhairisha safari zao za kitalii hapa nchini pamoja na nchi nyingine.

“Mwaka jana uchumi wa dunia umeonyesha kuimarika tena ambapo idadi ya watalii imeongezeka na kuwa na matumaini ya uchumi wa dunia kuendelea kuimarika,idadi ya watalii wa nje hivi sasa inaendelea kuongezeka,mapato yatokayo na utalii  kwa ujumla yameongezeka kwa kila mwaka kwa mfano   mapato ya utalii yaliongezeka kutoka  zaidi ya milioni 135 mwaka 2008/2009 hadi kufikia zaidi ya milioni 881 mwaka 2009/2010’’,anasema.

Hifadhi ya Taifa ya Mikumi ina nyumba za kulala watalii na hoteli za kisasa kwa ajili ya watalii wa ndani na nje na kusisitiza kuwa hivi sasa TANAPA imejenga baadhi ya nyumba kwa ajili ya watalii wa ndani na nje ya nchi na bei ya malazi inategemea uwezo wa mtu.

Ameyataja malengo ya hifadhi hiyo kuwa ni kujenga hosteli mpya ,kubwa na za kisasa ili kukidhi mahitaji ya makundi ya kielimu na kuongeza mapato yatakayotokana na gharama za malazi  na kusisitiza kuwa ujenzi huo utafanikiwa endapo ada za viingilio vya watalii zitapandishwa  ili kuweza kukidhi mahitaji ya hifadhi,uendelezaji hifadhini na huduma za watalii.

Hata hivyo anasisitiza kuwa hifadhi ya Taifa ya Mikumi itaendelea kuimarisha miundombinu yake kwa awamu kila mwaka mpya wa fedha  na kwamba kati ya kilometa 550 za barabara zilizopo ni kilometa 400 zinatumika kwa utalii na kilometa 150 zinatumika kwa kazi za utawala na doria.

Mipango mingine ya kuiendeleza hifadhi hiyo ya Taifa ni kuendelea kubainisha  maeneo mapya yenye vivutio vya utalii na kutengeneza barabara na vivuko zaidi ili kuwafikisha watalii kwenye vivutio mbalimbali na wawepo hifadhini kwa siku nyingi ili kuongeza mapato.

Mikakati mingine anaitaja kuwa ni kutengeza barabara ya kuunganisha utalii wa hifadhi ya Mikumi na pori la Selous ili watalii wawepo hifadhini kwa siku nyingi na kuongeza mapato  ya hifadhi na uchumi wa nchi kwa ujumla

Ametoa wito kwa shirika la ugavi wa umeme nchini TANESCO kuingiza umeme wa TANESCO hifadhini ili kukidhi mahitaji ya uendeshaji na huduma kwa watalii kutokana na ukweli kuwa  umeme uliopo hifadhini hautoshelezi mahitaji ya watalii.

Akizungumzia changamoto ya ujangili ndani ya hifadhi Shemkunde anaitaja aina ya ujangili unaofanywa katika mbuga hiyo kuwa  ni wa kuwinda wanyama na kuua,kuingia hifadhini bila kibali,kukata miti ovyo,kupasua mbao,kuchoma mkaa,kuvamia mpaka wa hifadhi,kupitia lango rasmi na  kuvamia hifadhini kwa shughuli za kilimo na makazi.

Hata hivyo anasema upatikanaji wa taarifa za ujangili mara nyingi zimekuwa zinapatikana kwa kuwashirikisha watoa habari vijijini waliotambuliwa kwa njia za kiintelijensia inayofanywa  na watumishi askari na wahifadhi kwa kuwashirikisha watoa habari.

3 Comments
  • Tunashikiru kwa taarifa hii, hii inaonyesha ukuaji wa utalii Tanzania. Lakini nahofia ni njia zipi anuwahi zitakozotumiwa pindi myama mkali atakapojitokeza, je ni kumuua au yeye kuua watu.

    Pia, kwa mujibu wa picha uliyoweka mahali hapa, naona watu wanajisaidia haja ndogo. Je huu ni utalii au uharibifu wa mazingira? Unaonyesha taswira gani katika jamii? Kwamba twende tukaharibu mazingira?

    Ni vema ukajaribu kutafakari sana ni picha gani iwekwe pale mtu unapokua unahamasisha jambo, tena jambo lenyewe nyeti kama utalii.

    Tunashukuru kwa taarifa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *