Mabadiliko ya Mitaala yanavyoathiri mfumo wa Elimu Tanzania

Jamii Africa

DHANA na msingi mkubwa wa maendeleo yoyote duniani ni kubadilika. Hii ina maana kuwa mabadiliko yenye tija kwa wananchi, yanayoonesha wapi mustakhabali wa nchi ilikotoka, iliko na inakoelekea na ilipokosea.

Mabadiliko yasiyoharibu yaliyokwishafanywa na kuboresha yajayo ndiyo mahitaji makubwa ya wananchi. Mabadiliko yoyote lazima yachukue muda katika utekelezwaji wake kabla ya kubadilishwa tena.

Kwa muda mrefu tangu Sera ya Elimu iundwe kwa mara ya kwanza mwaka 1995, mfumo wa elimu wa Tanzania umekabiliwa na changamoto ya mabadiliko ya mara kwa mara yaliyoathiri taasisi na mfumo mzima wa elimu.

FikraPevu inaona kuwa, yamkini mabadiliko haya ya elimu yanatokana na mabadiliko yanayotokea kwenye mifumo mikuu ya kiutawala.

Kutodumu kwa muda mrefu katika utekelezwaji, kuhitilafiana na hali halisi ya elimu nchini, kutoangalia na kuzingatia upungufu katika utekelezaji wa mabadiliko ya mitaala iliyopita kwa ujumla ni kasoro kubwa za mabadiliko haya yanayotokea sasa ambayo athari zake ni kurudisha nyuma elimu.

Mnamo Mei 2014 serikali ilizindua Sera mpya ya Elimu na Mafunzo yenye dhamana ya kusimamia sekta nzima ya elimu. Haya pia ni mabadiliko makubwa ambayo yametokana na kufutwa kwa sera kadhaa zilizokuwa zinasimamia elimu ambazo ni Sera ya Elimu na Mafunzo ya 1995, Sera ya Elimu na Mafunzo ya 1996, na Sera ya Elimu ya Juu ya mwaka 1999.

Sera hii mpya ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014, imeainisha matamko kadhaa ambayo serikali ikishairikiana na wadau mbalimbali wa elimu, itayatekeleza.

Matamko makubwa ambayo utekelezaji wake umeanza kuonekana ni yale yanayohusu mabadiliko ya muundo wa elimu awali, msingi, sekondari na elimu ya juu ambapo tofauti na muundo huo mpya wa elimu utakuwa ni 1 + 6 + 4 + 2 + 3.

Hii maana yake ni kwamba, elimu msingi kwa sasa itaanzia awali/chekechea hadi kidato cha nne ambayo upatikanaji wake utakuwa ni wa lazima na bure.

Muundo huo mpya wa elimu umeanza kutekelezwa na serikali ikisaidiwa na wadau wachache walioonesha mwitikio katika kuchangia sekta hii ya elimu. 

Awali muundo wa elimu uliokuwa unatumika ni 2+7+4+2+3 ambao licha ya ufanisi wake katika kuboresha elimu kwa muda mrefu bado umeonekana kutofaa kutokana na kutumia muda mwingi zaidi kabla ya mwanafunzi kuhitimu.

Lakini muundo huu mpya ulioainishwa ndani ya Sera ya Elimu na Mafunzo utagusa pia umri ambao mwanafunzi atatakiwa kujiunga na elimu ya awali ambapo badala ya miaka 5, kwa sasa itakuwa ni miaka 6.

Muda wa elimu ya msingi utakuwa ni miaka 10 ikijuimuisha miaka 6 ya darasa la 1 hadi darasa la 6 na miaka 4 ya kidato cha 1 hadi cha 4.

Kwa mujibu wa utafiti wa FikraPevu, darasa la 7 pamoja na mitihani iliyokuwa inatumika kuwapima wanafunzi uelewa wao kabla ya kujiunga na sekondari itafutwa.

Hali hii inawatia mashaka wadau mbalimbali wakishauri kuwa mitihani hiyo iendelee kutumika kumpima mwanafunzi kabla ya kujiunga na sekondari.

"Tathmini hii ilipendekeza kuwa muundo wa 1+6+4+2+3 ambao mhitimu atamaliza mzunguko wa masomo kwa muda mfupi na mikondo ya ufundi ijumuishwe kwenye elimumsingi na sekondari" (Ukurasa wa 9: Sera ya Elimu na Mafunzo ya 2014).

Mnamo Januari 8, 2017, serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ilitangaza mabadiliko katika mfumo wa elimu yatakayohusisha mitaala inayotumika kwa sasa ya elimu msingi, hatua ambayo imekuja ikiwa ni utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya 2014.

Mabadiliko ya muundo wa elimu ni miongoni mwa mabadiliko hayo ya mitaala.

Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwmaka 2014 ilizinduliwa rasmi mwaka 2014 lakini hata hivyo utekelezaji wa mipango, mikakati na matamko yake umeanza mwaka 2017 katika hatua za mwanzo kabisa.

Ndani ya muda wote huo mfumo wa elimu ulikuwa unatumia sera za elimu za zamani nilizokwishafutwa.

Je, kulikuwa na ulazima upi wa kuziachia sera hizi ziendelee kutumika huku kukiwa na sera mpya?

Taasisi ya Elimu Tanzania (TIE) ikishirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imekwishaandaa tayari mtaala wa elimumsingi darasa la 1 hadi la 2 na ule mtaala wa elimu msingi darasa la 3 hadi la 6.

Hii yote ni mitaala itakayotumika kwenye ngazi ya elimumsingi lakini sababu za utekelezaji wake hazijafahamika.

Licha ya hatua hizi zote zinazofanywa, bado serikali haijapeleka waraka rasmi kwa wakuu wa shule za msingi huku mwaka mpya wa masomo ukiwa umekwishaanza.

Licha ya kubadili muundo wa elimu, kufuta darasa la saba na mitihani ya darasa la saba, mabadiliko ya mitaala hii itagusa pia masomo ambapo kuanzia darasa la tatu masomo yatakayofundishwa ni 10 ambayo ni Kiswahili, Kiingereza, Uraia na Maadili, Hisabati, Maarifa ya Jamii, Sayansi na Teknolojia na Somo la Dini ambayo mihutasari kwa ajili ya masomo hayo imekwishaandaliwa.

Pia kuna ongezeko la somo la Elimu ya Sanaa na Michezo na Vilabu vya Ujasiriamali.

Wadau mbalimbali wanapendekeza kuwa masomo haya yanayoanza kufundishwa katika ngazi hii ya elimu lazima yapate muendelezo wake katika ngazi za juu za elimu ili kumsaidia mwanafunzi kujenga mazowea na haya masomo na kuyaelewa ipasavyo.

Hata hivyo, tumeona kuwa serikali imejizatiti katika kufanya jitihada za kuboresha hali ya elimu nchini kwa kutekeleza mipango na mikakati inayoonekana kuwa inafaa kama vile Sera ya Elimu.

Mengi yanastahili pongezi kwa hatua nzuri ambazo serikali imezichukua. Lakini maboresho hayo hayataweza kufanikiwa endapo changamoto zilizopo ndani ya mfumo wa elimu zitaendelea kuwepo.

Bila jitihada za dhati za kuziondoa changamoto hizi serikali itakuwa inadunisha elimu badala ya kuiboresha.

FikraPevu imebaini kuwepo kwa upungufu ufuatao unaoambatana na utekelezaji wa mabadiliko ya mfumo wa mitaala, kama ifuatavyo;-

Waketekezaji wakubwa wa mabadiliko haya ni walimu:-  Kutokana na mpango wa elimu bure uandikishwaji wa wanafunzi wa darasa la 1 na awali hasa kwa shule za umma umeongezeka na hivyo kufanya uwiano wa mwalimu-wanafunzi kuwa mkubwa.

Hali hii inatokana na serikali kusitisha ajira za walimu tangu mwaka 2015/2016.

Upandishaji wa madaraja na viwango vya mishahara, uboreshaji wa nyumba za kuishi walimu hasa wa vijijini, mazingira ya kufundishia na kujifunzia, posho na stahiki mbalimbali na madeni bado ni kero ambazo zinawakumba walimu wengi.

Je, bila kumjali walimu kwa kumtatulia kero zake hizi, utekelezaji wa mitaala hii mipya utapata ushirikiano kutoka kwa walimu hawa?

Semina elekezi kwa watekezaji wa mitaala mipya;- mahitaji ya semina elekezi (orientation seminar) kwa walimu kwa ajili ya utekelezaji wa mitaala hii mipya bado ni makubwa.

Serikali ilipeleka semina walimu wawili kutoka kila shule kwa ajili ya kupatiwa maelekezo haya. Changamoto iliyojitokeza mwaka huu baada ya kuanza kwa mpango wa elimu bure ni kwamba walimu hawa wameonekana kutotosheleza kwa idadi kubwa ya wanafunzi iliyoongezeka.

Tafiti pia zinaonesha kuwa wadau wengi wa elimu kama vile wamiliki wa shule binafsi hawaungi mkono uamuzi wa serikali kuondoa mtihani wa darasa la saba kuwapima uelewa wao kabla ya kujiunga na sekondari.

Hii ni kwa sababu kwa mfumo wa elimu yetu, mitihani ndicho kipimo pekee cha uelewa wa mwanafunzi. Kuondoa mitihani hii ni kuruhusu wanafunzi wasiofaa kuendelea na elimu.

Kama serikali imeondoa mitihani ya darasa la saba, kwanini mitihani hii isifanyike darasa la sita?

Tofauti za usimamizi na uendeshaji wa shule pia ni changamoto nyingine kwani shule nyingi za msingi zenye usimamizi binafsi zinatumia Lugha ya Kiingereza.

Hata hivyo T.I.E imelekeza kuwa msisitizo mkubwa kwa wanafunzi wa darasa la 1 na 2 uwe kwenye Lugha ya Kiswahili (KKK – Kusoma, Kuandika na Kuhesabu).

Kwanini suala la lugha lisiachwe kwenye mamlaka ya usimamizi wa shule kama ilivyoainishwa kwenye Sera ya Elimu na Mafunzo?

Usimamizi, uendeshaji na ugharamiaji wa elimu unaofanywa na serikali pia ni kizingiti kingine kinachokwisha ufanisi katika utekelezaji wa sera nyingi, mikakati na mipango mingi ya elimu.

Usimamizi kwenye ngazi zote za mamlaka za elimu kuanzia Wizara hadi shuleni ni dhaifu.

Pia kutokana na udhaifu kwenye ugharamiaji wa uendeshaji wa shule, mikakati na mipango mingi imeonekana kushindwa.

Shule nyingi zinategemea ruzuku kutoka serikalini na wadau mbalimbali wa elimu. Mpango wa elimu bure umekuja na changamoto zake katika ugharamiaji.

Ikiwa shule inashindwa kuwa na fedha kwenye mfuko wa shule, je, itaweza kununua vitabu na vifaa vingine vya kufundishia? Je, serikali ikishatenga fungu la fedha kwenye bajeti ya Wizara ya Elimu katika utekelezaji wa mabadiliko haya ya mitaala, yatakwenda sambamba na ongezeko la idadi ya gharama?

Uhaba wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia; utafiti pia unaonesha kuwa kwa kiasi kikubwa uhaba wa vifaa vya kufundishia unaolikumba taifa kwa sasa unaotokana na ongezeko kubwa la wanafunzi hasa wale wa shule za msingi unahusiana kwa karibu na utekelezaji wa mabadiliko haya mapya ya mitaala.

Vitabu vya kiada na ziada; mihutasari; vitabu vya rejea; maabara na vifaa vyake yote haya yanaweza kuchelewesha utekelezaji wa mabadiliko haya mapya ya mitaala.

Serikali pamoja na wadau wote wa elimu ni lazima waangalie na kufanya tathmini ya wapi ambako wanatakiwa kuanzia ili kuboresha sekta ya elimu.

FikraPevu inaona kwamba, kuanzisha mipango na mikakati kila siku ikiwa bado mazingira hayajaandaliwa kule inakoenda kutekelezwa ni kazi bure.

Ipo tofauti kubwa sana ya taasisi za elimu zinazomilikiwa na watu binafsi na mashirika na zile za umma.

Serikali ikiendelea kufumbia macho changamoto hizi za elimu basi tutakuwa mashuhuda wa kuona mipango na mikakati hii ikitekelezwa kwa ufanisi zaidi kwenye shule binafsi kwa sababu shule zetu za umma hazitaweza kumudu ushindani mkubwa kutoka shule hizo.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *