MADAKTARI katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando, Mwanza, wameungana na wenzao wa nchi nzima kusitisha mgomo na kuanza kutoa huduma ya matibabu, wakisubiri utekelezaji wa ahadi ya serikali na hivyo kupunguza adha iliyowakumba wananchi wa kanda ya ziwa.
Mwandishi wa FikraPevu aliyetembelea hospitali hiyo ameshuhudia madaktari waliokuwa zamu wakiendelea na kazi kwa mujibu wa ratiba.
“Ni kama unavyotuona tunaendelea na kazi kama kawaida. Mambo mengine tunasubiri utekelezaji wa ahadi ya Waziri Mkuu,” alisema daktari mmoja aliyekuwa kazini, lakini hakujitambulisha jina.
Hata hivyo, alisema baadhi yao hawakuwapo kazini mwishoni mwa wiki maelezo kwamba walikuwa wamesafiri nje ya jiji la Mwanza, wakihofia kukamatwa kwa kuhusikana mgomo huo.
“Mimi nipo kazini lakini sidhani kwamba sote tutakuwa kazini kwa sababu baadhi yetu walikuwa wamenza kusafiri nje ya jiji. Kauli ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda kwamba wanastahili kukamatwa nayo imechangia kuwatisha baadhi ya wenzetu,” alisema
Kwa upande wao, baadhi ya wagonjwa waliilaumu serikali kwa kuchelewesha mazungunzo na madaktari; na hivyo kusababisha madhara makubwa kwa wagonjwa na serikali kwa ujumla, na wengine walitupia lawama hizo kwa madaktari waliogoma.
“ Mimi binafsi ninampongeza Waziri Mkuu kwa hatua aliyoifikia; lakini kwa upande mwingine ninamlaumu kwa sababu amefikia muafaka ndani ya matatizo makubwa ambayo yametokea nchini tangu mgomo uanze,” alisema mgonjwa alijitambulisha kwa jina la Sospeter Nyanda.
Alidai kwa vyovyote vile, hali hiyo bado itaendelea kuwaathiri madaktari kiasi kwamba watafanya kazi katika hali ya wasiwasi; hadi serikali itakapoanza kutekeleza ahadi yake.
Alipoulizwa ofisini kwake juu ya mabadiliko hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali hiyo, Dk. Charles Majinge, alisema kwamba madaktari hospitalini hapo walikuwa kazini kama kawaida.
“ Mimi nilikuwa safarini; Lakini kwa ufupi ni kwamba madaktari katika hospitali ya Rufaa Bugando wanaendelea na kazi kama kawaida,” alisema Dk. Majinge.
Alisema aliporejea Mwanza alikutana na tangazo la madaktari hao katika mbao za matangazo kuhusiana na mgomo wao hadi madai yao yatakapopatiwa ufumbuzi.
Hata hivyo, alidai ni mapema mno kuthibitisha kwamba madaktari wote walikuwa wameripoti kazini .
“Siyo rahisi kusema kwamba madaktari wote wameingia ama wataingia kazini kwa mujibu wa ratiba za hospitali; ila nimewaagiza wakuu wa idara wafuatilie,” alifafanua Mkurugenzi huyo.
Alisema pia kwamba hakuna vifo vilivyotokea hospitalini hapo kutokana na mgomo huo, bali taarifa aliyoikuta inaonesha kuwepo kwa vifo kutokana na masuala ya kawaida.
“Kwa mfano kifo ninachokina hapa ni cha mama mmoja ambaye alifia wodini baada ya kuvuja damu nyingi mara baada ya kujifungua katika hospitali ya Butimba. Taarifa inaonyesha kondo la nyuma halikutoka na hivyo akavuja damu nyingi,” alisema Dk Majinge.
Habari hii imeandaliwa na Juma Ng’oko, Mwanza
Huyu Dk Majinge huwezi kumsikia wala kumuona kwenye MEDIA wakati wa Mgomo unaendeleaanapenda kuonekana msafi anakimbia na kuwaachia ofisi wasaidizi wake, na kusingizia kuwa alikuwa nje ya ofisi natabiri tar 7/3 hataonekana akitoa statement mpka mgomo iushe!!
Kifo cha huyo Mama si cha kawaida probably madakatri hawakuwa kazini, Postpartum hemorrhage (PPH) due tu Retained Placenta!!! hata kama ni Placenta Accreta, Yeye kama Obstetrician he should have known that huyo Mama hakutakiwa kufa(Maternal death was preventable) kama Madaktari wangekuwa kazini, na kama Daktari yeyote angehusika najua My GOOD old friend angefanya maisha ya huyo daktari kuwa Magumu sana!!