Kwa mara nyingine tena, China ni mwenyeji wa mkutano kuhusu mtandao wa Internet, unaofanyika katika mji wa Wuzhen, mkoani Zhejiang hapa China. Mada mbalimbali zinajadiliwa kwenye mkutano huu, ikiwa ni pamoja na maendeleo ya huduma ya Internet na Usalama wa Internet. Kwenye hotuba iliyotolewa na Rais Xi Jinping, na kusomwa kwa niaba yake na mkuu wa Idara ya usimamizi wa mtandao wa Internet ya China Bw. Wang Huning, Rais Xi amesema, “China iko tayari kuweka kanuni na mifumo mipya ya usimamizi wa mtandao wa Internet, ili kuzinufaisha pande zote na kukabiliana na hali ya kukosa uwiano iliyopo kwa sasa”.
Rais Xi ametoa kauli hii kutokana na ukweli kwamba China kwa sasa imepiga hatua kubwa kwenye sekta ya mtandao wa Internet, ikiwa ni pamoja na kufikisha mkonga wa mawasiliano karibu katika kila kona ya nchi, kuwa na viwanda vingi vya kutengeneza zana zinazotumia huduma ya internet kama vile kompyuta na simu aina ya smartphone, makampuni makubwa ya huduma za Tehama kama Huawei na ZET, na hata kuweka sheria na kanuni zilizopevuka kwenye usimamizi wa mtandao wa internet. Maendeleo haya bila shaka yanaifanya China istahili kuwa mwenyeji wa mkutano huu.
Kwa watu wengi wa nje au hata wageni wanaokuja kwa mara ya kwanza hapa China, licha ya kuvutiwa na maendeleo iliyopata China kwenye sekta ya mtandao wa internet, pia wanapenda kujua ni mbinu gani ambazo China imeweza kutumia kufanya mtandao wa Internet uwe salama.
Tukianza kuangalia upande wa maendeleo, kwa sasa hapa China, watu wengi wamepiga hatua kwenye matumizi ya Internet, kutoka kuwa njia ya mawasiliano au kupata habari, na kufikia kuwa njia muhimu ya kupata huduma za kimsingi za jamii, na hata kupunguza matumizi ya pesa taslimu. Kwa sasa miamala mbalimbali inafanyika kwa kutumia tovuti au vikoa kama vile Wechat na Alipay, au kufanya biashara au manunuzi kwa kutumia tovuti na vikoa kama vya tovuti maarufu za Taobao, au Jingdong. Lakini pia watu wanaweza kununua tiketi za ndege, treni au hata kufanya booking ya hoteli kwa kutumia tovuti na vikoa mbalimbali, teknolojia hii pia imefika kwenye eneo la matibabu na hata elimu.
Kwenye upande wa usalama, serikali ya China imewekeza vya kutosha kwenye kile kinachoitwa Great Firewall, ambacho kinazuia tovuti na vikoa visivyoendana na sheria, kanuni, maadili na hata kuhatarisha utulivu na masikilizano ya jamii. Na pia kuna sheria na kanuni matumizi ya internet
Kwenye mkutano huu Tanzania imewakilishwa na Dr. Kennedy Gastorn, ambaye ni katibu mkuu wa Shirika la ushauri wa kisheria la Asia na Afrika, ambaye kwenye mkutano huo ametaja hatua inazopiga Tanzania kwenye matumizi ya mtandao wa Internet, hasa kuwanufaisha watu wa kawaida, akitolea mfano kikoa kinachoweza kuwafahamnisha wakulima wa muhogo maendeleo ya zao la muhogo na hata kugundua kama muhongo umeathiriwa na ugonjwa. Kwa nchi kama Tanzania, hayo ni mafanikio makubwa, japokuwa tukiangalia ukubwa wa internet na matumizi yake, ni sawa na tone la mvua kwenye bahari.
Wakati nikipitia maendeleo ya huduma ya Internet kwa Tanzania, bado kuna kitu kimoja ambacho naona kinatatiza. Serikali imekuwa na kasi kubwa sana katika kuwekeza kwenye kufikisha huduma ya internet karibu kila kona ya Tanzania, lakini matumizi ya internet na elimu kuhusu matumizi yenyewe bado viko nyuma sana. Bado kuna uelewa mdogo sana kuhusu faida za mtandao wa internet kwa watanzania wengi. Matumizi makubwa ya internet yamejikita kwenye mitandao ya kijamii. Karibu kila mtanzania ukimuuliza atakwambia anafahamu tovuti za mitandao wa Facebook, YouTube, na wengine wengi watakwambia wanafahamu au hata kutumia vikoa vya WhatsApp, Line, IMO na vingine. Lakini ni karibu hakuna au ni wachache sana wanaofahamu wanaotumia tovuti zinazohusu taaluma mbalimbali kama kilimo, biashara, afya, elimu, au hata kujua tovuti ya serikali au hata idara zake. Hali hii inasikitisha na kukatisha tamaa.
Hapa China kuna idara maalum inayosimamia mtandao wa internet Cyberspace Administration of China (CAC), na kazi yake ni hiyo tu, kusimamia mtandao wa Internet. Lakini kwa sisi Tanzania inaonekana kama bado eneo hili halijapewa msimamizi maalum, na badala yake limepachikwa kwenye tume ya usimamizi wa mawasiliano TCRA. Hapa China pia watu wanaelemishwa kuhusu matumizi ya mtandao wa internet na faida na manufaa yake, lakini kwa sisi Tanzania bado watu wanajifunza wenyewe baada ya kununua simu au kompyuta. Hii ni changamoto. Wachina hapa wanawekewa ulinzi dhidi ya wadukuzi na hata kuchukua hatua watu wanapobainika kufanya vitendo hivyo, lakini kwa sisi maeneo haya yote bado tuna udhaifu. Hakuna ubaya kama tukifanya ushirikiano zaidi kwenye maeneo haya.
Ni vizuri tukitambua kuwa matumizi ya internet kwa sasa yamepiga hatua kubwa ikilinganishwa na miaka kumi iliyopita. Hivi karibuni tume ya mawasiliano ilisema idadi ya watanzania wanaotumia simu za mkononi imeongezeka kutoka watu milioni 2.1 wa mwaka 2005 na kufikia watu milioni 40.1 kwa mwaka 2016. Na karibu kila mtanzania mwenye smartphone, akitaka kutumia huduma ya internet anaweza kufanya hivyo. Lakini maendeleo hayo pia yameonyesha udhaifu mkubwa kwenye jinsi watanzania tunavyitumia internet, kiasi kwamba wengine wanaishia kuvunja sheria.
Utafiti uliofanywa hivi karibuni na Twaweza, umeonyesha kuwa watu 358 walikamatwa katika mwaka 2015, na wengine 911 walikamatwa katika mwaka uliofuata kutokana na makosa ya mtandao wa internet. Kwa baadhi ya watu wanaweza kuilamu serikali kuwa inazuia uhuru wa kutoa mawazo, lakini mimi nalaumu “ujinga” au matumizi mabaya ya uhuru wa kutoa maoni, ndivyo vinawaponza watu. Hatuwezi kuilaumu serikali kwa kuwaadhibu watu wanaotumia mtandao kutukana viongozi wetu au kueneza chuki na uongo, kwa kisingizio cha kulinda uhuru wa kutoa maoni. Labda tujiilamu kuwa hatujaweka utaratibu wa kuwafundisha watu kuhusu mambo ya kuepuka wakati wa kutumia mtandao wa internet.
Tukubali kuwa tunatakiwa kupata japo “elimu ya kufuta ujinga” kwenye matumizi ya internet, iwe ni mashuleni au hata kama ni kwenye madarasa maalum. Na sio kuilaumu serikali bila kuangalia ni kwanini serikali inachukua hatua inazochukua. Sheria zilizowekwa na bunge, zipo kuhakikisha watu wanatumia internet kwa njia inayostahili, na sio kuzuia uhuru wa watu kutoa maoni, kama inavyosemwa na baadhi ya watu. Tunatakiwa kukumbuka kuwa tunapotumia internet tuna haki na wajibu.