MWELEKEO WA MVUA ZA MACHI HADI MEI (MASIKA) 2012 NCHINI TANZANIA

Jamii Africa

MWELEKEO WA MVUA ZA MACHI HADI MEI (MASIKA) 2012 NCHINI TANZANIA
Taarifa hii inatoa tathimini ya msimu wa mvua za Vuli kwa miezi ya Oktoba hadi Disemba
2012, mvua zinazoendelea katika maeneo ya kanda ya kati, magharibi, nyanda za juu kusini
magharibi na mikoa ya kusini pamoja na mwelekeo wa mifumo ya hali ya hewa na mvua za
Masika katika kipindi cha miezi ya Machi hadi Mei, 2012.
A. UTANGULIZI
Tathimini ya mvua za Vuli katika kipindi cha miezi ya Oktoba hadi Disemba 2011 inaonyesha
kuwa maeneo mengi ya nchi yalipata mvua za kutosha. Baadhi ya maeneo ya nchi yalipata mvua
nyingi na kulikuwa na vipindi vya mvua kubwa kuelekea mwishoni mwa msimu ambazo
zilisababisha maafa katika baadhi ya maeneo ya Dar es Salaam, Mara, Manyara, Mbeya, Arusha,
Kilimanjaro na Mwanza. Hata hivyo, mtawanyiko wa mvua hizo haukuwa mzuri. Maeneo
machache yanayopata msimu mmoja wa mvua (mikoa ya Ruvuma, Mtwara, Lindi pamoja na
kusini mwa Morogoro) yalipata kiwango kidogo cha mvua.
Mwelekeo wa msimu wa mvua za Machi hadi Mei, 2012 unaonyesha maeneo mengi yanayopata
misimu miwili ya mvua kwa mwaka yanatarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani,
isipokuwa kwa mkoa wa Shinyanga ambao unatarajiwa kupata mvua za wastani. Mvua
zinazoendelea kunyesha kwenye maeneo yanayopata msimu mmoja wa mvua kwa mwaka
zinatarajiwa kuwa za wastani katika maeneo mengi isipokuwa katika maeneo ya kusini mwa
Iringa, Ruvuma na Mtwara ambayo yanatarajiwa kupata mvua za wastani hadi chini ya wastani.
Mvua hizi zinatarajiwa kuendelea mpaka mwishoni mwa mwezi wa Aprili 2012. Viashiria
vilivyopo na vinavyotarajiwa kusababisha mvua hizi ni kuwepo kwa joto chini ya wastani katika
maeneo ya tropikali ya bahari ya Atlantiki, sambamba na kuwepo kwa joto juu ya wastani katika
maeneo ya kusini-magharibi mwa bahari ya Hindi. Hali hii inatarajiwa kusababisha upepo wenye
unyevunyevu kutoka misitu ya Kongo kuvuma kuelekea nchini mwetu.
B: TATHMINI YA MVUA ZA VULI OKTOBA HADI DISEMBA 2011
Mvua katika kipindi cha miezi ya Oktoba hadi Disemba 2011, ziliendelea vizuri katika maeneo
mengi ya nchi.. Hata hivyo mtawanyiko wake haukuwa wa kuridhisha ambapo baadhi ya
maeneo yalipata mvua kubwa kuelekea mwishoni mwa masimu. Vifuatavyo ni viwango vya
mvua pamoja na wastani wa muda mrefu katika baadhi ya vituo hivyo:
2
Maeneo yanayopata mvua mara mbili kwa mwaka:
Pwani ya Kaskazini: Tanga 244.5 mm (280.8%), Pemba 389.2mm (189.5%), Mlingano
557.9mm (336.7%), Handeni 164.4mm (68.9%), Kizimbani 282.7mm (95.8%), Zanzibar
342.0mm (96.4%), Morogoro 83.8mm (110.1%) na JNIA 469.9mm (94.2%).
Nyanda za juu Kaskazini Mashariki: Moshi 102.4mm (122.8%), Lyamungu 179.2mm
(189.2%), Same 66.0mm (65.5%) na KIA 105.5mm (329.7%).
Kanda ya Ziwa Viktoria: Mwanza 247.2mm (113.2%), Bukoba 347.8 mm (128.8%), Musoma
142.8mm (117.8%) na Shinyanga 276.5mm (125.1%).
Maeneo yanayopata msimu mmoja wa mvua kwa mwaka:
Magharibi: Tabora 91.7 mm (63.2%) na Kigoma 202.2mm (101.1%).
Kanda ya Kati: Dodoma 38.2mm (51.8%), Hombolo 60.2mm (154.4%) na Singida 50.6mm
(34.7%).
Nyanda za Juu Kusini Magharibi: Iringa 141.3mm (94.1%), Mbeya 92.0mm (36.9%), Tukuyu
312.6 mm (253.7%) na Igeri 163.0mm (250.8%).
Maeneo ya Kusini: Mtwara 81.7mm (70.0%), Kilwa 118.5mm (166.2%) na Songea 81.4mm
(169.6%).
Viwango vya mvua chini ya asilimia 75 ya wastani kwa kipindi kirefu hutafsiriwa kama chini
ya wastani, wakati viwango vya kati ya asilimia 75 hadi 125 hutafsiriwa kama mvua za
wastani na vile vya zaidi ya asilimia 125 hutafsiriwa kama juu ya wastani.
C: MWELEKEO WA MIFUMO YA HALI YA HEWA
Mwelekeo huu umezingatia hali ya mifumo ya hali ya hewa iliyopo na inayotarajiwa na athari
zake kwa msimu ujao wa mvua za Masika (Machi hadi Mei), 2012 hapa nchini.
Uchambuzi wa hali ya joto katika ukanda wa tropikali ya bahari ya Pasifiki kwa kipindi cha
mwezi Februari 2012 unaonyesha hali ya joto lililo chini ya wastani ambalo linaashiria kuwepo
kwa La Niña hafifu. Mwelekeo katika kipindi cha Mwezi Machi hadi Mei unaonyesha kuwepo
kwa ongezeko kidogo la joto la bahari litakalopelekea kutoweka kwa La Niña na joto la Bahari
linatarajiwa kuwa la wastani.
Joto chini ya wastani katika tropikali ya Bahari ya Atlantiki linatarajiwa kuendelea katika
kipindi chote cha msimu likiambatana na ongezeko kidogo la joto kusini-magharibi mwa bahari
ya Hindi na hivyo kupelekea kuwepo kwa upepo kutoka magharibi kuvuma kuelekea katika
maeneo ya nchi yetu , hali ambayo inatarajiwa kusababisha ongezeko la mvua hususani
magharibi mwa nchi.
Tofauti ndogo ya joto kati ya Magharibi na Mashariki mwa Bahari ya Hindi inatarajiwa kuwepo
kwa kipindi chote cha Mwezi wa Machi, 2012. Hali hii inatarajiwa kusababisha kuvuma kwa
upepo kutoka Baharí ya Hindi kuelekea pwani ya Afrika Mashariki.
Mifumo ya migandamizo ya hali ya hewa kwa maeneo yaliyopo kaskazini mwa Tropiki ya
Kansa inatarajiwa kuwa hafifu ukilinganisha na maeneo yaliyopo Kusini mwa Tropiki ya
Kapirikoni. Hali hii inatarajiwa kusababisha Ukanda wa Mvua kutoka kusini kuelekea kaskazini
kupanda kwa haraka hivyo kupelekea mvua katika msimu wa masika kuisha mapema.
3
Kutokana na ongezeko dogo la joto linalotarajiwa katika ukanda wa kusini-magharibi mwa
Bahari ya Hindi pamoja na viashiria vingine, matukio ya vimbunga kusini-magharibi mwa
Bahari ya Hindi yanatarajiwa kuongezeka na hivyo kusababisha kuongezeka au kupungua kwa
mvua katika baadhi ya maeneo nchini kulingana na nguvu ya vimbunga hivyo na maeneo
vitakapotokea.
D: MWELEKEO WA MVUA MACHI –MEI 2012
(i) Mvua za Masika
Maeneo ya kaskazini mwa nchi yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka, mvua
zinatarajiwa kuanza wiki ya kwanza ya mwezi Machi, 2012. Mvua hizo zinatarajiwa kuwa kama
ifuatavyo:
Kanda ya Ziwa Viktoria: (Mikoa ya Kagera, Mara, Mwanza na Shinyanga): Mvua zinatarajiwa
kuanza wiki ya kwanza ya mwezi Machi, 2012. katika mikoa ya Kagera, Mara na Kigomakaskazini,
na kusambaa katika maeneo mengine (Mwanza na Shinyanga) wiki ya pili ya mwezi
Machi. Mvua hizo zinatarajiwa kuwa za juu ya wastani katika mikoa hiyo, isipokuwa mkoa wa
Shinyanga ambapo mvua zinatarajiwa kuwa za wastani .
Ukanda wa Pwani ya Kaskazini: (Mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Pwani, Morogoro-kaskazini
pamoja na Visiwa vya Unguja na Pemba): Msimu wa mvua unatarajiwa kuanza wiki ya kwanza
ya mwezi Machi, 2012. Mvua za msimu katika maeneo hayo zinatarajiwa kuwa za wastani hadi
juu ya wastani.
Nyanda za juu Kaskazini Mashariki: (Mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara):
Mvua zinatarajiwa kuanza wiki ya kwanza ya mwezi Machi, 2012. Mvua hizo zinatarajiwa kuwa
za wastani hadi juu ya wastani.
Hata hivyo, baadhi ya maeneo yanayopata misimu miwili ya mvua yalipata mvua zisizo za
msimu katika wiki ya nne ya mwezi Februari, 2012 zilizosababishwa na kuwepo kwa matukio ya
vimbunga hafifu katika Bahari ya Hindi.
(ii) Mvua za Msimu
Kanda ya Magharibi (Mikoa ya Kigoma, Tabora na Rukwa ):
Mvua zinazoendelea katika maeneo haya zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani
isipokuwa maeneo ya mikoa ya Tabora na Rukwa-mashariki ambayo mvua zinatarajiwa kuwa
za wastani. Mvua hizi zinatarajiwa kuisha wiki ya nne ya mwezi Aprili, 2012.
Maeneo ya kusini (mikoa ya Ruvuma, Mtwara na Lindi)
Mvua zinaendelea katika maeneo haya na zinatarajiwa kuwa za wastani hadi chini ya wastani,
isipokuwa kaskazini mwa mkoa wa Lindi ambapo zinatarajiwa kuwa za wastani. Mvua hizi
zinatarajiwa kuisha mwishoni mwa wiki ya tatu ya mwezi Aprili, 2012.
Kanda ya kati (Mikoa ya Singida na Dodoma):
Mvua za wastani hadi juu ya wastani zinatarajiwa katika maeneo haya, isipokuwa mkoa wa
Singida ambao unatarajiwa kupata mvua za wastani. Msimu wa mvua unaendelea na unatarajiwa
kuisha wiki ya pili ya mwezi Aprili, 2012.
4
Nyanda za juu Kusini Magharibi: (Mikoa ya Mbeya, Iringa na Morogoro-kusini):
Mvua zinaendelea katika maeneo haya na zinatarajiwa kuwa za wastani, isipokuwa maeneo ya
kusini ya mkoa wa Iringa na Morogoro ambapo mvua za wastani hadi chini ya wastani
zinatarajiwa. Msimu wa mvua unatarajiwa kuisha mwishoni mwa mwezi Aprili, 2012.
Mwelekeo wa mvua uliotolewa hapa umezingatia zaidi kipindi cha msimu(miezi mitatu) na
hali ya mvua katika maeneo makubwa. Tofauti katika maeneo madogo madogo na mabadiliko
ya muda mfupi yanarajiwa. Vipindi vifupi vya mvua Kubwa ni matukio ya kawaida hata
katika maeneo yanayotarajiwa kuwa na upungufu wa mvua. Aidha vipindi virefu vya
upungufu wa mvua vinaweza kutokea hata katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za juu
ya wastani.
Mamlaka ya hali ya hewa Tanzania Itaendelea kufuatilia Mwenendo wa mifumo ya hali ya
hewa pamoja na vimbunga katika bahari ya Hindi na kutoa taarifa kuhusiana na mwelekeo
wa mvua nchini.
.
Kielelezo Matarajio na mwelekeo wa mvua za Masika na Msimu2012
3: USHAURI
5
Kilimo na Usalama wa Chakula
Maeneo mengi ya nchi yanatarajiwa kuwa na unyevu wa udongo wa kutosha isipokuwa maeneo
machache ya kusini mwa nchi ambapo upungufu wa unyevunyevu wa udongo unatarajiwa katika
mwezi Aprili, 2012. Maeneo yanayotarajiwa kupata mvua juu ya wastani, unyevunyevu wa
udongo kupita kiasi unaweza kuathiri maendeleo ya mazao hususani katika mashamba yaliyopo
mabondeni. Katika maeneo ya pwani ya kaskazini, nyanda za juu kaskazini-mashariki, ukanda
wa ziwa Victoria pamoja na magharibi (Kigoma) wakulima wanashauriwa kuendelea na taratibu
za kawaida za kilimo.
Maeneo ya magharibi (Tabora na Rukwa), maeneo ya kati, nyanda za juu kusini-magharibi
pamoja na maeneo ya kusini mwa nchi wakulima wanashauriwa kuendelea na shughuli za
kawaida za kilimo. wakati huu mazao yanapoelekea kukomaa. Aidha maeneo yanayopata msimu
mmoja wa mvua kwa mwaka yanaweza kunufaika kwa kuotesha mazao kama vile mihogo, na
mazao ya muda mfupi kama vile viazi vitamu na jamii ya mikunde. Mamlaka inawashauri
wakulima waendelee kutafuta na kufuata ushauri wa Maafisa Ugani katika maeneo yao.
Maji na Nishati
Vina vya maji katika maziwa, mabwawa na mito vinatarajiwa kuongezeka katika maeneo
yanayotarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani. Maeneo mengine yaliyosalia,
hayatarajiwi kuwa na ongezeko kubwa la vina vya maji.
Malisho ya mifugo
Hali ya malisho inatarajiwa kuwa nzuri katika maeneo mengi nchini. Wafugaji wanashauriwa
kuvuna na kuhifadhi malisho kwa matumizi wakati wa kiangazi. Hata hivyo wafugaji
wanashauriwa kuzingatia ushauri kutoka kwa maafisa mifugo katika maeneo yao.
Mamlaka za Miji
Mamlaka za miji katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu ya wstani,
zinashauriwa kusafisha mifumo ya maji taka ili kuepusha maji kutuama na kupunguza madhara
yatokanayo na mafuriko.
Sekta ya Afya
Maeneo yanayotarajiwa kuwa na mvua za wastani hadi juu ya wastani, kuna uwezekano wa
kutokea milipuko ya magonjwa ya malaria na kipindupindu. Mamlaka husika zinashauriwa
kuchukua tahadhari na maandalizi stahiki ili kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza.
Menejimenti ya Maafa
Taasisi za maafa na wadau husika, wanashauriwa kuchukua hatua muafaka za maandalizi ya
kukabiliana na majanga ya hali ya hewa yanayoweza kutokea.

Imetolewa na Dkt. Agnes L. Kijazi
MKURUGENZI MKUU,

MAMLAKA YA HALI YA HEWA TANZANIA (TMA)

MAM 2012 Statement_final _Swahili_

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *