Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imepanga kuwa Mei 28, 2018 itatoa uamuzi kama Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa JamiiForums, Maxence Melo na mwenzake wana kesi ya kujibu au la.
Uamuzi huo wa Mahakama ulitolewa jana Mei 22, 2018 jijini Dar es Salaam na Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama hiyo, Godfrey Mwambapa baada ya upande wa mashtaka kufunga ushahidi wao.
Katika kesi hiyo ya jinai namba 457/2016, Melo na mwanahisa wa mtandao huo, Micke William wanakabiliwa na shtaka la kushindwa kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi kwa kuzuia taarifa binafsi za wateja wao.
Kabla ya uamuzi wa mahakama, Wakili wa Serikali, Batilda Mushi alidai mahakamani hapo kuwa kesi hiyo imekuja kwa ajili ya uamuzi na kwamba wao wamefunga ushahidi.
Baada ya maelezo hayo, Hakimu Mwambapa ameahirisha kesi hiyo hadi, Mei 28 atakapotoa uamuzi dhidi ya Melo na mwenzake kama wana kesi ya kujibu au laa.
Tayari mashahidi wawili wa upande wa Jamhuri wameshatoa ushahidi wao mahakamani hapo dhidi ya washtakiwa.
Katika kesi ya msingi, Micke na Melo, wanadaiwa kuwa kati ya Mei 10 na Desemba 13,2016 , eneo la Mikocheni, wakiwa Wakurugenzi wa Jamii Media Co Ltd ambao unaendesha tovuti ya JamiiForums wakijua Jeshi la Polisi Tanzania linafanya uchunguzi kuhusiana na mawasiliano ya kimtandao yaliyochapishwa katika tovuti yao, walishindwa kutekeleza amri ya kutoa data walizonazo kwa nia ya kuzuia uchunguzi.
Chapisho hilo lilidai kuwa Kampuni za CUSNA Investment na Ocean Link ilikuwa inakwepa kodi bandarini, kuchonga nyaraka, kutorosha makontena na kunyanyasa wafanyakazi wa kitanzania. JamiiForums iliamini kuwa chapisho hilo lilikuwa halina nia mbaya ya kuichafua kampuni hiyo.
Katika kesi nyingine namba 458 inayohusu kuendesha mtandao wa Jamiiforums.com bila kutumia kikoa cha dot.TZ inayomkabili Maxence Melo na Micke William ilisikilizwa tena jana ambapo shahidi mwingine wa Jamhuri alitoa ushahidi wake mbele ya mahakama ambapo alidai kuwa mtandao huo unaendeshwa kwa kikoa cha dot.com na siyo dot.TZ.
Katika shauri hilo ambalo linasimamiwa na Hakimu Huruma Shahidi, upande wa Jamhuri uliwakilishwa na Wakili Batilda Mushi huku upande wa Watetezi ukiwakilishwa na Wakili Peter Kibatala akishirikiana na Jeremiah Mtobesya na Jebra Kambole
Shauri lilianza kusikilizwa kwa upande wa Jamhuri kumuongoza shahidi wao aliyejitambulisha kwa jina la Afande Peter Kayumbi.
Wakili wa Jamhuri, Batilda Mushi alianza kwa kumuuliza shahidi: Unafanya kazi wapi?
Shahidi: Nafanya kazi katika Ofisi ya upelelezi iliyopo Polisi central Dar
Wakili Batilda: Kazi yako hasa ni nini?
Shahidi: Kusikiliza watuhumiwa kupeleleza kesi na baadae kuja kutoa ushahidi Mahakamani
Wakili Batilda: Elimu yako umeipata wapi?
Shahidi: Elimu yangu nimeipata ndani na nje ya nchi na nina uzoefu wa karibu miaka 9 katika kazi yangu
Wakili Batilda: Elimu yako ulichukua ni juu ya nini hasa?
Shahidi: Elimu ya kuchukua vielelezo juu ya makosa ya mtandao na namna ya kupeleleza makosa ya mtandao
Wakili Batilda: Unakumbuka nini mnamo tarehe 14/12/2016?
Shahidi: Nilikuwa ofisini na niliitwa na Mkuu wangu ZCO, Wambura na nilipewa jalada la kesi lililokuwa linahusu kumiliki tovuti ambayo haijasajiliwa kwa kikoa cha .co.tz
Baada ya kupokea nilisoma jalada na kugundua kuwa watuhumiwa walikuwa Maxence Melo na Micke William
Wakili Batilda: Watuhumiwa hao unaweza kuonyesha Mahakama ni wepi?
Shahidi: Ndio (Huku akinyanyuka na kwenda kuwaonyesha watuhumiwa kwa Hakimu)
Wakili Batilda: Baada ya hapo ulifanya nini?
Shahidi: Baada ya kuwajua watuhumiwa, kwa kuwa Max alikuwa ameshakamatwa, tangu 14/12/2016 hivyo nilimuomba kwa ajili ya mahojiano. Baada ya kuongea nae aliniambia anaendesha tovuti aliyosajili tangu 2008 nchini Marekani kwa .com
Baada ya hapo juhudi za kumtafuta mwenzake Micke zilifanyika na Januari 16, 2017 naye alihojiwa
Wakili Batilda: Baada ya kuwahoji ulifanya nini shahidi?
Shahidi: Pia, niliandika barua kwenda tzNIC ili kupata taarifa kama tovuti ya JamiiForum imesajiliwa kwa kikoa cha .co.tz
Wakili Batilda: Uliandika wewe hiyo barua?
Shahidi: Mimi nili-draft na ikapitiwa na kiongozi wangu Bakari, alisaini na kunirudishia nami nikaituma
Wakili Batilda: tzNIC walijibu nini?
Shahidi: tzNIC walijibu kwanza JamiiForum waliisajili 2010 mara ya kwanza kwa kikoa cha .co.tz. mwaka 2013 iliondolewa na baadae mwezi Juni 2016 ikasajiliwa tena, ilisajiliwa tena kama Jamiiforum.co.tz isipokuwa alieleza kuwa haikuwa ikitumia kikoa hicho
Wakili Batilda: Uligundua nini katika upelelezi wako?
Shahidi: Niliandika barua BRELA kujua kama wamesajiliwa pale. Walijibu kuwa hakuna kitu kinaitwa Jamiiforum isipokuwa JamiiMedia na ndani ya JamiiMedia ndio kuna JamiiForum inafanya kazi
Pia, nilikusanya maelezo ya mashahidi ambao asilimia kubwa walikuwa wanatoka ofisi ya JamiiMedia iliyopo Kinondoni, Mikocheni. Na baadae niliandaa jalada kwa ajili ya kulipeleka ofisi ya Mwanasheria ili aweze kusoma na baadae kuitolea uamuzi
Wakili Batilda: Uligundua nini kama mpelelezi kwa taarifa kutoka tzNIC?
Shahidi: Nikitaka kujua kama Jamiiforum ilikuwa inaendeshwa kwa kikoa cha .co.tz na walijibu haiendeshwi kwa kikoa hicho bali JamiiForums.com ndio hasa niligundua hicho
Wakili Batilda: Ulihoji mashahidi ambao ni Wafanyakazi? Ulihoji akina nani na uliwahoji wapi?
Shahidi: Tulifika katika ofisi zao zilizopo Mikocheni, Kinondoni na kukuta zinafanya kazi na matangazo yanarushwa ambapo nilikuta kama wafanyakazi 7 hivi ambao wengi wao walikuwa ni Wahariri. Wahariri yaani Moderators
Wakili Batilda: Unamaanisha nini kwa kusema Moderators?
Shahidi: Kwa majibu yao ni kwamba wanachuja habari inapoingia kwenye mtandao wao kuona kama inaweza kwenda kwa jamii
Wakili Batilda: Unawakumbuka wafanyakazi hao kwa majina?
Shahidi: Siwezi kuwakumbuka wote kwa hakika ila kuna Asha, Deusdeus, na mwingine anaitwa Mdoe sijui
Wakili Batilda: Kingine ulichofanya juu ya jalada hili?
Shahidi: Niliandaa jalada la kwenda kwa Wakili wa Serikali
Wakili Batilda anamwambia Hakimu hana maswali ya ziada
Baada ya Wakili wa Jamhuri Batilda Mushi kumaliza kumuongoza shahidi wake, Hakimu anaruhusu upande wa utetezi kuanza kumhoji shahidi (Cross-examination). Wakili Peter Kibatala anaanza kumhoji shahidi.
Wakili Kibatala: Shahidi, Unafahamu mashitaka yanayowakabili washtakiwa?
Shahidi: Ndio
Wakili Kibatala: Naomba useme mashitaka yanayowakabili, yaani kama vile wizi au ujambazi kama hufahamu si shida tuendelee tusipoteze muda.
Shahidi: Ndio nafahamu, watuhumiwa wanashtakiwa kwa kuwa walikuwa wanaendesha tovuti ambayo haijasajiliwa kwa kikoa cha Tanzania
Wakili Kibatala: Kuna lingine?
Shahidi: Shitaka lilikuwa moja tu!
Wakili Kibatala: Kuna sehemu umesema Max wakati unamuhoji alikusimulia vitu fulani hivi, unakumbuka alikamatwa lini na muda gani?
Shahidi: Alikamatwa 14/12/2016 majira sikumbuki exactly
Wakili Kibatala: Ulimuhoji saa ngapi?
Shahidi: Max hakuhojiwa na mimi
Wakili Kibatala: Haya uliyosimulia vipi? Ni hear-say? Alitoa kisheria au mlikuwa sehemu mnapiga tu story?
Shahidi: Yapo kisheria
Wakili Kibatala: Hiyo statement uliyosema ulitoa wewe?
Shahidi: Hapana
Wakili Kibatala: Ulishuhudia ikiandikwa?
Shahidi: Hapana
Wakili Kibatala: Kwa hiyo ni hear-say? Umeitoa kama kielelezo Mahakamani?
Shahidi: Hapana sijatoa
Wakili Kibatala: Nimesikia umeandika barua kwenda tzNIC na BRELA umezitoa kama ushahidi?
Shahidi: Hapana
Wakili Kibatala: Unasema BRELA walikujibu vitu viwili vitatu, hayo majibu umetoa kama kielelezo?
Shahidi: Hapana
Wakili Kibatala: Nimesikia umesema pia tzNIC walikujibu, ulitoa kama kielelezo?
Shahidi: Hapana
Wakili Kibatala: Nani alikuwa muhifadhi(Custodian) wa hizi barua?
Shahidi: Sikuwa mimi
Wakili Kibatala: Hati ya mashtaka inadai kwamba Maxence Melo Mubyazi mshitakiwa wa kwanza na Micke William mshitakiwa wa pili kuwa kama directors (Wakurugenzi) wa JamiiForum. Uliwahi kutapa barua ya kielelezo cha directorship? (kurugenzi)
Shahidi: Ndio nilishapata
Wakili Kibatala: Unafahamu kama mpelelezi au ulishafanyia kazi tofauti ya JamiiForum na JamiiForums?
Shahidi: Hapana
Wakili Kibatala anaomba na kupewa Exhibit D1 kutoka kwa Hakimu Huruma Shaidi. Kisha anampa shahidi na kumuuliza kama alishawahi kukiona na kukifanyia kazi
Shahidi anajibu kuwa hajawahi kukiona wala kukifanyia kazi
Wakili Kibatala: Kwa kukiona unafahamu ni nini?
Shahidi: Mpaka nisome (Kibatala anampa asome). Shahidi anaendelea kwa kusoma kwa haraka haraka inajaribu kuelezea kuhusu JamiiForum
Wakili Kibatala: Na kuwa imesajiliwa sio?
Shahidi: Ndio
Wakili Kibatala: Kutoka kwenye Exhibit D1, Unahafamu Maxence na Micke wana uhusiano gani kati Maxence na Micke na taarifa ya usajili?
Shahidi: Sitaki kuzungumzia Exhibit D1 Kwa sababu sikifahamu
Wakili Kibatala: Hati ya mashitaka inasema hivi Maxence Melo aliendesha Forum ambayo haijasajiliwa wa kikoa cha do.tz. Je, wewe unakifahamu hicho kitu?
Shahidi: Ndio, nakifahamu
Wakili Kibatala: Umetolea ushahidi hiki kitu do.tz?
Shahidi: Hapana (Wakili Kibatala anajisemesha “Sasa kama unatoa ushahidi kitu ambacho hakipo kwenye hati, nakosa hata cha kukuuliza.”)
Wakili Kibatala: Mhe. Hakimu sina maswali zaidi
Baada ya Wakili Kibatala kumaliza kumuhoji shahidi Hakimu anauliza upande wa Utetezi kama wana maswali ya ziada, Wakili Jebra Kambole anasema anayo
Hakimu anaruhusu Wakili Kambole kumhoji shahidi
Wakili Kambole: Shahidi umesema JamiiForums imesajiliwa kwa .co.tz lakini ukasema kilikuwa hakitumiki?
Shahidi: Ndio
Wakili Kambole: Umetoa ushahidi hapa Mahakamani kwamba hakitumiki?
Shahidi: Ndio, kwa maelezo ya shahidi aliyepita
Wakili Kambole: Nakuuliza wewe sio shahidi aliyepita
Shahidi: Sijatoa kielelezo chochote mimi
Wakili Kambole anamaliza na kusema hana maswali ya ziada. Wakili Jeremiah Mtobesya anapewa muda wa kumhoji na anaanza kumuuliza shahidi
Wakili Mtobesya: Shahidi kwa sababu umekuja kama mpelelezi, ni nani ana-draft kosa ambalo linapelekea upelelezi?
Shahidi: CRO-Sehemu ya kupokea taarifa
Wakili Mtobesya: Hivyo wewe unapeleleza jalada kutoka CRO?
Shahidi: Kama mpelelezi unapewa jalada lililofunguliwa na unaanza kufanya kazi kwa jalada ulilopewa
Wakili Mtobesya anasema hana Maswali zaidi
Baada ya upande wa utetezi kusema wamemaliza kuuliza maswali yao Hakimu Shahidi anauambia upande wa Jamhuri kumalizia kama wana maswali.
Wakili wa Jamhuri Batilda Mushi anarejea tena kumuongoza shahidi(Re-examination)
Wakili Batilda: Shahidi jukumu lako kama mpelelezi katika kesi hii lilikuwa ni nini?
Shahidi: Jukumu langu kubwa ni kuthibitisha kosa lilikokuwa linalalamikiwa
Wakili Batilda: Katika kuthibitisha huko ulifanya nini?
Shahidi: Kwa jibu watakalokupa tzNIC ndio litakuwa la kuanzia katika upelelezi
Wakili Batilda Mushi: Wewe uligundua nini katika upepelezi wako?
Shahidi: Kwanza tzNIC hawakuwa na ubishi kuwa hawa watu hawajajisajili, wamejisajili lakini walikuwa hawatumii kikoa cha .tz (dottizii)
Wakili Mtobesya anaomba kuongea na kuruhusiwa na kusema “Shahidi ni kama anajaribu kuziba majibu ya awali sasa anasema .tz(dottizii). Awali hakusema hivi
Hakimu Shaidi: Anauliza upande wa Jamhuri “But this is a new issue?” (Lakini hili ni jambo jipya?)
Batilida na Shahidi: Hapana. Ilikuwa hivi toka mwanzo.
Hakimu Shaidi: Okay, tuendelee maana mimi mwenyewe si ninaweka rekodi hapa na ninajiamini.
Wakili Batilda: Shahidi wewe una-draft mashtaka?
Shahidi: Hapana
Wakili Batilda: Nani anafanya hivyo?
Shahidi: Ofisi ya Mwanasheria wa Serikali
Wakili Batilda anasema amemaliza kuuliza maswali
Hakimu, Shaidi: Anauliza upande wa Jamhuri “Mna shahidi mwingine?”
Wakili Batilda: Hapana
Hakimu, Shahidi: Mnafunga?
Wakili Batilda: Hapana tunaomba kuahirisha
Hakimu anauliza wote, Mnataka tarehe ngapi? Wakili Peter Kibatala anaomba mbele ya tarehe 12/06/2018
Hakimu Shaidi: Tarehe 18 Juni?
Wote (Upande wa Utetezi na Jamhuri): Sawa
Wakili Kibatala anaomba kwa Hakimu kuwa upande wa Jamhuri ukija siku hiyo waje na shahidi zaidi ya mmoja. Hakimu anaridhia na kuuliza upande wa Jamhuri kama wamesikia ombi la Utetezi na upande wa Jamhuri unasema sawa na anaihirisha shauri hadi hadi Juni 18, 2018.
Kufahamu kwa undani mwenendo wa kesi 3 zinazoikabili JamiiForums pitia hapa