KUNA kipindi maisha humuongoza binadamu afanye nini ili aweze kuishi kulingana na mazingira anayoishi. Hivyo ndivyo ilivyo kwa baadhi ya vijana na kinamama wanaoishi katika vijiji vya Sambaru, wilaya ya Ikungi na Londoni, wilaya ya Manyoni.
Kila siku vijana na kinamama hao huamkia katika maeneo yaliyokuwa yakichimbwa dhahabu, siku za nyuma, na wachimbaji wadogo ambayo hivi sasa yanamilikiwa na kampuni ya Lake Victoria Resources.
Katika maeneo hayo, watu hao hukusanya mabaki ya mawe madogo na vumbi la mchanga kwa ajili ya kusafisha ili wapate dhahabu; wauze.
Kwa mujibu wa wenyeji, maeneo hayo awali yalikuwa yanamilikiwa na wachimbaji wadogo, lakini hivi sasa yako chini ya ulinzi wa walinzi wa kampuni hiyo ambao kabla ya kuingia na kuanza kukusanya mchanga au mawe, watu hao hutoa ‘kitu kidogo’ ili waruhusiwe.
Kijana akikusanya mchanga wa dhahabu, Sambaru, wilayani Ikungi
Kutokana na hali hiyo, makumi ya watu – hususan vijana na kinamama huingia sehemu hizo ambazo miaka mitano iliyopita zilikuwa zinazalisha dhahabu kwa wingi. Tangu kampuni hiyo ilipochukua umiliki wa maeneo hayo, mwaka 2010 haijaanza uzalishaji.
Hata hivyo, kwa vijana na kinamama wanaolazimika kutoa hongo ya sh. 10,000 kwa siku ili waruhusiwe kuingia sehemu hizo, wanaomba Lake Victoria Resources iendelee kuvuta pumzi wakati wao wanaendelea kuendesha maisha kupitia eneo hilo.
Vijana wakikusanya vipande vya mawe katika eneo lililokuwa likichimbwa dhahabu, Sambaru, wilayani Ikungi
“Japokuwa tunapata kiasi kidogo cha fedha, lakini hawa jamaa wakiendelea kuchelewa na sisi tutaendelea kupata angalau mkate wetu wa kila siku, “anasema mmoja wao ambaye ni kijana kwa sharti la kutotaja jina lake.
Kijana huyo anasema, kwa siku hawezi kukosa faida ya sh. 5,000 au zaidi baada ya kutoa gharama mbalimbali kabla hajapata dhahabu. Gharama hizo ni zile zinazohusiana na kusaga mawe, uoshaji mchanga na uchenjuaji wa udongo.