Somo la TEHAMA na wanafunzi wa vijijini

Albano Midelo

WALIMU wanaofundisha katika mazingira magumu wamedai kuwa somo la Teknolojia ya Habari na Mawasiliano TEHAMA linawabagua  wanafunzi wa vijijini.

Walimu hao wamedai kuwa licha ya wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kuanzisha somo hilo, mazingira yao hayaruhusu  kufundishwa somo hilo kwa uhakika katika shule za msingi na sekondari.

Beston Mwambene ni mwalimu wa shule ya msingi Ihovyo iliyopo katika kata ya Totowe wilayani Chunya anasema TEHAMA ni somo jipya ambalo limefanya Dunia kuwa kijiji kimoja,hata hivyo alisema wanafunzi wa vijijini  wapo nje ya kijiji  kutokana na mazingira magumu.

Mwambene anasema  licha ya umuhimu wa somo hilo katika ulimwengu wa sasa,walimu wengi katika maeneo ya vijijini inawawia vigumu kufundisha mada za somo la TEHAMA kama vile mada ya kompyuta kutokana na ukweli kuwa mwalimu mwenyewe hajawahi kutumia kompyuta.

“Katika kitabu cha TEHAMA darasa la saba kuna mada   kama vile mtandao wa ndani wa kompyuta,mtandao wa intaneti,kutumia tovuti,maana ya baruapepe,hebu niambie mwalimu wa kijijini kama hapa hata baruapepe anaisikia kwenye vyombo vya habari halafu unamwambia afundishe wanafunzi,ni jambo ambalo haliwezekani’’,anasisitiza Mwambene.

Mwembene anaishauri serikali kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kwanza kutoa elimu ya TEHAMA kwa walimu ambao watakuja kuwafundisha wanafunzi mada hizo ili wajengewe uwezo katika somo hilo ni muhimu kutokana na mabadiliko ya teknolojia ya mawasiliano duniani kuathiri Nyanja mbalimbali za maisha .

picha inamuonesha mwalimu mkuu wa shule ya msingi Ihovyo Beston Mwambene akionesha changamoto za somo la TEHAMA kwa wanafunzi na walimu wa vijijini

Hata hivyo alisema katika maeneo ya vijijini bado inaonekana kuwa elimu ya TEHAMA ina ubaguzi kwa kuwa  somo la kompyuta haliwezi kufundishwa kwa nadharia badala yake wanafunzi wa vijijini wanatakiwa kujifunza kwa vitendo  ili nao wawe na ubora kama ilivyo kwa wanafunzi  wa shule za msingi na sekondari katika maeneo ya mijini.

“Hatuwezi kufanya maigizo ya kufundisha somo la kompyuta kwa kuchora ubaoni halafu  ukadhani mtoto ameelewa bila kuona kompyuta halisi au ukawaambia mashine ya mahesabu ni jamii ya kompyuta,elimu hii inakwenda na ubaguzi kwa kuwa wanafunzi wa shule za vijijini   watapata shida ukilinganisha na shule za mijini ambao wamezoea kuiona kompyuta pamoja na kuitumia’’,anasisitiza.

Agustino Mlekani ni mwalimu shule ya msingi Namambo kata ya Totowe wilayani Chunya anasema changamoto iliyopo  kwa serikali ni kuhakikisha kuwa nishati ya umeme inakwenda hadi vijijini  ili  wanafunzi waweze kujifunza somo la TEHAMA kwa nadharia na vitendo .

“Tupo katika ulimwengu wa Sayansi na Teknolojia lakini tumefikaje hapa,sisi wengine wa vijijini tunakuwa kama wasindikizaji tu kwa kuwa hatuna vifaa vya kujifunzia na kufundishia katika somo la TEHAMA, wizara ya elimu ilitakiwa iandae mafunzo ya muda mfupi kwa walimu wa vijijini ambao watafundisha somo ya TEHAMA’’,anasema.

Katika kukabiliana na changamoto ya ufundishaji wa somo la TEHAMA katika shule za msingi na sekondari katika jimbo la Songwe Chunya ,mbunge wa jimbo hilo ambaye pia ni Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Philipo Mlugo hivi karibuni ametoa  kompyuta za mkononi (laptop) 40 zenye thamani ya shilingi milioni 48 kwa ajili ya walimu wanaofundisha masomo ya Sayansi katika shule  sekondari pamoja na waratibu elimu kata jimboni mwake .

Mlugo amebainisha lengo la kutoa kompyuta hizo katika shule za sekondari  jimboni mwake ni kuhakikisha kuwa walimu wa masomo ya Sayansi  wanakwenda sanjari na mabadiliko ya teknolojia ya habari na mawasiliano ulimwenguni ambayo yamefanya dunia kuwa kijiji kimoja.

Mabadiliko ya  Teknolojia ya Habari na Mawasiliano Duniani yameathiri Nyanja mbalimbali za maisha kiuchumi, kisiasa, kijamii na kiutamaduni.Hali hii imeleta ushindani katika shughuli za kila siku na kusababisha mabadiliko makubwa kiuchumi.

Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Tanzania iliamua kuanzisha somo la Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kwa elimu ya msingi na Sekondari nchini,kutokana na  TEHAMA  kuifanya Dunia kuwa kama kijiji kimoja.

TEHAMA inampa mwanafunzi maarifa na stadi za matumizi ya habari,vyombo vya mawasiliano,maktaba na kompyuta na kwamba ufundishaji wa somo hilo unahitaji mwalimu kujifunza kila wakati ili aweze kukabiliana na mabadiliko ya teknolojia ya mara kwa mara.

Mwongozo wa wizara ya elimu na mafunzi ya ufundi kwa mwalimu anayefundisha somo la TEHAMA  wa mwaka 2007 unamtaka mwalimu kuutumia vyema mwongozo huo ambao utamwezesha kumjengea mwanafunzi maarifa na stadi za matumizi ya vyombo vya mawasiliano kama vile maktaba, kompyuta,redio,luninga na magazeti kulingana na mada zilizopo kwenye muhtasari.

 

 

 

1 Comment
  • si kweli somo la tehama haliwezekani kufundishwa vijijini ni ubunifu wa walimu kuwa haba wanaweza wa kafaragua zana za kufundishia kingine tehama mawazo ya wengi ni kompyuta si kweli kompyuta ni sehemu tu tehama

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *