Majambazi wa DRC waua polisi wa Tanzania ziwani, JWTZ wajeruhiwa

Jamii Africa

ASKARI mmoja wa Tanzania amepoteza maisha baada ya kutokea mapigano katikati ya Ziwa Tanganyika kati ya majambazi yenye silaha toka nchi jirani na askari wa Tanzania wakiwamo polisi na wanajeshi wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).

Taarifa zilizoripotiwa katika mtandao wa JamiiForums.com na kuthibitishwa na polisi zimeeleza kwamba askari wa Tanzania akiwamo Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya ya Kigoma Mohamed Kilonzo, walikwenda kumuokoa Mtanzania aliyetekwa na majambazi hayo na kutokea mapigano hayo.

Katika tukio hilo majambazi wote sita waliuwawa na askari mmoja wa Tanzania alifariki kutokana na majeraha makubwa wakati wengine sita wakiwamo askari wa JWTZ walijeruhiwa baadhi yao vibaya sana.

Kamanda wa Polisi Mkoani Kigoma Frassa Kashai, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuahidi kulitolea taarifa tukio hilo baadaye, kwa kuwa wakati huo walikuwa wakishughulikia suala hilo ikiwa ni pamoja na kuwahudumia majeruhi na kufuatilia usalama wa eneo hilo.

Taarifa katika mtandao wa JamiiForums.com zilizotumwa na mwanachama wa mtandaoa huo mwenye jina la KAUMZA zilieleza;
“Leo mchana kumetokea mapigano makali kati ya askari wa jeshi la polisi na JWTZ kwa upande mmoja na majambazi kutoka Congo (DRC). Katika mapigano hayo Oc-cid wa Kigoma bwana Mohamed Kilonzo amepigwa risasi kifuani pamoja na askari polisi mwingine amepigwa risasi ya shingo. Kwa upande wa JWTZ, askari mmoja kavunjwa miguu, mwingine risasi imeingia kiunoni na mwingine kapigwa mkononi.

“Hadi ninapoleta taarifa hii, majeruhi wapo theatre takribani masaa manne sasa na madaktari wanaendelea kufanya jitihada za kuwasaidia. Na kwa upande wa adui, habari zilizopo ni kuwa wote wameuawa. Chanzo cha tukio hili ni kuwa majambazi hao kutoka Congo kumteka raia wa Tanzania na askari wetu kutaka kumuokoa. Tuombe Mungu awaponye”

Taarifa zaidi tutaendelea kuwaletea huku ukifuatilia: Mapigano katika Ziwa Tanganyika

10 Comments
  • Hii sio haki wala Ushujaa wageni wanaingia nakafanya watakacho kanakwamba hili ni shamba la Bibi? hebu vyombo vyenye dhamana viwe makini na mambo kama haya kwani Mchelea mwana kulea hulia Mwenyewe leo wameingia Kigoma, kesho wataingia Sirali, Kesho kutwa wataingia, Upande wa kusini na siku nyingine Isibania na kadhalika.

    Ni hayo tu ndugu zangu Tz isigeuzwe Jamvi la Wageni.

  • Zamani wakati wa Nyerere kulikuwepo na Marine force. Inaelekea Law Enforcement katika Lake Tanganyika wamesahauliwa. Tafadhali bwana muandishi fualitilia hii habari ni muhimu sana. Nasikitika kwa mashujaa waliopoteza maisha na waliopata majeruhi.

  • BWana ee..! kila siku majambaz wa Kongo, Rwanda na Burundi, wengine ni sisi tunawalea mitaani et kwamba wa Tz wana upendo, mwishowe wanatuvunja miguu na kutuua kila siku. lazima tujenge utamaduni wa kuwahoji wageni. kila pembe ya nchi wamejaa tu.

  • mwenyezi yupo pamoja nao kwani walikuwa wanalitetea taifa letu pamoja na kwamba kuna watu wachache ndio wanaofaidi keki ya taifa hili get well soon to all kamanda.

  • Hii inasikitisha sana, mgeni anaingia na kufanya atakavyo nchini mwetu. Namsihi Mwena aanzishe operation maalum kupambana na wahalifu hawa mipakani. Pongezi sana makamanda kwa kazi mlioifanya kutetea taifa letu na Mungu azilaze roho za makamanda wetu waliouwawa mahali pema peponi. Amina.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *