Mamlaka ya Dawa yadai haijui athari za dawa feki

Jamii Africa

MAMLAKA ya Chakula na Dawa nchini (TFDA), imesema haijui ukubwa wa tatizo na athari za dawa feki zinazoingizwa na kusambazwa kwa ajili ya matumizi ya binadamu katika maeneo tofauti hapa Tanzania.

Pamoja na hayo, TFDA imekiri kuwepo kwa dawa nyingi feki zinazoingizwa na kusambazwa hapa nchini ikiwemo mikoa ya Kanda ya Ziwa, na kwamba kazi ya ukaguzi ambayo imekuwa ikifanywa na mamlaka hiyo bado inakabiliwa na changamoto kubwa, kutokana na baadhi ya watu wasio waaminifu kuendelea kufanya biashara hiyo haramu.

Mkurugenzi wa Mamlaka ya Chakula na Dwa nchini (TFDA), Hiiti Sillo (kulia), akiwaonesha waandishi wa habari miongoni mwa kopo la dawa feki walizozikamata. Wa pili kulia ni Kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza, Libelatus Barlow akifuatilia taarifa  za TFDA katika kikao kilichofanyika leo jijini Mwanza

Kauli hiyo imetolewa leo jijini Mwanza na Mkurugenzi Mkuu wa TFDA, Hiiti Sillo, wakati alipokuwa akizungumza katika kikao cha pamoja baina ya Mamlaka hiyo, waandishi wa habari na Jeshi la polisi, kuhusiana na oparesheni ya kukamata dawa bandia iliyofanyika Kanda ya Ziwa.

Mkurugenzi huyo wa TFDA, Sillo alisema mamlaka yake haina takwimu sahihi zinazobainisha ukubwa wa tatizo na athari zinazowapata wananchi punde wanapotumia dawa hizo bandia, zinazodaiwa kuingizwa kwa wingi kutoka nje ya nchi.

“Hatuna takwimu sahihi kuhusu ukubwa wa tatizo hili. Wala hatujui ni idadi ya watu wangapi walioweza kuathirika ama kukumbwa na vifo kutokana na kutumia dawa hizi feki.

“TFDA tumejikita kufanya ukaguzi wa kuwakamata wauzaji na wasafirishaji wa dawa bandia. Tumefanya oparesheni kali sana Kanda ya Ziwa kuanzia Machi na Juni mwaka huu, na tumeweza kukamata dawa nyingi za bandia”, alisema Mkurugenzi huyo TFDA, Sillo.

Akizungumzia dawa zilizokamatwa katika msako huo uliohusisha vyombo vya dola, Sillo alisema kwamba dawa nyingi zimekamatwa katika nyumba za kulala wageni (Guest House), duka za dawa baridi, vituo vya kuuzia simu, stationary, stoo na vituo vya mabasi makubwa yaendeyo mikoani.

Kufuatia na kuonekana kushamiri kwa tatizo hilo, Mkurugenzi huyo wa TFDA aliiomba jamii kushirikiana na mamlaka hiyo pamoja na vyombo vya dola kwa kutoa taarifa juu ya watu wanaouza dawa bandia, na kwamba kufanya hivyo itasaidia maradufu kudhibiti uingizwaji na usambazwaji wa dawa hizo zenye hatari katika afya ya binadamu.

Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi mkoani Mwanza, Liberatus Barlow (RPC), alisema jeshi lake lipo makini kwa kuwakamata watu wote wanaokutwa na dawa hizo feki, na kwamba zaidi ya watu 13 wamekamatwa kwa muda mfupi na polisi kisha kufunguliwa mashtaka mahakamani.

Kamanda Barlow alieleza kusikitishwa kwake na taarifa za kuwepo kwa baadhi ya watu kutumia mabasi ya abiria kusafirisha dawa hizo feki kutoka mpakani Tunduma Mbeya kisha kuzipeleka Dar es Salaam na Mombasa nchini Kenya, na kwamba kamwe jeshi lake mkoani hapa halitawafumbia macho wahalifu hao.

Habari hii imeandikwa na Sitta Tumma – FikraPevu, Mwanza

4 Comments
  • Nashangaa sana TFDA kusema kwamba hawajui ukubwa wa tatizo la dawa feki na athari zake kwa wananchi.Nashangaa pia wao kusema kwamba tatizo hili liko zaidi kanda ya ziwa.Tatizo hili liko mikoa yote.Hawa jamaa ni wasomi uchwara sana.Niwaelimishe TFDA kwamba dawa zote ziko made to kill in the long term.This is deliberately done.They are only made to cure in the short term ili tusistuke,ni danganya toto tu.Hii added problem ya u-fake is meant kuharakisha mauaji.Si rahisi kujua idadi ya ya watu ambao wameshakufa kwa sababu ya kutumia dawa fake,shughli nzima is very inteligently done,lakini kwa mtu mwenye ufahamu wa athari ya matumizi ya dawa zenye sub-optimal active ingredients,atakubaliana na mimi kwamba hali ni mbaya.Tabia ya TFDA mara kwa mara kutokiri kwamba tatizo ni kubwa,na kutokuwa tayari kufanya uchunguzi wa kina kuhusu tatizo hili, inatufanya tuamini kwamba they are collaborators katika conspiracy ya kuangamiza kizazi hiki.

  • mnataka kuniambia TFDA hawana taaluma ya kutosha,au hawajiamini na taaluma yao,au ndo walewale? wasije wakatumaliza hao maana yake nchi hii siku hizi mh

  • Ni hatari sana kwa Wataalam wa TFDA kushindwa kujua ukubwa wa athari ya dawa feki kwani nyinyi ndio tunaoweza kusema tunawategemea kutuelimisha zaidi juu ya hizi athari
    kwa Wananchi wa kawaida.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *