Maofisa Ugani: Kada muhimu sekta ya kilimo inayosahaulika. Ni wachache na hawana vitendea kazi

Jamii Africa

MAOFISA ugani ni miongoni mwa kada ya uongozi na wataalam wanaonyooshewa vidole kuwa chanzo cha kuzorota kwa kilimo chenye tija kwenye mazao ya chakula na biashara, pamba ikiwemo, FikraPevu inaripoti.

Licha ya kuajiri robo tatu ya Watanzania zaidi ya 20 milioni wenye uwezo wa kufanya kazi, mchango wa sekta hiyo bado hauridhishi kutokana na sababu kadhaa.

FikraPevu inafahamu kwamba, moja ni kuendeleza kilimo cha utamaduni ambacho siyo tu kinategemea misimu ya mvua, bali kinatumia zana duni na matumizi hafifu ya elimu na pembejeo za kisasa.

Zipo sababu kadhaa zinazosababisha wakulima wengi kuendeleza kilimo cha utamaduni, kubwa ni kukosa ushauri wa kitaalam kutoka kwa Maofisa Ugani wakati wa maandalizi ya shamba, uchaguzi na ununuzi wa mbegu, kupanda, matumizi sahihi ya pembejeo na uvunaji.

Lawama nyingi kuhusu kukosekana huduma ya ugani huelekezwa kwa maofisa ugani ambao wanatuhumiwa kukaa maofisini badala ya kuwatembelea wakulima mashambani.

Hata hivyo, uchunguzi wa kina wa FikraPevu uliohusisha mahojiano na wakulima, Maofisa Ugani, viongozi na watendaji katika ngazi ya vijiji, kata na wilaya unagundua kuwa kitendo cha wakulima kukosa ushauri wa kitaalam kuhusu kilimo chenye tija kina makandokando mengi zaidi ya lawama za Maofisa Ugani kutofika vijijini.

Kwanza, kada hiyo ni kati ya watumishi wa umma ambao idadi yao haitoshelezi wala kulingana na mahitaji halisi. Ni wachache!

Licha ya uchache wao, kada hiyo ya Maofisa Ugani pia imetelekezwa siyo tu kimaslahi, bali hata kwa kutopatiwa nyenzo na vitendea kazi kuwawezesha kutekeleza wajibu wao.

Hii inadhihirishwa na ukweli kwamba licha ya kuhitajika kupatikana angalau Ofisa Ugani mmoja kwa kila kijiji (kama siyo kila kitongoji kwa maeneo makubwa kiutawala), kada hiyo hivi sasa wanapatikana kwenye ngazi ya kata.

Hata baadhi ya kata hazina huduma ya Maofisa hao kiasi kwamba walioko kata jirani kulazimika kuhudumia kata nyingine.

Baadhi ya maofisa hao hulazimika kuhudumia vijiji hadi 10 kwa Kata moja au zaidi, huku wakitembea zaidi ya kilometa 10 kwenda na kurudi kuhudumia wakulima.

 

Maofisa ugani hawataki kuishi vijini kuhudumia wakulima?

“La hasha! Tunapenda na hakika ndiyo furaha na fahari yetu kwa sababu huko ndiko tunakoonyesha ujuzi na uwezo wetu. Tungependa kuishi na wakulima vijijini ambako ndiko fani yetu inahusika,” anaanza kujibu swali hilo Ofisa Ugani wa Kata ya Malya, Wilaya ya Kwimba, mkoani Mwanza, Hamisi H. Mzee.

Kuhusu lawama kwamba wanashindwa kuwatembelea wakulima, Mzee anasema: “Wengi wetu hatuwezeshwi. Siyo tu kwa usafiri wa kuwafikia wakulima, bali hata kwa motisha ya kufanya hivyo.”

Anasema wapo Maofisa Ugani wanaolazimika kutembea kwa miguu umbali wa zaidi ya kilometa 10 kwenda na kurudi kila siku kuwatembelea na kuwashauri wakulima ili kuongeza tija kwenye kilimo.

“Baadhi kama mimi niliyemudu kununua pikipiki yangu binafsi tunamudu kuwatembelea wakulima. Tena kwa gharama zetu kuanzia mafuta na matengenezo ya chombo,” anasema Mzee akionyesha pikipiki yake aliyoinunua miaka sita iliyopita.

Anamshukuru Mkuu wa Wilaya ya Kwimba, Mtemi Msafiri, kwa kuunda Kikosi Kazi Maalum kuhamasisha kilimo cha pamba, na kufanikisha upatikanaji wa pikipiki kutoka kwa makampuni ya pembejeo ambazo zimegawanywa kwa Maofisa Ugani.

“Kwa juhudi za Mkuu wa Wilaya tumewezeshwa angalau lita 36 za mafuta kufanikisha shughuli za uhamasishaji wakati wa maandalizi ya mashamba, kilimo na upandaji wa pamba,” anasema Mzee katika mahojiano na FikraPevu.

Anasema msimu huu, Maofisa Ugani kwa kushirikiana na Kikosi Kazi Maalum kuanzia ngazi ya Wilaya, Kata na Vijiji wamefanikisha kurejesha ari ya kilimo cha pamba wilayani Kwimba.

“Kata yangu ya Malya pekee tumelima zaidi ya ekari 748.5 za pamba kutokana na uhamasishaji wa Vikosi Kazi kuanzia ngazi vijiji, kata hadi wilaya,” anasema.

Hata hivyo, ni ekari 369 pekee ndizo zilizoota, wakati 322 hazikuota kutokana na changamoto ya mbegu na mvua zisizoridhisha, na ekari 46 hazikupandwa kabisa baada ya mvua kukatika mapema.

Licha ya kuhamasishwa, baadhi ya wakulima pia waliamua kugeukia mazao mengine kama choroko, dengu, alizeti, mpunga na mahindi.

 

Pikipiki kwa maofisa maofisini badala ya Maofisa Ugani

Akizungumzia kwa sharti la kutotajwa jina, mmoja wa wataalam katika Idara ya Kilimo wilayani Kwimba anashauri pikipiki zilizogawanywa kwa maofisa walioko Makao Makuu ya Halmashauri zipelekwe vijijini kwa maofisa ugani ili kuongeza huduma kwa wakulima.

“Pikipiki zina uwezo wa kuhimili mazingira ya vijijini zisitumike kama usafiri wa kwenda na kurudi kazini kwa maofisa. Zitaleta tija zikipelekwa vijijini kukuza sekta ya kilimo kupitia huduma ya ugani kwa wakulima,” anashauri mtaalam huyo.

 

Upangaji wa bei, gharama za uzalishaji

“Bei ya kununua pamba izingatie gharama halisi ya uzalishaji. Hii siyo tu itawapa pato la uhakika wakulima, bali pia itaongeza ari wengi kulima pamba,” hiyo ni kauli ya Mkulima Mshauri kutoka Kijiji cha Kiliaboya, Ngulimi John.

Anapendekeza bei ya sasa ya msimu uliopita ya Shs. 1, 000 kwa kilo iongezeka angalau hadi kufikia Shs. 1, 200 kwa kilo kutokana na kupanda kwa gharama za kilimo kuanzia kwenye mbegu na viuadudu.

Akijibu hoja kuhusu bei, Mkaguzi wa Pamba Wilaya ya Kwimba kutoka Bodi ya Pamba nchini (TCB), Penina Range, anasema upangaji wa bei ya kununulia pamba hutegemea mambo kadhaa, bei ya soko la dunia na nguvu ya shilingi ikiwemo.

Kwa wastani, gharama ya kuzalisha kilo moja ya pamba ni kati ya Shs. 500 hadi Shs. 600, sawa na Shs. 300, 000 kwa ekari moja kulingana na upatikanaji wa pembejeo, usimamizi na uzingatiaji wa kanuni na mahitaji ya kitaalam pamoja na umbali anakotoka mkulima.

 

Kusimamia malengo, na kubadilishana uzoefu

Miongoni mwa changamoto zinazokwamisha maendeleo ya sekta ya kilimo cha pamba ni kukosekana kwa usimamizi wa malengo kwa serikali na wadau kubadilisha taratibu hata katikati ya msimu.

“Msimu huu tumeanza kuona mafanikio baada ya serikali na wadau wa pamba kusimamia malengo ya kutumia dirisha moja kuanzia kwenye upatikanaji na usambazaji wa mbegu pamoja na ununuzi,” anasema Ofisa Ugani wa Kata ya Malya, Hamisi H. Mzee.

Kupitia mfumo wa dirisha moja, kazi ya kupokea, kugawa mbegu na ununuzi wa pamba hufanywa na Kikosi Kazi cha Kijiji husika (Village Task Force, VTF), inayoongozwa na mkulima maarufu kama Mwenyekiti, Mtendaji wa Kijiji, wagani kazi, maofisa ugani na wakulima ambao ni wajumbe.

Kikosi Kazi pia kimeundwa katika ngazi ya kata na wilaya kikiwa na jukumu la kuhamasisha, kusimamia, kuelekeza na kutekeleza malengo ya kilimo chenye tija cha zao la pamba.

Kutokana na kutofautiana kwa mazingira na changamoto za kazi, Mzee anashauri pawepo utaratibu wa Maofisa Ugani, wataalam wa kilimo, wakulima pamoja na wadau wengine wa zao la pamba kukutana mara kwa mara kubadilishana uzoefu na kuzitafutia ufumbuzi wa pamoja changamoto zinazokwamisha maendeleo ya sekta hiyo.

Makala haya yataendelea……..

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *