Mapanga ya wabunge wa Chadema, polisi yakamata 15

Jamii Africa

JESHI la Polisi Mkoani Mwanza, limewakamata watu 15 wanaosadikiwa kuwakata mapanga wabunge wawili wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Highness Kiwia (Ilemela), na Salvatori Machemli (Ukerewe), na kusema kwamba upo ulazima wa kuhojiwa wabunge hao ili polisi wapate taarifa sahihi juu ya suala hilo zito.

Kamanda wa Pilisi Mkoani Mwanza, Liberatus Barlow akisisitiza jambo kwa waandishi wa habari leo ofisini kwake. (Picha na Sitta Tumma).

Polisi imesema, kazi ya kuwahoji watuhumiwa hao 15 inaendelea na kwamba lazima hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya wahalifu watakaobainika kutenda kosa hilo lililofanyika usiku wa kuamkia Aprili mosi mwaka huu, katika eneo la Ibanda Kabuholo Kata ya Kirumba, na kwamba polisi haitaangalia washakiwa wanatoka chama gani na wana rangi au umbo gani.

Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoani Mwanza, Liberatus Barlow (RPC), amewaambia jioni hii ya leo waandishi wa habari kwamba, watuhumiwa hao wamekamatwa na wameunganishwa na watu waliowavamia na kuwajeruhi baadhi ya wanawake ambao walikutwa wakijadili namna ya kwenda kusimamia kura za wagombea wao katika Kata ya Kirumba jijini hapa.

“Tumewakamata watu 15 hadi sasa wanaosadikiwa kuhusika na tukio la shambulizi dhidi ya waheshimiwa wawili, Highness Kiwia wa Ilemela na Salvatori Machemli mbunge wa Ukerewe.

“Lakini kwa hawa waheshimiwa tutawahoji pale inapobidi kufanya hivyo. Mimi sijasema tutawakamata, inawezekana tukawahoji ili kupata maelezo yao. Na kama kuhojiwa kwa wabunge hawa si lazima polisi Mwanza, wanaweza kuhojiwa sehemu yoyote maana polisi tupo kila sehemu”, alisema Kamanda Barlow huku akikataa kuwataja majina watu hao 15 kwa madai kwamba upelelezi bado unaendelea.

Jana, Mkuu wa Kitengo cha Upelelezi wa Makosa ya Jinai wa Jeshi la Polisi Mkoani Mwanza, Deusdedith Nsimeki (RCO), limwambia mwandishi wa habari hizi kwamba, wanatarajia kuwakamata na kuwahoji wabunge hao wanaoendelea na matibabu katika hospitali ya taifa ya Muhimbili kutokana na majeraha makubwa waliyoyapata.

Katika maelezo yake, RCO alisema polisi wanaweza kuwakamata wabunge hao, Kiwia na Machemli wakiwa bado wamelazwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili wanakopatiwa matibabu, au inaweza kuwasubili watoke hospitalini kisha iwakamate.

“Hawa wabunge lazima tuwakamate watueleze vizuri kuhusiana na tukio la kukatwa kwao mapanga usiku. Watueleze kwa nini walienda huko Kabuholo gizani usiku tena bila kutoa taarifa polisi?.

“Kukatwa kwao mapanga isiwe sababu ya kutokamatwa na polisi, lazima tuwakamate tuwahoji. Inawezekana wabunge hawa ndiyo chanzo kikubwa katika kesi hii.

“Tunaweza kuwakamata wakiwa wamelazwa hospitalini hukohuko, au tukaamua kuwasubiri watoke hospitalini halafu tuwakamate!. Sheria zinaturuhusu sisi kumsomea mashtaka mtu yeyote hata kama kalala kitandani”, alisema RCO Nsimeki ambapo baadaye akatania kwa kusema: “Unajua mtu anaweza kukutwa na mke wa mtu akakatwa mapanga na kichwa kikaning’inia, sasa utasema huyo mtu si chanzo?”.

Katika maelezo yake jana kwa waandishi wa habari ofisini kwake, Kamanda Barlow alikanusha vikali taarifa za mbunge wa Ukerewe, Machemli kwamba wakati wakishambuliwa walikuwapo askari polisi wakiwa na silaha aina ya SMG, ambapo alisema: “Taarifa hizo si kweli. Polisi walifika na kufanya kazi ngumu kweli ya kuwaokoa hawa waheshimiwa. polisi hao hao walikuwa wakijificha hadi kwenye uvungu wa magari kukwepa mawe, hizi taarifa si kweli”.

Hata hivyo, juzi Machemli alinukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari akilituhumu jeshi la polisi kwa madai kwamba wakati wakishambuliwa na kuumizwa walikuwepo baadhi ya askari polisi wakiwa na SMG, na kwamba alijaribu kujivuta kwenda kumshika mguu askari polisi mmoja ili amnyang’anye silaha ili ajiokoe, lakini alipigwa teke.

“Aisee nimepata kipondo kama mbwa mwizi. Tumepikika hasa…lakini wakati tunashambuliwa na kukatwa mapanga walikuwepo askari polisi hatua chache wanatuangalia na SMG. Nilijivuta kumsogelea polisi nimnyang’anye silaha nijisaidie lakini akanipiga teke nikaendelea kupata kipondo”, alisema Machemli wakati alipohojiwa na mwandishi wa habari wa Shirika la Utangazaji nchini Uingereza (BBC), Erick David Nampesa.

Hata hivyo, kikao hicho cha jana kati ya RPC Barlow na waandishi wa habari nusura kivunjike baada ya RPC kutoa amri ya kuzuiliwa mwandishi wa habari wa Mwananchi, Fredrick Katulanda kufika katika eneo zilizopo ofisi za makao makuu ya polisi mkoani Mwanza, baada ya Katulanda kukataa kumpa RPC namba za magari yanayodaiwa kuwepo eneo la tukio wakati wabunge hao wakishambuliwa. Lakini baadaye tofauti zao hizo zilimalizika.

Habari hii imeandikwa na Sitta Tumma – Mwanza.

2 Comments
  • polisi fanyeni kazi yenu ili haki itendeke ili wananchi tuendelee kua na imani na jeshi hlo ambapo ndyo kimbilio la wanyonge sisi.hususani kipindi hiki ambapo kwa kiasi fulani wananchi wamekosa imani na nyie

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *