KAMA Serikali ingesitisha kununua ‘mashangingi’ mawili tu kwa mwaka na kuelekeza fedha za magari hayo katika utafiti wa mifugo ingesaidia kutengeneza maabara kubwa ya kisasa ambayo ingetumika kama benki ya vinasaba vya wanyama (Gene Bank) katika Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (Taliri) kituo cha Mpwapwa, FikraPevu inaripoti.
Uchunguzi wa FikraPevu umeonyesha kwamba, maabara hiyo ya kisasa imekwama kwa miaka minne sasa licha ya serikali kuwapaleka wataalam wake kwa mafunzo katika nchi za Ethiopia na Brazil ili kupata ujuzi wa namna ya kutafiti na kuhifadhi vinasaba vya mifugo.
Kwa mujibu wa uchunguzi huo, gharama za kununulia vifaa vya maabara hiyo katika Kituo cha Utafiti wa Mifugo Mpwapwa sasa imefikia kiasi cha Shs. 500 milioni, ikiwa imeongezeka kutoka Shs. 300 milioni zilizokuwa zimekadiriwa awali mwaka 2013.
FikraPevu inatambua kwamba, gari moja aina ya Toyota Land Cruiser, maarufu kama ‘shangingi’ linagharimu kiasi cha Shs. 300 milioni, hivyo kama bajeti ya ununuzi wa magari hayo ingepunguzwa magari mawili tu, ingetosheleza kununulia vifaa vinavyotakiwa kwenye maabara hiyo.
Germanus Bahati Tungu, mmoja wa watafiti wakongwe ambaye ni miongoni mwa waliopatiwa mafunzo Ethiopia na Brazil, anasema kununuliwa kwa vifaa hivyo vya maabara kungesaidia kuhifadhi mbegu mbalimbali za wanyama, hususan ng’ombe, mbuzi, nguruwe na kuku wa kienyeji.
Tungu anasema kwamba, endapo vifaa hivyo vingepatikana vingesaidia uzalishaji wa mbegu za kutosha na uhifadhi, hivyo kuiwezesha taasisi hiyo kusambaza mbegu bora za ng’ombe aina ya Mpwapwa kwa wakulima kwa kupandikiza mimba kwa ng’ombe wengine kutumia viinitete (embryonic insemination) badala ya kutumia dume.
“Lakini sasa mambo ni magumu katika uzalishaji wa mbegu kwa sababu hatuna vifaa vya kuhifadhia na siyo rahisi kuzalisha ng’ombe wa kutosha kwa wakati mmoja kwani kwa kawaida ng’ombe anazaa mara moja tu kwa mwaka,” anasema Tungu, ambaye huenda mwakani akastaafu kabla ya kuutumia ujuzi wake aliousomea kwa gharama za kodi ya wananchi.
Anaongeza: “Nasikitika nitakuwa sijaitendea haki taaluma yangu, nimepelekwa nje kwa gharama, lakini kama maabara hii ingewezeshwa kwa kununuliwa vifaa, ujuzi wangu wote ningeutumia kuhakikisha tunaweka vinasaba vya kutosha.”
Mkurugenzi wa Kituo cha Taliri-Mpwapwa, Dk. Eliakunda Kimbi, lengo la kuanzisha benki hiyo ya vinasaba (Gene Bank) siyo tu kurahisisha uzalishaji wa mbegu bora za mifugo na kusambaza kwa wakulima, bali pia kuhifadhi hata mbegu za wanyama za asili.
Anasema, ingawa kituo hicho kinasambaza ng’ombe aina ya Mpwapwa waliotafitiwa kituoni hapo pamoja na mbuzi bora aina ya Malya Blended wanaozaa watoto mapacha, lakini pia wanataka kuhifadhi vinasaba vya mbuzi wa asili kama wanavyofanya hivi sasa ambapo wanao mbuzi kama Gogo White, Newala Goats na Ujiji Goats (Buha).
Pia wanao ng’ombe wengine wa asili kama Singida White, Iringa Red na Ufipa ambao wanaendelea kuwafanyia tafiti za kuwahifadhi na kutathmini uwezo wa mifugo hiyo ya asili.
“Kwa kawaida, hata kama ng’ombe hawa wa asili (Zebu) wanafanana kama ilivyo kwa mbuzi wa asili, lakini wana tofauti kubwa kutoka eneo moja na jingine, hivyo ni vyema kuhifadhi vinasaba vyake kwa kuwa aina nyingi zinatoweka hivi sasa,” anasema Dk. Kimbi.
Akizungumzia mafanikio ya tafiti ambazo zimekwishafanyika kituoni hapo mpaka sasa, Dk. Kimbi anasema wamefanikiwa kufanya utafiti wa ng’ombe aina ya Mpwapwa ukilenga kuhifadhi aina hiyo ya koosafu, kuzalisha idadi ya kuwatosheleza kwa ajili ya wafugaji na kuimarisha kizazi (purity maintenance and stabilization).
Aidha, anasema wamefanya utafiti kutathmini uwezo wa uzalishaji wa kuku wa asili kwa kuangalia aina nne za kuku hao ambao ni Kuchi, Kishingo, Horace na Sasamala.
“Tumefanya utafiti wa majani na mikunde mbalimbali kwa ajili ya kuongeza upatikanaji wa mbegu za malisho bora kwa wafugaji ambapo kwa sasa jumla ya aina 80 za malisho zinahifadhiwa katika hifadhi ya vinasaba vya malisho (Gene Bank) hapa kituoni,” anasema Dk. Kimbi.
Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, msimu wa 2015/2016 kituo hicho kilizalisha kiasi cha malisho (hay) mikate 26,108 ambayo 56% iliuzwa kwa wafugaji na 44% ilitumika kwa ajili ya mifugo ya kituo.
FikraPevu inafahamu kwamba, kwa zaidi ya miaka 110 kituo hicho cha Mpwapwa, chini ya majina tofauti, kimekuwa kitovu cha utafiti wa mifugo nchini.
Taasisi hiyo ilianzishwa na wakoloni wa Kijerumani mwaka 1905, kikiwa kama kituo cha utafiti wa mifugo ambapo kiliendelea mpaka baada ya Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia.
Kabla ya kuhamia katika eneo la Kikombo kilipo hivi sasa, kituo hicho kilikuwa kimenzishwa mwaka 1903 katika Kijiji cha Godegode, takriban kilometa 20 kutoka Mpwapwa mjini.
Sababu za kuhamishia kituo hicho mjini Mpwapwa, kwa mujibu wa Dk. Kimbi, ni baada ya kushuhudia farasi na ng’ombe wao wengi wakifa kwa magonjwa ambayo hawakuwa wameyafahamu, hivyo kuamua kuanza utafiti.
“Baadaye ikagundulika kwamba wanyama hao walikuwa wakifa kwa ugonjwa wa Sotoka (Rinderpest), hivyo wakajenga josho la kuogeshea wanyama mwaka 1907. Josho hilo ndilo kongwe kuliko yote Afrika Mashariki,” anasema Dk. Kimbi.
Akielezea historia, Dk. Kimbi anasema, mnamo mwaka 1922 wakoloni Waingereza walianza kukihudumia kituo hicho na kuanzisha Maabara ya Utafiti wa Magonjwa ya Mifugo (Veterinary Pathology Laboratory).
Kuanzia mwaka 1924 hadi 1929 shughuli kuu za kituo hicho zikawa utafiti wa magonjwa ya Sotoka na Ndigana (Rinderpest and Trypanosomiasis), lakini sasa utafiti huo ukawa unafanyika kwa wanyama wote waliokuwepo kituoni hapo na maeneo ya jirani kwa vile ilionekana magonjwa hayo yalikuwa yakiwashambulia na wanyama wengine mbali ya farasi.
Zaidi ya dozi 50,000 za kuzuia Sotoka (anti-rinderpest serum) zilitolewa kila mwaka.
Makao makuu ya Idara ya Sayansi ya Mifugo na Utunzaji wa Wanyama, kama ilivyojulikana wakati huo wa ukoloni, ikahamia Mpwapwa kutoka Dar es Salaam mwaka 1929.
Aidha, uboreshaji wa ng'ombe wa kienyeji wenye asili ya Iringa, Rungwe, Singida na Masailand ulikuwa umeanza mapema mwaka 1923.
“Kuanzia mwaka 1930 hadi 1938, utafiti wa utunzaji wa mifugo ulipata sura mpya baada ya kuletwa mtaalam wa madawa na malisho. Shughuli za uzalishaji wa mifugo zilipamba zaidi mwaka 1944 baada ya kuteuliwa mtaalam wa vijinasaba (geneticts). Taasisi Kuu ya Mifugo ikaanzishwa mwaka 1951, na wakati huo huo kituo kikaona umuhimu wa kuiendeleza sekta ya mifugo, hivyo kikaanzisha kituo cha mafunzo ambacho sasa kinajulikana kama Livestock Training Agency (LITA),” anasema.
Dk. Kimbi anasema kwamba, makao makuu ya idara hiyo yalirejeshwa Dar es Salaam mwaka 1954 na kumwacha Ofisa Mkuu wa Mifugo hapo Mpwapwa ambaye alisimamia Maabara ya Utafiti, Kituo Kikuu cha Uzalishaji, na Utafiti wa Mifugo na Malisho.
Wanyama wa kufugwa waliokuwepo kituoni hapo walikuwa ng'ombe, nyati, kondoo, mbuzi, nguruwe, kuku na farasi.
Mnamo mwaka 1962 kulikuwa na mabadiliko ya muundo wa wizara na kukifanya kituo hicho kiitwe Kituo cha Majaribio ya Mifugo kikiwa kinahusika na mambo ya kilimo, utunzaji wa mifugo na uvuvi.
Mwaka 1966 Sera ya Maendeleo ya Mifugo iliyopitishwa na Bunge ikiwa inasisitiza umuhimu wa kueneza ng'ombe wenye ubora wa juu vijijini ilikifanya kituo kikazanie uzalishaji wa ng'ombe, ambapo sasa kikajulikana kama Kituo cha Uzalishaji wa Mifugo (Livestock Breeding Station). Mwishoni mwa miaka ya 1960 kituo hicho kikaitwa tena Taasisi ya Utafiti na Mafunzo ya Mifugo kikiegemea zaidi maendeleo ya mifugo.
Kuanzia mwaka 1977 utafiti wa mafunzo na mifugo viligawanywa katika taasisi mbili tofauti, Taasisi ya Utafiti, ambayo kuanzia Julai 1981 ilijulikana kama Taasisi ya Uzalishaji na Utafiti wa Mifugo (LPRI) ikiwa chini ya Mkurugenzi na Chuo cha LITA kikawa chini ya Mkuu wa Chuo. Shirika la Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRO) lilianza kusimamia taasisi hiyo mwaka 1981 hadi lilipokufa mwaka 1989, na kuanzia hapo mpaka sasa taasisi hiyo pamoja na chuo viko chini ya Wizara inayoshughulikia mifugo japo imekuwa ikibadilishwa kila mara.
Hivi sasa taasisi hiyo inajishughulisha na uzalishaji wa ng'ombe aina ya Mpwapwa, Mbuzi wa Maziwa jamii ya Malya (Malya Blended Goat), Kuku wa Kienyeji, Malisho, Lishe, Matibabu ya Mifugo, na Utoaji wa Elimu kwa Wakulima na Wafugaji.