Mchochota wa Ini aina ya B – Ugonjwa hatari zaidi ya UKIMWI

Dr. Joachim Mabula

INI huchuja sumu kutoka kwenye damu na kufanya kazi nyingine muhimu 500. Kwa sababu hiyo, Mchochota wa Ini, yaani, uvimbe katika Ini unaweza kuharibu afya ya mtu.

Mchochota wa Ini unaweza kusababishwa na kunywa kileo kupita kiasi au sumu inapoingia mwilini. Hata hivyo, mara nyingi ugonjwa huo husababishwa na virusi. Wanasayansi wamegundua virusi vitano vinavyosababisha ugonjwa huo na wanasema kwamba huenda kuna vingine vitatu.

Moja tu kati ya virusi hivyo vitano—virusi vya Mchochota wa Ini aina ya B (HBV)—huua watu 600,000 hivi kila mwaka, idadi ya watu inayolingana na wale wanaokufa kutokana na Malaria. Zaidi ya watu Bilioni Mbili, yaani, asilimia 33 hivi ya watu wote ulimwenguni, wameambukizwa virusi vya HBV, na wengi wao hupona baada ya miezi michache. Watu Milioni 350 hivi huendelea kuwa na virusi hivyo mwilini. Maisha yao yote, iwe wana dalili za ugonjwa huo au la, watu hao wanaweza kuwaambukiza wengine.

Mtu aliye na virusi vya HBV mwilini akianza matibabu mapema, anaweza kuzuia Ini lake lisiharibike sana. Lakini watu wengi hawajui kwamba wameambukizwa kwa kuwa ni uchunguzi fulani hususa wa damu unaoweza kuonyesha virusi hivyo. Hata uchunguzi wa kawaida wa kuangalia utendaji wa Ini unaweza kukosa kuonyesha virusi hivyo. Kwa hiyo, Mchochota wa Ini aina ya B unaweza kuua kimyakimya bila kuonyesha dalili zozote. Huenda dalili zikaonekana waziwazi miaka mingi baada ya mtu kuambukizwa. Zinapoonekana, huenda Tayari Ini limenyauka au lina Kansa, na magonjwa hayo huua asilimia 25 ya watu walio na Virusi vya HBV.

Kwa kweli, asilimia 35 hivi ya watu hawajui jinsi walivyoambukizwa.

Hata hivyo, hinachojulikana ni kwamba Virusi vya Mchochota wa Ini aina ya B havirithiwi na haviambukizwi kwa kumgusa mtu aliye na Virusi hivyo au kula chakula pamoja naye. Badala yake, mtu huambukizwa virusi hivyo wakati damu au umajimaji mwingine wa mwili kama vile Mate, Shahawa, au umajimaji unaotoka katika sehemu ya uke ya mtu aliyeambukizwa unapoingia kwenye mfumo wa damu, kupitia kidonda kwenye ngozi au tando-telezi za mwili.

Watu wengi wanaendelea kuambukizwa kwa kutiwa damu yenye virusi hivyo, hasa katika nchi ambako hakuna vifaa bora vya kuchunguza virusi hivyo katika damu. Virusi vya HBV vina uwezo mkubwa zaidi wa kuambukiza kwa kulinganishwa na Virusi vya UKIMWI. Hata kiasi kidogo sana cha damu yenye Virusi hivyo kama ile inayobaki kwenye wembe, inaweza kupitisha virusi hivyo, na tone la damu iliyokauka kwa juma moja au hata zaidi inaweza kumwambukiza mtu Virusi hivyo.

AINA ZA MCHOCHOTA WA INI?

Kuna Virusi vitano vinavyojulikana kusababisha Mchochota wa Ini, na vile vitatu vinavyojulikana sana Hupewa alama ya A, B, na C. Bado kuna vingine vinavyodhaniwa kuwa vinasababisha ugonjwa huo. Aina zote za Mchochota wa Ini huwa na dalili kama za homa na huenda zikatia ndani Homa ya nyongo Manjano(Jaundice). Watu wengi, hasa watoto hawaonyeshi dalili zozote.

Dalili za Mchochota wa Ini aina ya B na C zinapoonekana, huenda tayari Ini huwa limeharibika sana.

MCHOCHOTA WA INI AINA YA B (HBV)


Uenezwaji
Njia za uenezwaji zinafanana na zile za Virusi vya ukimwi, ingawa Virusi vya Mchochota wa Ini aina B huambukiza mara 50 hadi 100 zaidi ya Virusi vya UKIMWI. Tofauti na Virusi vya UKIMWI, Virusi vya Mchochota wa Ini aina B vinaweza kustahimili kuishi nje kwa angalau siku saba. Katika muda huu, Virusi hivi vinaweza kusababisha maambukizi kama vitaingia kwenye mwili wa binadamu ambaye hana kinga ya chanjo.

Muda ambao virusi hukaa ndani ya mwili hadi kuanza kuonyesha dalili ni siku 90 kwa wastani, ila hutofautiana kuanzia siku 30 hadi 180. Virusi vinaweza kugundulika siku ya 30 hadi ya 60 baada ya maambukizi na kuendelea katika muda tofauti tofauti.

Virusi vya HBV hupatikana katika damu, Shahawa, na Umajimaji unaotoka kwenye sehemu za uke za watu walioambukizwa. Virusi hivyo huambukizwa wakati umajimaji huo unapoingia mwilini mwa mtu asiye na kinga. Virusi hivyo vinaweza kupitishwa mama anapojifungua (Mama mwenye Virusi hivyo
anaweza kuvipitisha kwa mtoto wake).

Vifaa vya kitiba, matibabu ya meno, au vya kuchanja mwili visiposafishwa vizuri.

Mtu anapotumia vitu ambavyo vimetumiwa na mtu mwingine kama vile sindano, wembe, vitu vya kukata kucha, miswaki, au kitu chochote kile kinachoweza kupitisha kiasi kidogo cha damu kupitia kidonda kwenye ngozi.

Kupitia kufanya ngono.

Wataalamu wa kitiba wanasema kwamba virusi vya HBV haviambukizwi kupitia wadudu, au kwa kukohoa, kushikana mikono, kukumbatiana, kupigana busu kwenye mashavu, kunyonyesha, au kula chakula au vinywaji katika chombo kimoja, vijiti vya kulia (Mfano vya Wachina), au vyombo vingine vya kulia. Watu wazima wengi wenye virusi hivyo hupona na huwa na kinga ya ugonjwa huu. Ni rahisi sana kwa virusi hivyo kudumu katika damu ya watoto wadogo. Usipotibiwa, Mchochotawa Ini aina ya B unaweza kusababisha Ini liache kufanya kazi na hatimaye kutokeza kifo. Kuna chanjo ya kuzuia ugonjwa huo.

MATIBABU:
Hamna matibabu mahususi ya kuponya Mchochota wa Ini aina B. Huduma itolewayo inalenga katika kufariji, kupunguza maumivu na kutoa lishe bora ili kufidia maji anayopoteza mgonjwa anapotapika na kuharisha.

Baadhi ya watu wenye Mchochota wa Ini aina B ambao ni sugu hutibiwa kwa dawa zinazoua virusi. Matibabu haya yanaweza kugharimu mamilioni ya pesa za kitanzania.

Kansa/Saratani ya Ini mara nyingi hutokea kwa watu ambao ni nguvu kazi ya taifa na wanaotegemewa na familia zao. Kwa nchi zinazoendelea kama Tanzania, wengi hufa miezi michache baada ya kugunduliwa tatizo. Ila kwenye nchi zilizoendelea kama Japan, upasuaji na tiba za mionzi na
kemikali hurefusha maisha.

Watu waliopatwa na kusinyaa kwa Ini (Liver Cirhosis) wakati mwingine hupewa Ini lingine kutoka kwa watu wazima ingawa watu walio tayari kutoa Ini ni wachache sana.

Kuishi Ukiwa Na Mchochota Wa Ini Aina Ya B

Virusi hivyo hudumu mwilini ikiwa mfumo wa kinga wa mwili haujaviondoa katika muda wa miezi sita.

Damu kutoka kwa mtu mwenye virusi hivyo inapaswa kupanguswa haraka na vizuri mtu akiwa amevaa glavu kwa kutumia kipimo 1 cha dawa ya kuondoa madoa kilichochanganywa na vipimo 10 vya Maji.

Kutibiwa mapema kunaweza kupunguza madhara.

Kwa sababu ya kuogopa kubaguliwa, wengi hawaendi kupimwa au hawawaelezi wengine kwamba wana ugonjwa huo.

KUZUIA KUENEA KWA HBV
Ingawa HBV huathiri watu ulimwenguni pote, asilimia 78 hivi ya wale ambao virusi hivyo vimedumu mwilini huishi Asia na katika visiwa vya Pasifiki.
Katika mengi ya maeneo hayo, mtu 1 kati ya watu 10 Ana virusi hivyo. Wengi wao huambukizwa virusi hivyo kutoka kwa mama zao wanapozaliwa au utotoni kupitia damu ya watoto wenye Virusi hivyo. Chanjo kwa ajili ya watoto waliotoka tu kuzaliwa na watu walio katika hatari ya kuambukizwa imesaidia kuzuia kuenea kwa Virusi hivyo. Katika maeneo ambayo chanjo hiyo imetumiwa, maambukizo yamepungua sana.

Chanjo tatu mpaka nne za kuzuia Virusi vienezavyo Mchochota wa Ini aina B zikitolewa kwa mpishano uliopangwa zinaweza kulinda kwa zaidi ya miaka 20 na zaidi. Kwa wale walio chini ya miaka 18 kama hawakupata chanjo wakiwa wadogo wanapaswa kupata chanjo.

2 Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *