Mfamasia wa wilaya ya Magu mbaroni kwa wizi wa dawa

Jamii Africa

MFAMASIA wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu mkoani hapa, Kanuti Kimaro ametiwa mbaroni akituhumiwa  kutokuwa mwaminifu  kwa mwajiri wake na kisha kuuza mgawo wa dawa za binadamu  pamoja na vitendanishi vya kisasa (M.R.D.T) ambavyo vinatumika katika upimaji wa ugonjwa wa malaria; vyote vikiwa na thamani ya shilingi milioni 30.

Chanzo cha habari kimeifahamisha FikraPevu kwamba Mfamasia huyo alikamatwa Disemba 13 mwaka  huu na kwamba hadi sasa anashikiliwa katika kituo kikuu cha Polisi Wilayani Magu.

Inadaiwa kuwa wizi huo utasababisha wakazi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo kukoswa dawa kupitia  katika zahanati, vituo vya afya pamoja na Hospitali ya  wilaya  hiyo kwa muda wa miezi minne mfululizo.

Kwa sharti la kutotajwa jina, chanzo chetu kinadai kwamba Kimaro alikamatwa na maafisa kutoka Taasisi  ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) wilayani humo.

Inadaiwa kwamba Mfamasia huyo anatuhumiwa kuuza dawa mbalimbali za binadamu pamoja na ‘kit’ 8 zenye jumla ya vipande 800 vya vitendanishi vinavyotolewa na wafadhili kwa ajili ya kurahisisha zoezi la upimaji wa  viini vya ugonjwa  wa malaria.

“Akiwa peke yake Mfamasia huyo alikiuka taratibu za Wizara kisha akaenda Bohari Kuu ya Dawa (MSD) Jijini Mwanza ambapo alikabidhiwa  mgawo  wa dawa pamoja na vitendanishi kutoka serikalini. Lakini cha ajabu, Kimaro  akaziuza  kwa wafanyabiashara binafsi, badala ya kuzifikisha ofisini ili ziweze kuwasaidia wananchi“ kilidai chanzo cha habari.

Inadaiwa kuwa kwa kutumia wadhifa wake, baada ya kuuza dawa Kimaro alirejea Magu na kumtaka mtumishi katika kitengo cha stoo aandike kuwa amepokea dawa pamoja na vitendanishi hivyo.

“Alipofika Magu akamtaka mfanyakazi kitengo cha ‘Stores’ eti aingize dawa hizo kwenye ‘Ledger Book’. Kilichotokea ni kwamba mtumishi huyo aligoma kuingiza taarifa hewa; na huenda taarifa zikawafikia Takukuru” kilisema chanzo cha habari.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Col. Ngudungi alikiri kuwepo kwa suala hilo.

“Ni kweli suala hilo lipo na tayari limeshaanza kujadiliwa na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya” Ngudungi alithibitisha ofisini kwake, Desemba 27 mwaka huu.

Alisema tayari ofisi yake imeanza kuchuku hatua ikiwemo kumsimamisha kazi kwa sababu amekiuka kanuni namba 37 ya sheria ya mwaka 2007 ya utumishi wa umma.

Alisema mtuhumiwa huyo amesimamishwa kazi tangu Disemba 19 mwaka huu.

“Kusema kweli mfamasia amefanya kitendo cha ajabu; kwamba badala ya kulinda dawa za serikali na mwajiri wake, yeye ndiye anashiriki katika kuhujumu. Mimi ninasema lazima sheria ichukue mkondo wake dhidi ya afisa huyo ambaye kwa kweli ameidhalilisha Wilaya ya Magu” alisema Mkuu wa Wilaya ya Magu, Zainab Kondo.

Alisema ana wasiwasi na utendaji kazi wa Bodi ya Hospitali na kwamba ofisi yake kwa kushirikiana na Takukuru, Jeshi la Polisi na Usalama wa Taifa wanaendelea na uchunguzi zaidi.

Kamanda wa Takukuru Mkoani hapa, Christopher Mariba hakupatikana ofisini kwake wala kwa njia ya simu ili aweze kuzungumzia suala hilo. Ilidaiwa kuwa alikuwa nje ya ofisi kwa ajili ya kazi nyingine. Hata hivyo, simu yake mara kadhaa  iliita bila kupokelewa.

Habari hii imeandikwa na Juma Ng’oko, Mwanza

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *