Mfumo wa China ni sahihi kama Tanzania inataka kupiga hatua ya maendeleo

Daniel Mbega

KWA muda mrefu kumekuwa na malumbano baina ya makundi mbalimbali ndani ya nchi kuhusu mfumo gani ambao Tanzania inaufuata katika kufikia maendeleo yanayohitajika.

Wengi wanajiuliza, je, Tanzania inafuata taratibu na kanuni za Ujamaa na Kujitegemea kama Katiba ya Jamuhuri ya Muungano ya mwaka 1977 ilivyoainisha kama mfumo wake rasmi wa maendeleo?

Kwa mtazamo wangu nasema hapana, ila tumesombwa na mafuriko ya mfumo wa ubepari unaotawala dunia ya sasa.

Ukitazama kwa undani utaona kwamba Tanzania inashindwa kufikia maendeleo yanayohitajika katika mfumo huo kwa kuwa tumesombwa na mafuriko ya ubepari bila kujua nini cha kufanya kama taifa na tuanzie wapi.

Jambo la kushangaza tunahusudu mfumo wa ubepari bila kujua nini misingi yake na sisi kama taifa tumeshindwa kufikiria namna ya kuishi katika mfumo huo, matokeo yake tumebaki kusubiri wamiliki wa mfumo kutuambia namna ya kuishi, kimsingi, kama taifa tumegeuka kuwa ‘kikaragosi’ tukisubiri wajuzi watugeuze vile wapendavyo.

Ni jambo la busara ikiwa tutajifunza kutoka kwenye mataifa yenye nguvu leo hii duniani na kuona ni mfumo upi hasa kama taifa utatufaa na kutuletea maendeleo ya haraka.

Hivi sasa tunayaona mataifa makubwa mawili yenye nguvu duniani ambayo ni Marekani na China.

Marekani inakadiriwa kuwa na Pato la Ndani la Taifa (Gross Domestic Product – GDP) la Dola za Kimarekani 16 trilioni wakati mapato ya China yanakadiriwa kuwa na Dola 10 trilioni kwa mwaka.

Kwa mapato hayo na kasi ya maendeleo iliyopo, baadhi ya wanauchumi wanadhani China tayari imeshaipiku Marekani kiuchumi. Inaweza kuwa kweli ama isiwe kweli kulingana na mifumo tofauti inayofuatwa na mataifa hayo.

Ni dhahiri ya kwamba mataifa haya mawili yamefika hapa kwa mifumo aina mbili tofauti ya maendeleo.

Marekani imefika hapo ilipo leo kwa kuamini katika mambo makubwa matatu katika mfumo wake rasmi wa maendeleo ambao unajumuisha ubepari binafsi (private capitalism), demokrasia ya kiliberali (liberal democracy) na kipaumbele kwenye haki za siasa dhidi ya haki za kiuchumi (prioritize political rights over economic rights).

Kwa upande mwingine, China ina mfumo ulio tofauti na ule wa Marekani ambao nao huamini katika mambo matatu kama ifuatavyo; ubepari wa umma (state capitalism), kutokuwepo na demokrasia (Non liberal democracy) na kipaumbele kwenye haki za kiuchumi dhidi ya haki za siasa (prioritize economic rights over political rights).

Kwa kutazama mifumo hii tofauti hapo juu ni dhahiri utagundua kwamba Tanzania imebebwa kwenye mafuriko ya mfumo unaofuatwa na Marekani na washirika wake wa Mataifa ya Ulaya Magharibi.

Lakini swali ni kwamba, kama Marekani wameendelea kwenye mfumo huo, kwa nini Tanzania inashindwa kusonga mbele?

Hapa ni vyema kutambua kuwa Marekani ni taifa kongwe ukilinganisha na Tanzania yenye miaka 55 ya uhuru. Marekani ilipata uhuru wake miaka 240 iliyopita kutoka kwa Waingereza.

Ili Tanzania ifike pale Marekani ilipo leo inahitaji zaidi ya miaka 185.

Lakini kwa upande mwingine, hebu tuitazame China yenye uhuru wa miaka 67 tu lakini inaifukuzi Marekani kwa karibu sana kiuchumi.

Ikumbukwe kwamba, mfumo wa Marekani unaamini zaidi katika ubepari binafsi (private capitalism) ambao huchochea zaidi utajiri wa watu wachache huku wengi wakibaki katika dimbwi la umaskini.

Kwa tafsiri zaidi, ubepari binafsi unashamirishwa na uwekezaji binafsi ambao kwa kiasi kikubwa umekumbatiwa na Tanzania.

Hii inamaanisha kwamba, kama taifa hatuwezi kusonga mbele kwa kuwa na matajiri wachache huku wengi wetu tukibaki maskini kwani hapa ndipo tunapoona ombwe la walionacho na wasionacho.

Ripoti ya Oxfam ya Januari 2016 inadhihirisha kuwa matajiri 62 tu ndio wanamiliki uchumi wa zaidi ya asilimia 50 ya watu wote duniani.

Hii inatupa tafsiri sahihi ya ubepari binafsi ambapo utagundua ya kuwa uchumi unaongozwa na watu binafsi badala ya umma ama serikali.

Kwa hali hii mfumo huo siyo rafiki kwa maendeleo ya Tanzania na naweza kudiriki kusema ya kuwa kama tutaufuata hatutaweza kuendelea kwa miaka mingi ijayo.

Demokrasia kwa wengi wetu ni jambo jema na la msingi, lakini swali la kujiuliza hapa demokrasia tunayoifurahia ni ipi na inatoka wapi? Je, demokrasia hii inayohubiriwa na mfumo wa Marekani kama sehemu muhimu ya maendeleo tunaielewa kwa undani kama nguzo muhimu ya maendeleo kwetu ama demokrasia hii tumeinunua kama vile tunavyonunua bidhaa kutoka nchi za nje au tumeomba kama msaada mwingine tu?

Tafiti zimedhihirisha kwamba, Marekani yenyewe kama taifa kubwa limeweza kuifikia demokrasia wanayojivunia leo baada ya miaka 157 ya uhuru, japokuwa tafiti nyingine zinaonyesha ya kuwa bado nchi hiyo  haijafikia demokrasia halisi.

Tafiti nyingine zimekwenda mbali na kusema kuwa ili kuwepo na demokrasia ya kweli ni lazima kuwe na uchumi imara kwani ndio huchochea kuwepo kwa demokrasia imara.

Nchi mbalimbali kama vile Taiwan, Singapore, Chile, China zimedhihirisha ya kuwa uchumi imara ndio nguzo ya demokrasia na si vinginevyo.

Ukitazama kwa undani utaona kwamba, demokrasia ya Tanzania na Afrika kwa ujumla inalega kwa kuwa umaskini uliokithiri umeshindwa kuipa nguvu, ndiyo maana tunaendelea kutegemea misaada na mikopo.

Hii inadhihirishwa na uwezo wa wananchi maskini walio wengi kuchagua viongozi kwa uhuru kwa kuwa pindi tupewapo vitenge, pesa ama chakula kidogo huishia kuchagua watu waliotupatia hayo mahitaji bila kujali kama tunachagua watu sahihi au la.

Kwa hiyo ni ukweli tukisema kuwa Watanzania walio wengi wanashindwa kuchagua viongozi imara kwa kuwa hawana nguvu ya uchumi ambayo itatufanya tuwe na jeuri ya kumchagua yule tunayomhitaji ili kuleta maendeleo badala ya wale ambao hutupatia pesa na chakula.

Kauli kama “Ukiwachagua hawa hatutawaletea maendeleo kijijini kwenu” husikika kila wakati uchaguzi unapowadia. Je, kwa umaskini uliopo na kwa kauli za vitisho kama hizi, Watanzania wanaweza kumchagua kiongozi bora mwenye kuwaletea maendeleo?

Lakini vipi kuhusu mfumo unaoingoza China, unaweza kuisaidia Tanzania kufikia maendeleo ya haraka?

Kwa mtazamo wangu, naona unafaa na tuanze haraka sana kama tunataka kufika maendeleo kwa miaka mifupi ijayo.  

Kwanza kabisa ni vyema tukafamu ya kuwa China ni nchi ya Kisoshalisti inayoongozwa na siasa za Kikomunisti yenye kuamini chama kimoja, ingawa wengine hujiuliza kama nchi hiyo ni ya Kisoshalisti ama Kibepari? Tutalijibu hili wakati mwingine kwa sasa tutafakari huu mfumo kwanza.

China kama nchi ilirudi kwenye misingi yake ya Kisoshalisti baada ya Deng Xiaoping kugundua kuwa Mao Tse Tung alikiuka misingi hiyo na kuanza kuwakumbatia mabepari.

Kama nilivyoainisha hapo juu, China inaamini katika ubebari wa umma (state capitalism) ambapo uchumi na njia kuu za uzalishaji mali humilikiwa na serikali na umma kwa ujumla, tofauti na ubepari binafsi ambao husisitiza juu ya uwekezaji binafsi.

China inamiliki uchumi wake kwa asilimia zote ikimaanisha ya kuwa viwanda, benki, huduma za kijamii ni mali ya serikali na huduma zote za msingi huwafikia watu kwa haraka zaidi. Jambo muhimu sana hapa ni , serikali ndiyo hupanga bei ya bidhaa zinazozalishwa.

Natumaini kwa aina hii ya mfumo tunaona ni kwa namna gani serikali ya watu wa China inavyosongoa mbele kwa haraka kwani uchumi wake hautetereshwi na wawekezaji binafsi na endapo wawekezaji watakwenda China, serikali huchukua hisa katika kampuni hizo za kigeni ili iendelee kuwa na nguvu.

Hebu tafakari ni kwa kiasi gani Tanzania tumebinafsisha kila kitu kwa muktadha ya kwamba serikali haitaki kufanya biashara inataka kubaki msimamizi tu.

Kila kitu sasa hivi Tanzania kimebaki chini ya wawekezaji ambao hutoa huduma za jamii, humiliki viwanda, migodi, kilimo na nyanja nyingine nyingi za maendeleo.

Kwa kuwa mabepari wametambua tumeshasombwa na mafuriko hawataki tutoke huko wametuwekea vikwazo vingi ili waendelee kunufaika wao na Watanzania wabaki kuwa wasindikizaji tu.

Kwa kuhitimisha, kama Tanzania inataka kutoka hapa ilipo leo ni dhahiri tujifunze kutoka kwa China na turudi kwenye ubao tuanze kutenda kama vile misingi ya Ujamaa na Kujitegemea ilivyowekwa huku tukijifunza dunia inavyobadilika na kuiweka misingi hiyo katika mfumo tuliochagua.

Tukizidi kufuata mfumo wa Marekani ni dhahiri hatutaendelea kamwe.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *