“Afya njema ni msingi mkubwa wa maendeleo katika taifa. Nchi ambayo wananchi wake hawana afya njema kamwe haiwezi kupata maendeleo, hii ni kwa sababu mwananchi asiye na afya njema hawezi kushiriki kwenye ujenzi wa taifa”, ni maneno ya Rais wa Tanzania, John Magufuli aliyoyatoa Novemba 25, 2017 wakati akifungua Hospitali ya Taaluma na Tiba ya Mloganzila iliyopo mkoani Pwani.
Licha ya juhudi mbalimbali za serikali ikishirikiana na wahisani kuboresha sekta ya afya, bado sekta hiyo inakabiliwa na changamoto ya upungufu wa Watumishi wa Afya wakiwemo madaktari na wauguzi. Changamoto hii inaziweka rehani afya za wananchi kwa sababu wakienda katika baadhi ya vituo vya afya na hospitali hawapati huduma zinazostahili.
Kulingana na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inaeleza kuwa Tanzania ina upungufu wa watumishi wa afya 95,059 ambapo waliopo ni 89,842 ili kukidhi mahitaji yote wanahitajika watumishi 184,901. Upungufu huo ni zaidi ya nusu ya watumishi wa afya wanaohitajika nchini. Hii inadhihirisha wazi kuwa wananchi wengi hawapati huduma bora za afya na kuathiri mwenendo wa uchumi wa taifa.
Sera ya Afya ya mwaka 2007, inaielekeza serikali, “Kuinua hali ya afya ya wananchi wote na hasa wale walioko kwenye hatari zaidi, kwa kuweka mfumo wa huduma za Afya utakaokidhi mahitaji ya wananchi na kuongeza umri wa kuishi wa watanzania. Kutoa huduma muhimu za afya zenye uwiano wa kijiografia, viwango vya ubora unaokubalika, gharama nafuu na zilizo endelevu”.
Madhumuni ya Sera bado hayajazingatiwa ipasavyo ikizingatiwa kuwa upungufu wa madaktari unaenda sambamba na mgawanyo usio mzuri wa watumishi wa afya katika maeneo mbalimbali nchini na kusababisha maeneo hasa ya mijini kuwa na madaktari wengi kuliko maeneo mengine ya nchi.
Hali ilivyo sasa
Rais John Magufuli katika hotuba yake aliyoitoa katika hospitali ya Mlonganzila amekiri wazi kuwa hakuna mgawanyo ulio sawa wa madaktari katika vituo vya afya na hospitali nchini. Ifuatayo ni sehemu ya hotuba yake inayoelezea mgawanyo wa madaktari;
“Kwa sababu panakuwepo na mgawanyiko usiowiana wa madaktari kati ya hapa Dar es Salaam na mikoani. Hali kadharika na hospitali za rufaa bingwa na zisizo za rufaa. Napenda nitoe mifano michache; hospitali ya Taifa Muhimbili yenye takribani vitanda 1,600 ina jumla ya Madaktari Bingwa, madaktari wanafunzi na Wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Muhimbili wapatao 532.
Hiyo maana yake ukigawa kwa hesabu za haraka haraka kila daktari unahudumia vitanda 3 lakini katika mkoa wa Tabora, daktari mmoja alikuwa akihudumia wagonjwa 208,309 kwa mujibu wa Sensa ya mwaka 2012.
Mfano mwingine ni wa hapa hapa Dar es Salaam, hospitali ya Manispaa ya Temeke yenye kuhudumia wastani wa wajawazito wanaojifungua 100 kwa siku ina Madaktari Bingwa wawili. Lakini hospitali ya Taifa ya Muhimbili yenye kuhudumia wastani wa wakina mama wanaojifungua katika ya 40 na 50 kwa siku ina madaktari bingwa 40 ukiachilia mbali ya madaktari wanafunzi waliopo. Hii inadhihirisha kuwa hakuna mgawanyo mzuri wa madaktari wachache tulionao.
Ni kweli hospitali zetu za kibingwa zinahitaji kuwa na madaktari wengi lakini haina maana madaktari wengi kwenye hospitali bingwa wakati hospitali nyingine zenye kuhudumia watu wengi hazina madaktari.
Ninafahamu kwa mfano madaktari wa Muhimbili wanapoajiriwa pale wanapoamua kwenda kusoma Masters (Shahada ya Uzamili) huwa wanabaki palepale hawaendi mikoani. Tukiruhusu hali hii kuendelea wananchi wengi watakuwa hawahudumiwi vizuri kwenye hospitali za chini na hata wakipewa rufaa kwenda hospitali bingwa watakuwa tayari wamechelewa na kushindwa kutibika”.
Jengo la Hospitali ya Taaluma na Tiba ya Mloganzila
Mkakati wa serikali kutatua tatizo Mgawanyo wa Madaktari
Mkakati wa serikali ni kuhakikisha wanasomesha madaktari wengi zaidi na kuwapeleka mikoani ambako hospitali nyingi hazina madaktari bingwa. Kwa kulitambua hilo serikali inaendelea kutoa vibali vya ajira kwa wanafunzi waliohitimu katika fani ya afya.
Rais Magufuli anasema katika hotuba yake, “Tumetoa vibali vya ajira vipatavyo 3,410 na katika humo patakuwa na madaktari pamoja na wataalamu mbalimbali wa afya, lengo ni kupunguza pengo la watumishi wa afya lililopo”,
“Lakini sio kwamba tunataka kuongeza idadi tu hapa tunahimiza ubora wa wataalmu wanaozalishwa kwenye vituo vyetu”.
Serikali imekuwa ikieleza kuwa uhaba wa madaktari katika vituo vya afya hautokani na uchache wa madaktari bali uwezo kuwaajiri wote kwa wakati mmoja.
Hata hivyo, rais Magufuli ameagiza mamlaka husika kuzirudisha hospitali za Mikoa chini ya usimamizi wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kutoka Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) ili kuongeza ufanisi na utendaji wa hospitali hizo ambazo zina madaktari bingwa.
Rais amesema taaluma lazima iheshimiwe kwa sababu Wizara ya Afya inafahamu kwa kina mahitaji ya sekta ya afya ikiwemo upungufu wa madaktari.
“Natambua suala la Wizara ya Afya kusimamia hospitali za rufaa na bingwa maalumu pekee na hospitali zingine kuanzia ngazi ya mkoa kuwa chini ya TAMISEMI nalo ni tatizo. Wizara ya Afya ndio msimamizi wa sera, ndio wanaojua daktari gani aende mkoa gani ”,amesema Rais.