"rushwa adui wa haki” ni msemo ulitumika sana na mwasisi wa taifa la Tanzania mwalimu Julius Nyerere katika harakati zake za kupinga utoaji na upokeaji rushwa ambayo ililenga kupotosha haki na usawa miongoni mwa wananchi.
Msemo huu hakuutumia katika maneno bali alipinga rushwa kivitendo na kuhakikisha viongozi na wananchi wanaepukana na mdudu rushwa na kujenga jamii inayoheshimu utawala wa sheria na haki za binadamu.
Hata chama ambacho alikuwa anakiongoza ambacho kinashika dola mpaka leo, Chama Cha Mapinduzi (CCM), katika katiba yake kina kipengele cha ahadi za mwanachama ambazo kila mtu aliyetaka kujiunga na chama hicho alitakiwa kuapa au kutamka kwa dhati kabla ya kukubaliwa kuwa mwanachama wa chama hicho.
Ahadi namba nne inasema “Rushwa ni adui wa Haki, Sitapokea wala kutoa rushwa” maneno haya yalichukuliwa kwa uzito mkubwa na mara kwa mara wanachama walikumbushwa ahadi hiyo kwa lengo la kukiimarisha chama, lakini sidhani kwa wakati huu kama ahadi hiyo inatendewa kazi kama zamani.
Ahadi hiyo ilikuwa ni nuru sio tu kwa wananchama wa CCM bali kwa taifa lote. Faida ilionekana katika upatikanaji wa huduma za kijamii kama vile maji, umeme, hospitali, elimu, makazi na chakula ambapo kwa kiasi kikubwa zilikuwa za kuridhisha kulingana na uchumi wa wakati huo ambao ulikuwa unategemea zaidi kilimo cha mazao ya biashara. Haki haikupatikana kwa fedha wala vitu bali kwa utu na upendo.
Hali ya mambo ni tofauti na wakati huu, hata wanachama wa chama hicho wengi wao wametuhumiwa kwa nyakati tofauti kuhusika na ufisadi mkubwa kama wa Richmond, Tegeta Escrow. Hii ni udhihirisho kuwa ahadi hiyo haina nguvu tena kama ilivyokuwa wakati wa uongozi wa Mwalimu Nyerere, ambapo kila mtu aliogopa kujiingiza katika vitendo vya kupokea na kutoa rushwa ili kuhakikisha rasilimali za nchi zinawanufaisha wananchi wote bila kujali matabaka.
Rushwa imekuwa rafiki wa haki na wapo baadhi ya watu hasa vijana kukiri waziwazi kupokea na kutoa rushwa ili wapate haki kwa kisingizio kuwa bila ‘mlungula’ hakuna jambo linalowezeka.
Katika hali ya kawaida inaonekana rushwa inarahisisha upatikanaji wa stahili za maisha, lakini upande wa pili rushwa inaliangamiza taifa letu kwa kiasi kikubwa na kutishia kutoweka kwa amani na utulivu wetu ambao tumeujenga kwa muda mrefu.
Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na rais John Magufuli imethubutu kupambana na ufisadi kivitendo kwa sehemu lakini bado hatujafikia hatua ya kuimaliza kabisa ikizingatiwa kuwa rushwa inajitokeza kwa mazingira tofauti tofauti.
Watu wanathamini vitu kuliko utu, chuki na uhasama umeongezeka katika jamii yetu kwa sababu ya rushwa ambayo inazidi kuhalalishwa na hata wale watu wanaoaminika katika jamii kusimama kupinga upotoshaji wa haki, nao kwa wakati tofauti wamejiingiza katika kadhia hiyo.
Kuaminiana hakupo tena, watanzania ambao miaka ya nyuma tuliheshimiana na kuaminiana katika mambo mengi, leo tumegeuka kuwa wanyama kiasi kwamba watu wanaogopa kula na kunywa pamoja kwa kuhofia kuwekewa sumu.
Tunalipeleka wapi taifa hili ikiwa watu wanaopokea na kutoa rushwa ili kupotosha haki na kupora ardhi, mali za wananchi maskini, wanaonekana kama mashujaa na mfano wa kuigwa katika jamii. Wengi wanahoji kwanini hatuendelei ikilinganishwa na rasilimali nyingi tulizonazo, jibu ni rahisi tumekithiri katika rushwa.
Nchi ya China ambayo ni taifa kubwa duniani lenye uchumi imara, limefika hapo lilipo kwa sababu viongozi na raia wake wanatambua wazi madhara ya kuendekeza vitendo vya kupokea hongo. Sio ajabu kuona taifa hilo limejiwekea sera na sheria nzito za kupambana na rushwa ambazo hazichagui viongozi wala raia, wote wanawajibika mbele ya sheria.
Dawa ya rushwa sio kulaumiana au kunyosheana vidole na wengine kujiona watakatifu na rushwa haiwathiri, lakini mapambano haya yanahitaji utashi na dhamira ya dhati kwa kila raia. Tufahamu kuwa kupokea na kutoa rushwa ni tabia ambayo hujidhihirisha pale mtu anapotaka apewe fedha au vitu ili atimize au atimiziwe wajibu isivyo halali.
Katika mapambano haya tunatakiwa kushughulika na saikolojia za watu na sio matokeo ya kile kinachotendwa, ingawa adhabu ni sehemu ya kubadilisha tabia ya mtu.
Tufike mahali watanzania, kukataa rushwa kwa vitendo na kuangana pamoja kubadilishana tabia zetu ili wote tunufaike na rasilimali zetu kwa haki na usawa.
Mabadiliko yanaanza na wewe, kuwa sehemu ya mabadiliko katika nafasi uliyonayo ili taifa liepuke kuingia katika migogoro ambayo itakuwa vigumu kutoka. Rushwa hupofusha macho tusipoangalia tutatumbukia shimoni wote.